Tafuta

Vatican News
Injili ya Dominika ya Pili ya Mwaka A wa Kanisa :inamwonesha Yohane Mbatizaji akimshuhudia Yesu kuwa ndiye mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu. Injili ya Dominika ya Pili ya Mwaka A wa Kanisa :inamwonesha Yohane Mbatizaji akimshuhudia Yesu kuwa ndiye mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu. 

Mtumishi ni Bwana na mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu!

Somo la kwanza (Is 49:3,5-6),kifungu kinazungumzia juu ya mtumishi wa Bwana.Ni mtumishi anayetumwa kutimiza utume wake kwa mataifa yote.Somo la pili (1Kor 1:1-3),ni waraka wa mtume kwenda kwa waamini kuhusu maisha yao na uhusiano wao na Mungu.Injili (Yoh 1:29-34),inamwonesha Yohane Mbatizaji anamshuhudia Yesu kuwa ndiye mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu.

Na Padre William Bahitwa – Vatican

Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayasoma na kuyatafakari masomo ya dominika ya pili ya mwaka A wa Kanisa.

Somo la kwanza (Is 49:3,5-6) ni kutoka kitabu cha nabii Isaya. Ni kifungu kinachomzungumzia mtumishi wa Bwana na kimezoeleka zaidi kuitwa wimbo wa pili wa mtumishi wa Bwana. Katika wimbo huu, ni mtumishi mwenyewe anayeongea. Anajitambulisha kuwa ameitwa na kutumwa na Bwana na anatambulisha pia utume wake ambao Bwana amempa. Katika mwito wake, Bwana amemwita Israeli: “wewe u mtumishi wangu, Israeli”. Ni kana kwamba Mungu anasema “wewe ndiwe mtumishi wangu, wewe ndiwe Israeli”. Katika maneno haya nabii Isaya analitaja taifa zima la Israeli kama mtu mmoja, kama mtumishi wa Bwana ambaye anaitwa ili katika yeye Bwana atukuzwe. Ni hapa inapopatikana tafsiri kuwa mtumishi wa Bwana ambaye nabii Isaya anamzungumzia ni taifa zima la Israeli kama taifa teule la Mungu.

Mtumishi huyu kama, somo linavyoendelea kutuonesha, anautaja pia utume wake aliopewa. Utume huu ni kuziinua kabila za Yakobo na kuwa nuru kwa mataifa. Kabila za Yakobo ni makabila 12 ya Israeli. Ni namna nyingine ya kusema taifa zima la Israeli. Hapa mtumishi anaonesha kuwa anao utume wa kuufanya ndani ya Israeli yenyewe. Lakini pia anao utume wa kuufanya nje ya Israeli, yaani kwa watu wa mataifa. Na utume huo ni kuwa nuru. Sio kung’ara kwa utukufu wake bali kuangaza ili mataifa waone kile ambacho hawakuwa wamekiona awali, yaani uwepo wa Mungu kati yao. Utume wa kuwa nuru ni utume wa kuwa shahidi wa Mungu, kumshuhudia Mungu kwa mataifa. Tunachokiona katika somo hili ni kuwa Israeli ambaye anajipambanua kama mtumishi wa Bwana aliye na utume ndani na nje ya Israeli hakufanikiwa kuakisi unabii huu. Katika historia yake kama taifa alishindwa kuishi kadiri ya wito wake wa kuwa mtumishi wa Bwana. Ni katika mwanga huu, mtumishi huyu wa Bwana ameonekana kuwa ni Kristo ambaye kwa unabii huu wa Isaya alikuwa anatabiriwa. Ni Kristo aliyebeba kwa ukamilifu sura ya mtumishi wa Bwana na kutekeleza kwa ukamilifu utume wa kuwa nuru kwa Israeli na kwa mataifa yote.

Somo la pili (1Kor 1:1-3) ni kutoka katika waraka wa kwanza wa mtume Paulo kwa Wakorintho. Somo hili ni mwanzo wa waraka ambao Paulo aliwaandikia wakorintho. Ni mwanzo wa kawaida kabisa wa uandishi wa barua katika wakati wa Paulo. Kama ilivyokuwa imezoeleka Paulo anaanza kwa kueleza barua imetoka kwa nani na nani (Paulo na msaidizi wake Sosthenes), kwenda kwa nani (wakristo wa Korintho) na anahitimisha utangulizi huo kwa kuwasalimu – neema na amani viwe kwenu. Lakini katika mwanzo huu wa kawaida wa barua, Paulo ameweka baadhi ya maneno yanayotafakarisha na kuonesha kuwa waraka wanaokwenda kuusoma sio wa kawaida kama walivyozoea. Ni waraka wa mtume kwenda kwa waamini kuhusu maisha yao na uhusiano wao na Mungu. Na ni kwa sababu hiyo na sisi tunausoma hata leo katika liturujia kwa sababu tunashiriki maisha yaleyale ya kiimani waliyoyaishi wakorintho na tunatazamia tumaini lilelile walilokuwa nao hao wakristo wenzetu.

