Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Paul Desfarges wa Jimbo kuu la Algiers amewaandikia waamini wake waraka wa kichungaji mwaka mmoja tangu wafiadini wa Oran walipotangazwa kuwa ni Wemyeheri Askofu mkuu Paul Desfarges wa Jimbo kuu la Algiers amewaandikia waamini wake waraka wa kichungaji mwaka mmoja tangu wafiadini wa Oran walipotangazwa kuwa ni Wemyeheri 

Waraka wa Kichungaji Kutoka Jimbo kuu la Algiers: Ushuhuda

Wafiadini ni vyombo vya amani na mashuhuda wa umoja na udugu, kielelezo cha utukufu wa Mungu aliye hai! Ni watu waliosimika maisha yao katika sala na tafakari ya Neno la Mungu, mambo yaliyomwilishwa katika Injili ya huduma kwa watu wa Mungu nchini Algeria. Wafiadini hawa wanaendeleza Injili ya huruma na msamaha, chachu mpya ya upatanisho, haki na amani. MAJADILIANO!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, tarehe 8 Desemba 2018 yaliacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za watu wa familia ya Mungu nchini Algeria, inayoendelea kujitahidi kumwilisha moyo wa udugu, urafiki na huduma katika uhalisia wa maisha. Hii ni changamoto na mwaliko wa kuganga na kuponya madonda ya kihistoria yaliyopita, tayari kujenga na kudumisha sanaa na utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana kama alivyofanya Askofu Pierre Claverie wa Oran pamoja na watawa wenzake 18 waliotangazwa kuwa Wenyeheri, huko Algeria. Hawa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika huduma. Ni watu walioteseka, wakanyanyaswa, kudhulumiwa na hata kuuwawa kati ya mwaka 1994 hadi mwaka 1996 wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Algeria.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko wakati wa kuwatangaza wafiadini hawa kuwa Mwenyeheri, mifano bora ya kuigwa katika imani inayomwilishwa katika Injili ya huduma ya upendo, inayowachangamotisha wananchi wa Algeria kuishi kwa pamoja katika amani na kwamba, Kanisa linataka kutangaza na kushuhudia: Injili ya upendo inayosimikwa katika majadiliano ya kidini, amani, utulivu na urafiki! Askofu mkuu Paul Desfarges wa Jimbo kuu la Algiers anasema, Wenyeheri hawa wapya ni neema kwa familia ya Mungu nchini Algeria, nchi ambayo tangu karne ya kwanza, imeshuhudia damu ya wafiadini, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, hadi dakika ya mwisho, daima wakiendelea kuchuchumilia utakatifu wa maisha unaomwilishwa katika uhalisia wa kila siku, kama alama ya uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake.

