Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki Chad katika Waraka wake wa Noeli kwa Mwaka 2019 linakazia umuhimu wa ujenzi wa Jamii inayosimikwa katika misingi ya haki na amani. Baraza la Maaskofu Katoliki Chad katika Waraka wake wa Noeli kwa Mwaka 2019 linakazia umuhimu wa ujenzi wa Jamii inayosimikwa katika misingi ya haki na amani.  (AFP or licensors)

Waraka wa Baraza la Maaskofu Katoliki Chad: Haki na Amani!

Baraza la Maaskofu Katoliki Chad katika ujumbe wake wa Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2019 wanataka watu wa Mungu nchini humo kujizatiti katika ujenzi wa jamii inayosmikwa katika misingi ya haki na amani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa kwa upande wake, litaendelea kuwa ni sauti ya kinabii kwa wale wasiokuwa na sauti. Mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Mtakatifu Yohane wa XXIII katika Waraka wake wa Kitume “Pacem in terris” yaani “amani duniani” anafafanua kwa kina na mapana maana ya haki na wajibu kama sehemu muhimu sana ya mchakato wa ujenzi wa amani duniani. Anasema, watu wana haki ya kuishi na kuwa na maisha mazuri. Kuna haki zinazohusu tunu za kimaadili na kiutamaduni. Kutokana na haki ya asili, watu wote wana haki ya kushiriki ukuaji wa ustaarabu; na kwa hiyo ni lazima kila mtu aweze kupata elimu nzuri ya msingi, na mafunzo ya ufundi na ya elimu ya juu yanayolingana na kiwango cha maendeleo ya elimu cha nchi yake. Ni lazima kila bidii na juhudi zifanywe ili kila mtu aweze kufikia viwango vya juu vya elimu, kadiri iwezekanavyo kulingana na karama zake, na kuchukua dhima na majukumu katika jamii zinazolingana na karama hizo za maumbile na ujuzi alioupata. Kuna haki ya kila mtu ya kumwabudu Mungu kadiri ya kanuni nyofu ya dhamiri yake, na kuungama dini yake kibinafsi na hadharani.

Watu wana pia haki ya kuchagua hali ya kuishi wanayoipenda zaidi; kwa hiyo wana haki ya kujenga familia yao, ambamo mume na mke wana usawa wa haki na wajibu, au ya kufuata wito wa upadre au wa utawa.  Kadiri ya haki ya asili mtu ana haki ya kuwa na kazi, na pia ya kuweza kutumia kwa uhuru uwezo wake binafsi katika kazi. Haki hizo lazima ziungane na haki ya kufanya kazi katika hali na mazingira visivyoathiri uzima wa mwili au maadili ya mtu, wala visivyodhuru mchakato wa kukua kwa vijana hadi wafikie ukomavu wa utu. Haki hizo na wajibu hupata asili yao, nguvu zao na kutokuharibika kwao kutoka sheria ya maumbile (natural law), ambayo huhakikisha haki na kuamuru wajibu. Hivyo, kwa mfano, haki ya mtu kuishi inahusisha wajibu wa kulinda maisha yake; haki ya kuwa na maisha mazuri inahusisha wajibu wa kuishi kwa kujiheshimu; haki ya kuwa huru katika kutafuta ukweli, inaendana na wajibu wa kufanya juhudi katika kutafuta kwa upana na kina huo ukweli.

Amani ni msingi wa wema, heshima na maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu; ni paji na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha na kumwajibisha binadamu. Amani ni tunda la upendo linalopaswa kuboreshwa kwa njia ya malezi ya dhamiri nyofu; ukweli na uhuru; usalama wa raia na mali zao; kwa kulinda na kuheshimu utu wa binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi. Kanuni ya kwamba, kila mtu ni binadamu, yaani, nafsi iliyo na akili na utashi huru; na kila mtu ana haki na wajibu ambavyo vyote vinatokana moja kwa moja na asili yake hiyo inapaswa kuzingatiwa. Kwa hiyo haki na wajibu ni vya watu wote, visivyovunjika wala kubatilika. Kwa ufupi, amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo! Amani inatishiwa sana na mashindano; utengenezaji na biashara ya silaha pamoja na ulimbikizaji wa silaha duniani! Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani duniani!