Baadhi ya mawazo ya pekee yanayojitokeza ni kwamba Paulo anawaita wakristo walioko Korintho kuwa ni kanisa. Wakristo wa Korintho walikuwa ni jumuiya ndogo iliyokuwa ikikusanyika katika familia au miji ya watu kusali: kusikiliza Neno na kuumega mkate. Walifanya hivyo kama sisi tunavyokusanyika katika jumuiya zetu ndogondogo za kikristo kwenye miji na familia za wakristo wenzetu. Huo ndio mkusanyiko ambao Paulo anauita Kanisa. Nasi anatuonesha kuwa kanisa hatuanzi kuliishi parokiani bali kanisa linaanza katika hatua za chini, familia na jumuiya ndogondogo. Hatupaswi kuzipuuzia kwani ni kanisa na ndio msingi wa uhalisia wa kanisa unaojionesha katika parokia na Jimbo. Wazo la pili ni kwamba Paulo anawaita wakorintho watu waliotakaswa na watakatifu. Ni watu waliotakaswa kwa ubatizo kwa sababu ubatizo unamuweka mtu kuwa wakfu kwa Mungu na kumpa wito na hadhi ya utakatifu. Kumbe tangu mwanzo wa barua Paulo anawakumbusha wakorintho kuwa wao hasa ni akina nani na nafasi yao ni ipi katika jamii na kati ya watu wanaoishi nao. Wao ni watu waliowekwa wakfu na kuitwa kuwa watakatifu. Na ndivyo na sisi tulivyo na tunavyoitwa kuwa.

Injili (Yoh 1:29-34) ni kutoka kwa mwinjili Yohane na inamwonesha Yohane Mbatizaji anamshuhudia Yesu kuwa ndiye mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu. Mapokeo ya waisraeli katika Agano la Kale yametaja katika sehemu kuu tatu mwanakondoo wa Mungu, yaani mwanakondoo aliyetolewa na Mungu kwa ajili ya tukio maalumu. Wa kwanza ni mwanakondoo ambaye Mungu alimwonesha Abrahamu alipokuwa anataka kumtoa Isaka sadaka (Mwa 22:1-14), wa pili ni mwanakondoo ambaye Mungu aliwaagiza waisraeli kumchinja na kupaka damu yake kwenye miimo ya milango usiku ule wa kutoka Misri (Kut. 12:5 nk) na wa tatu ni mtumishi wa Bwana aliyekuwa kama mwanakondoo anayepelekwa machinjioni (Is 53:7). Katika mapokeo hayo Mungu ameonesha matendo yake makuu kupitia mwanakondoo.

Yohane kumtaja Yesu kama mwanakondoo ni kumuonesha kama yule anayekuja kutenda makuu ya Mungu kama walivyodhihirisha wanakondoo waliotangulia. Tena yeye Yesu anayaunganisha pamoja katika nafsi yake yote yaliytendwa kwa njia ya wanakondoo hao. Hata hivyo yeye anakuwa ndiye mwanakondoo haswa, mwanakondoo wa kweli, asiye na doa wala hatia na anayeondoa dhambi ya ulimwengu, kwa maana wote waliotangulia hakuna hata mmoja aliyetajwa kuondoa dhambi ya ulimwengu. Injili zinamtaja Yohane Mbatizaji kama nabii aliyemtolea ushuhuda Yesu na kumtambulisha alipokuja. Ushuhuda anaoutoa Yohane Mbatizaji leo kwa hakika ndio kilele cha ushuhuda wote alioutoa kwake.

Tafakari

Ndugu msomaji na msikilizaji wa Vatican News, masomo ya dominika hii yanatupa tafakari juu ya nafasi ya ushuhuda tuliyonayo kama wakristo. Sisi tuliowekwa wakfu kwa ubatizo na kuitwa kuwa watakatifu tunaalikwa kuwa mashahidi wa Kristo, kumkiri na kumtangaza kwa maisha yetu. Katika ushuhuda alioutoa Yohane Mbatizaji kwa Yesu, alimtaja kama ndiye mwanakondoo aondoaye dhambi ya ulimwengu. Inafaa pia kutafakari ni nini maana na matokeo ya dhambi ya ulimwengu katika maisha yetu ya kumshuhudia Kristo. Yohane hataji “dhambi za ulimwengu” bali dhambi ya ulimwengu. Hii siyo ile dhambi ya mtu mmoja moja bali ni dhambi katika katika ujumla wake. Hali ya ulimwengu kumgeuzia Mungu kisogo. Ni uharibifu wa ulimwengu katika ujumla wake: upotevu wake, ukosefu wake, uasi wake nk., kama dhambi ya asili. Tunaweza kuiona kama dhambi ya mfumo au hata ya jamii ambayo kwa namna moja au nyingine inahusiana na dhambi ya mtu mmoja mmoja. Jamii inaweza kujikuta katika mazingira ambapo kila aliye chini yake hawezi kujiepusha na dhambi fulani. Iwe ni dhambi iliyohalalishwa au ile inayolindwa kimfumo na jamii hiyo. Katika nafasi nyingine dhambi ambayo mtu mmoja mmoja anaifanya inaweza kukua ikawa dhambi ya jamii au ya kimfumo. Yote katika yote dhambi ya ulimwengu inakuwa ni ile dhambi inayopita uwezo wa ulimwengu, jamii au mfumo kujikwamua nayo.

Hali hii pia inaweza kujitokeza katika mtu mmoja mmoja. Pale ambapo katika maisha mtu anakuza kilema fulani cha dhambi au anakipuuzia na kilema hicho kinakua na kuzidi kukua hadi kufika mahala kinaota mizizi na kumlemea mtu kiasi ambacho anakosa uwezo tena wa kujikwamua nacho. Yohane Mbatizaji anamtambulisha kwetu leo Yesu kama ile nguvu ya nje tena nguvu itokayo kwa Mungu mwenyewe iliyo na uwezo wa kutusaidia na kutukwamua kutoka dhambi zinazozidi uwezo wetu kuondokana nazo. Ushahidi huu wa Yohana ndio ambao adhimisho la Misa linautanganza, pale Padre anapoonesha Ekaristi na kutamka Tazama mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu”. Ni tamko linalotukumbusha kuwa nasi kwa njia ya adhimisho la Misa tunakutana na nguvu hiyo inayoweza kutuweka huru. Tuitumainie, tuijongee ituokoe.

18 January 2020, 10:19