Upendo wa Kristo unawadai kusamehe na kusahau, kwa kuendeleza majadiliano ya kidini. Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Paul Desfarges, ameandika waraka wa kichungaji kama sehemu ya maadhimisho ya mwaka mmoja tangu, Mama Kanisa amtangaze Askofu Pierre Claverie wa Oran pamoja na watawa wenzake 18 kuwa Wenyeheri. Katika waraka huu anakazia pamoja na mambo mengine: sadaka na majitoleo kwa ajili ya kuimarisha umoja na mafungamano ya kijamii nchini Algeria. Kanisa nchini Algeria limekuwa na wafiadini na waungama imani na huu kwa sasa ndio utambulisho wao. Maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Algeria ni utambulisho wa sadaka ambayo Kristo Yesu ameitoa kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Algeria. Mpango mkakati wa shughuli za kichungaji nchini Algeria unawataka Wakristo kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano yao na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala, ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaomwilishwa katika huduma makini kwa jirani, lakini zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Waamini wanapaswa kukuza na kudumisha ndani mwao moyo wa upendo na ukarimu; kwa kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini kama sehemu ya ujenzi wa udugu wa binadamu; ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa watu wa Mungu nchini Algeria. Waamini wajenge mazoea ya kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya wananchi wa Algeria. Majadiliano ya kidini yanapaswa kuzama zaidi katika undani wa maisha ya watu wa Mungu na kamwe yasibaki yakiwa yanaelea elea katika ombwe, kiasi hata cha kuonekana kuwa ni mambo ya kisaokolojia na kijamii zaidi. Majadiliano ya kidini yawasaidie waamini kutambua kwamba, wanashiriki katika majadiliano yatakayowawezesha kushiriki pia katika wokovu wa roho zao ambayo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kumbe, majadiliano ya kidini ndani ya Kanisa Katoliki ni changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee ni mchakato wa: haki jamii, tunu msingi za kimaadili; amani, uhuru wa kuabudu pamoja na kuendeleza haki msingi za binadamu. Ikumbukwe kwamba, binadamu wote ni sawa kwa sababu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Inawezekana kabisa katika uhalisia wa maisha, Wakristo wakawa wamekwaruzana na waamini wa dini ya Kiislam. Jambo la msingi hapa ni kukumbuka kwamba, kila dini ina  magonjwa yake. Hija ya maisha iliyowakutanisha na Kristo Yesu, imewafungua macho ya maisha yao ya kiroho, kiasi kwamba, wanaweza kuwa na mwono mpana zaidi. Kuna haja ya kujifunza kujenga na kudumisha madaraja ya kukutana, kushirikiana na kupendana na waaminiwa dini ya Kiislam ambao ni wengi zaidi nchini Algeria. Kuna baadhi ya waamini wa dini ya Kiislam ambao wamejisadaka kwa ajili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu ilitiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu ni mfano bora wa kuigwa kwa watu wanaojisadaka kwa ajili ya haki, amani, ustawi na mafao ya wengi.

Hati hii ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Baba Mtakatifu Francisko anasema majadiliano ya kidini si alama ya udhaifu, bali ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Majadiliano ya kidini hayana mbadala, kwani waamini wa dini zote wanapaswa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha utamaduni wa ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu, ili hatimaye, familia ya binadamu iweze kukua na kukomaa katika mchakato wa upatanisho, kwa kuwakirimia watu matumaini yanayobubujika kutoka katika huduma. Dini mbali mbali zina uwezo wa kujenga utamaduni wa kuwakutanisha watu ili kujenga na kuimarisha umoja. Hati hii ni kikolezo cha ujenzi wa misingi ya usawa, haki, amani na maridhiano duniani. Askofu mkuu Paul Desfarges wa Jimbo kuu la Algiers anasema Kanisa nchini Algeria linao mfano bora wa kuigwa katika majadiliano na mahusiano ya kidini nao ni Mwenyeheri Charles Eugène de Foucauld aliyetangazwa kuwa Mwenyeheri na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI hapo tarehe 13 Novemba 2005. Katika maisha na utume wake alikazia umuhimu wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika maisha ya tafakari na sala inayomwilishwa katika huduma kwa wagonjwa, wafungwa, wazee, walemavu, wakimbizi na wahamiaji.

Askofu mkuu Paul Desfarges wa Jimbo kuu la Algiers anakazia pia nafasi ya vijana wa kizazi kipya katika maisha na utume wa Kanisa kwani wao ni leo ya Mungu inayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha. Kumbe, wafiadini hawa ni vyombo vya amani na mashuhuda wa umoja na udugu, kielelezo cha utukufu wa Mungu aliye hai!  Ni watu waliosimika maisha yao katika sala na tafakari ya Neno la Mungu, mambo yaliyomwilishwa katika Injili ya huduma kwa watu wa Mungu nchini Algeria. Wafiadini hawa wanaendeleza Injili ya huruma ya Mungu na msamaha, chachu ya maisha mapya yanayofumbatwa katika mchakato wa upatanisho, haki na amani. Yote haya yanahitaji majiundo makini ya kitaalimungu na maisha ya kiroho; kwa kukazia majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam nchini Algeria. Wakristo wajitahidi kufahamu mambo msingi katika imani na dini ya Kiislam, ili waweze kupendana, kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao msingi. Wajibidiishe kufahamu taalimungu na historia ya dini ya Kiislam, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Algeria.

Mashuhuda Algeria
05 December 2019, 16:19