Ni katika muktadha huu Baraza la Maaskofu Katoliki Chad katika ujumbe wake wa Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2019 linataka watu wa Mungu nchini humo kujizatiti katika ujenzi wa jamii inayosmikwa katika misingi ya haki na amani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa kwa upande wake, litaendelea kuwa ni sauti ya kinabii kwa wale wasiokuwa na sauti. Mauaji ya watu wasiokuwa na hatia pamoja na mashambulizi ya kigaidi ni mambo yanayohatarisha sana umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii nchini Chad. Watu wanapaswa kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao msingi, kwa kulinda, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni changamoto ya kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu kwa kuheshimu pia Katiba ya nchi ambayo kimsingi ni sheria mama! Baraza la Maaskofu Katoliki Chad linasikitika kusema kwamba, katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na mmong’onyoko mkubwa wa kanuni maadili na utu wema na matokeo yake ni kushamiri kwa rushwa na ufisadi pamoja na kuongezeka kwa maskini, wakati kundi la watu wachache ndani ya jamii wanakula na kusaza!

Siasa kimekuwa ni kichaka kwa wizi na ubadhirifu wa mali ya umma, utawala wa sheria, umetoweka na wajanja wachache wanaendelea kukwapua rasilimali na utajiri wa nchi kwa mafao binafsi. Baraza la Maaskofu Katoliki Chad linasema, kuna haja kwa familia ya Mungu nchini humo kuanza kujikita katika ujenzi wa Chad mpya. Kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko: Siasa safi ni msingi wa maendeleo endelevu na fungamani; demokrasia shirikishi na uongozi bora unaojikita katika hoja zenye mashiko na huduma kwa wananchi. Siasa safi inafumbatwa katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi unaowashirikisha wadau mbali mbali mbali katika jamii; marika pamoja na tamaduni, daima wakijitahidi kujenga imani kati yao kama sehemu ya kukuza na kudumisha amani. Siasa ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu na kwamba, siasa safi hutekelezwa kwa kufuata katiba, sheria na kanuni maadili; mambo msingi katika kukuza na kudumisha misingi ya amani, haki, ustawi na maendeleo ya wengi.

Siasa safi ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo katika jamii; ni matunda ya ukomavu yanayojikita katika uongozi bora, maridhiano, utawala wa sheria, uvumilivu, uaminifu na bidii. Kamwe tofauti za kiitikadi kisiwe ni chanzo cha vita, kinzani, vurugu na mipasuko ya kijamii inayowatumbukiza watu kwenye majanga na maafa makubwa kama inavyojitokeza kwa sasa nchini Chad. Umefika wakati wa kusimama kidete kulinda, kudumisha na kuendeleza misingi ya haki, amani, usawa na maridhiano kati ya wananchi wa Chad. Baraza la Maaskofu Katoliki Chad linaitaka Serikali pamoja na wadau mbali mbali wa elimu kuhakikisha kwamba, wanaboresha elimu nchini humo, ili kuwasaidia wananchi kupambana na ujinga, umaskini na maradhi. Sekta ya elimu isipokuwa na mvuto wala mashiko, matokeo yake ni kuwasukumizia vijana katika mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo na matokeo yake ni majanga na maafa makubwa kwa taifa.

Vijana wasipokuwa na mwelekeo na matumaini ya leo na kesho iliyo bora watachanganyikiwa na kuzama kwenye ugonjwa sonona matokeo yake watajikatia tamaa na hatimaye, kupoteza dira na mwongozo wa maisha. Vijana wapewe elimu itakayowasaidia kujiajiri wao wenyewe badala ya kutegemea ajira rasmi ambazo kwa sasa “zimeota miguu” yaani hazipatikani. Sanjari na hili, waalimu wajengewe pia mazingira bora ya kuishi na kufundishia; wapate ujira utakaowawezesha kumudu walau gharama ya maisha. Waalimu ni walezi  wanaopaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa. Baraza la Maaskofu Katoliki Chad linahitimisha ujumbe wake wa Noeli kwa kuzama katika mambo msingi yanayobainishwa katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu iliyotiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.

Huu ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Baraza la Maaskofu Katoliki Chad linawataka waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa kuchota nguvu yao kutoka katika imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Maaskofu Chad

 

 

16 December 2019, 12:40