Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki Canada limetoa Tamko Kuhusu Nyanyaso na Dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana ili kudumisha: amani, matumaini na mafungamano ya kijamii. Baraza la Maaskofu Katoliki Canada limetoa Tamko Kuhusu Nyanyaso na Dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana ili kudumisha: amani, matumaini na mafungamano ya kijamii.  (ANSA)

Tamko dhidi ya ukatili na nyanyaso za kijinsia nchini Canada

Kanisa linakumbuka tukio la mauaji ya wanawake wale ili kuboresha haki msingi za wanawake nchini Canada. Kuna kundi kubwa la wanawake ambao wamekuwa ni waathirika wa ukatili wa kimtandao. Kuna wanawake na wasichana ambao wametumbukizwa kwenye mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo pamoja na vipigo vya wanawake majumbani. Haki jami inahitajika hapa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Umoja wa Mataifa unakiri kwamba, unyanyasaji wa kijinsia na masuala ya rushwa ya ngono maeneo ya kazi dhidi ya wanawake na wasichana ni matokeo ya kukomaa kwa mfumo dume unaopelekea ukosefu wa usawa wa kijinsia na hivyo kuchochea kushamiri kwa tabia chafu ya ubakaji inayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za wanawake na wasichana. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kupinga tabia ya unyanyapaa, dhana na tamaduni potofu kuhusu wanawake, pamoja na kuhakikisha kwamba, nyanyaso na dhuluma dhidi ya wanawake zinatolewa taarifa ili wahusika waweze kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria, ili haki iweze kushika mkondo wake. Baraza la Maaskofu Katoliki Canada, miaka thelathini iliyopita, kuna wanawake 14 waliuwawa kikatili nchini Canada, kiasi cha kuacha majonzi na masikitiko makubwa miongoni mwa watu wa Mungu nchini Canada. Kanisa linataka kusimama kidete kupinga tabia ya ukatili, nyanyaso na dhuluma dhidi ya wanawake!

Kanisa linakumbuka tukio la mauaji ya wanawake wale ili kuboresha haki msingi za wanawake nchini Canada. Kuna kundi kubwa la wanawake ambao wamekuwa ni waathirika wa ukatili wa kimtandao, mkondo wa kusafirishia picha za ngono, udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsia. Kuna wanawake na wasichana ambao wametumbukizwa kwenye mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo pamoja na vipigo vya wanawake majumbani. Haya ni mambo ambayo yanakwenda kinyume kabisa cha utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Kuna aina mbali mbali za ubaguzi zinazoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia, hali inayochangia kuathiri mafungamano ya kijamii, kitaifa na kimataifa. Yote haya ni matukio yanayohitaji Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa kukuza na kudumisha haki, tayari kuanza mchakato wa msamaha na uponyaji wa ndani.

Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, iwe ni chachu kwa waamini kusimama kidete kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Simulizi mbali mbali za Maandiko Matakatifu zinaonesha mchango wa wanawake katika maisha na utume wa Yesu Kristo na hata kwa Kanisa katika nyakati hizi. Kanisa linasikitishwa na nyanyaso ambazo zimetendwa na viongozi wa Kanisa dhidi ya wanawake. Huu ni wakati wa kuhakikisha kwamba, matukio kama haya hayajirudii tena ndani ya Kanisa. Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Canada linapenda kujielekeza zaidi katika sera na mikakati ya kuzuia nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa kwa kukazia elimu makini pamoja na uragibishaji wa utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kudumisha imani, matumaini na mapendo miongoni mwa watu wa Mungu, ili kukuza amani, umoja na mafungamano ya kijamii.

Wanawake

 

03 December 2019, 11:48