Tafuta

Vatican News
Patriaki Bartolomeo wa kwanza katika ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2019: Upyaisho wa maisha ya kiroho na utume wa Kanisa kwa vijana wa kizazi kipya! Patriaki Bartolomeo wa kwanza katika ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2019: Upyaisho wa maisha ya kiroho na utume wa Kanisa kwa vijana wa kizazi kipya!  (ANSA)

Ujumbe wa Noeli 2019: Upyaisho wa maisha: Mwaka wa Vijana 2020!

Kanisa la Kiothodox katika maadhimisho ya Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2019 linatangaza kwamba mwaka 2020 ni mwaka maalum kwa ajili ya upyaisho wa shughuli za kichungaji katika maisha ya kiroho pamoja na Kanisa kujielekeza zaidi katika utume kwa vijana wa kizazi kipya. Huu ni mwaliko kwa watu wote wa Mungu kuhakikisha kwamba, wanajizatiti katika kutekeleza malengo haya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Noeli kwa Mwaka 2019 anasema, Mwaka 2020 ni mwaka ambao Kanisa lake limeutenga maalum kwa ajili ya upyaisho wa shughuli za kichungaji katika maisha ya kiroho pamoja na kujielekeza zaidi katika utume kwa vijana wa kizazi kipya. Huu ni mchakato wa kuwaendea ili kukutana na vijana kwenye maskani yao kama rafiki na wandani wa safari na kamwe si kama Mahakimu. Kanisa linataka kuwaendea vijana kama alivyofanya Kristo Yesu mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya Kondoo wake. Kanisa linapaswa kuwa makini daima, kwa kusoma alama za nyakati ili kutambua na kujibu mahitaji msingi ya vijana wa kizazi kipya. Mama Kanisa anapaswa kutambua mahitaji msingi ya maisha ya kiroho kwa vijana wa kizazi kipya mintarafu mazingira yao ya maisha ya kijamii.

Katika muktadha wa Mapokeo ya Kanisa, Patriaki Bartolomeo wa kwanza anataka kuwapatia vijana msaada mzito unaosimikwa katika ukweli na uhuru unaoleta ukombozi unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kwa njia hii, Yesu mwenyewe anawaweka huru zaidi. Kanisa la Kiothodox katika maadhimisho ya Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2019 linatangaza wazi kwamba mwaka 2020 ni mwaka maalum kwa ajili ya upyaisho shughuli za kichungaji katika maisha ya kiroho pamoja na Kanisa kujielekeza zaidi katika utume kwa vijana wa kizazi kipya. Huu ni mwaliko kwa watu wote wa Mungu kuhakikisha kwamba, wanajizatiti katika kutekeleza malengo yaliyobainishwa kwa ajili ya Mwaka 2020 na kwamba, nia hii njema inapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Huu ni upendeleo maalum kwa ajili ya utume wa Kanisa kwa vijana, ili kuwajengea vijana mwono sahihi wa maisha, kwa kuwa na imani thabiti inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu pamoja na nguvu ya uhuru wa binadamu.

Kiini cha utume wa Kanisa kwa ajili ya vijana ni: Utu, heshima na haki msingi za binadamu. Vijana wanapaswa kuchakarika ili kuweza kujipatia mahitaji yao msingi. Wajitahidi kupata mambo msingi yanayoridhisha matamanio yao halali ya maisha, yaani upendo kwa Mungu na jirani. Huu si upendo ndoana wa “kula na kulipa” eti ndio mtindo wa kisasa. Kanisa linatambua na kukiri kwamba, vijana wanayo mambo mengi wanayotamani katika maisha yao. Kumbe, ni wajibu wa Mama Kanisa kuwasaidia na kuwaongoza vijana ili kufanya maamuzi magumu katika maisha yao, kwa kuchagua mambo msingi yatakatowasaidia kukua na kukomaa katika utu, heshima na karama zao mbali mbali. Mwaka 2020 unapania kuwasaidia vijana kugundua na kutambua karama zao, ili waweze kuzitumia kwa ajili yao wenyewe na kwa mafao, ustawi na maendeleo ya jirani zao. Karama ni zawadi ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia kila mja wake.

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Noeli, yaani kuzaliwa kwa Mtoto Yesu ni muda muafaka wa kumshangalia kwa nyimbo na tenzi za rohoni, kwa sababu kwa njia ya huruma na upendo wake usiokuwa na kifani, ameamua kujinyenyekesha katika Fumbo la Umwilisho, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, ili hatimaye, kumfungulia lango la maisha na uzima wa milele. Mama Kanisa anashangilia na kumtukuza Mwana wa Mungu akitazamia na kutumainia utukufu wa Ufalme wa Mungu, kwa kumtolea ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Ushuhuda huu unapaswa kuwa ni kielelezo cha imani tendaji, matumaini thabiti na upendo wa dhati. Waamini waupende ulimwengu, lakini wasimezwe na malimwengu, kwa kuwa tayari kuyatakatifuza malimwengu kwa tunu msingi za Kiinjili na kiutu.

Mama Kanisa anataka vijana wajenge utamaduni wa kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha. Kanisa kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema linataka kuwaganga kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini, kwa kuwa ni majirani wema kwa watu wanaoteseka: kiroho na kimwili, ili kwa njia ya uwepo na huduma yao, waweze kuasha matumaini mapya kwa wale waliokata tamaa! Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, kwa kuganga na kuponya madonda ya ustaarabu wa ulimwengu mamboleo, Kanisa litaweza kusaidia kwa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu kuangaza akili na nyoyo za wamini kutoa ushuhuda wenye mvuto kwa maneno na matendo adili ambayo kimsingi ni chemchemi ya matumaini. Roho Mtakatifu anaendelea kutenda katika maisha ya waamini, kwani yeye ndiye mleta uzima, chemchemi ya wema, karama na maisha tele.

Mkristo anayetembea katika mwanga wa Roho Mtakatifu, anao uwezo wa kuushuhudia mwanga huo kwa jirani zake, kwa kuonesha urafiki na upendo wa dhati, daima akijitahidi kutafuta kile kilichochema, kizuri na kitakatifu. Mwaliko huu kwa vijana unatambua na kukiri vizingiti na kinzani nyingi zinazoweza kujitokeza katika maisha, kama Fumbo la Umwilisho linalofafanulia na Injili takatifu: Hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni! Ulimwengu mamboleo umegubikwa sana na ubinafsi pamoja na uchoyo mambo yanayovuruga umoja na mafungamano ya kijamii; upendo na mshikamano wa dhati, kiasi kwamba, hata urafiki miongoni mwa vijana hauwezi kuwa na mizizi inayozama na kujikita katika akili na nyoyo za vijana wa kizazi kipya. Huu ndio urafiki wa kujisikia, usiokuwa na mvuto wala mashiko. Sera mbali mbali na uchumi mamboleo zinawaacha watu wengi wakiwa watupu kutoka katika undani wao, kwa sababu ni uchumi usiozingatia mahitaji msingi ya binadamu, hali inayodumaza nguvu za ugunduzi.

Vijana ndio waathirika wakubwa wa maendeleo ya sayansi na teknolojia, licha ya mafao makubwa yanayopatikana katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya binadamu. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanataka kuwaaminisha vijana kwamba, kwa sasa wanaishi “Paradiso” na kusahau kwamba, vijana ni jeuri na matumaini ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Kumbe, wanapaswa kuwa makini ili kamwe wasimezwe na malimwengu na huko watakiona “kilicho mng’oa Kanga manyoya”. Vijana ni amana na utajiri wa Kanisa, wanapaswa kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa nguvu zote, wakitambua kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa imani tendaji. Ni katika muktadha huu Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Noeli kwa Mwaka 2019, anapenda kuwapongeza viongozi mbali mbali wa Kanisa la Kiorthodox walioteuliwa kuwaongoza watu wa Mungu huko ugenini, yaani “diaspora” kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa upyaisho wa maisha ya shughuli za kichungaji katika maisha ya kiroho pamoja na kujielekeza zaidi katika utume kwa vijana wa kizazi kipya.

Vijana wanapaswa kupyaisha dhamiri zao nyofu, kwa kutambua kwamba, wao ni Wakristo, kwa kudumisha utamaduni wa kushiriki kikamilifu katika Liturujia Takatifu; umuhimu wa maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa yanayojikita katika ushuhuda wa maisha kijumuiya. Mkazo zaidi ni katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja na mambo ya nyakati “Eschaton”. Vijana watambue kwamba, Kanisa ni Fumbo la Mwili wa Kristo na wala si chama cha kisiasa wala muunganiko wa Wakristo. Huu ni mwaliko kwa wakleri sehemu mbali mbali za dunia, kujizatiti katika shughuli za kichungaji zinazowawajibisha kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya vijana wa kizazi kipya kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu mwenyewe katika Fumbo la Umwilisho “Kenosis”. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli anahitimisha ujumbe wake kwa maadhimisho ya Noeli kwa Mwaka 2019 kwa kuwatakia heri na baraka kwa Sherehe ya Noeli na Mwaka Mpya 2020.

Sherehe hii ni kumbu kumbu hai ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu kiasi cha kuamua kuwa kati pamoja na waja wake. Yeye ndiye Emmanuel, yaani “Mungu pamoja nasi”. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, ameamua kuwa sawa na binadamu katika mambo yote isipokuwa hakutenda dhambi.

Patriaki: Ujumbe wa Noeli 2019
24 December 2019, 16:44