Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 4 ya Kipindi cha Majilio: Mtakatifu Yosefu Mtu wa haki! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 4 ya Kipindi cha Majilio: Mtakatifu Yosefu Mtu wa haki! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 4 ya Majilio: Mtakatifu Yosefu, Mtu wa haki!

Mtakatifu Yosefu, mume wa Bikira Maria amekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha mpango wa Mungu wa kumleta duniani mwanae Yesu Kristo kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu. Yosefu alimpokea Maria kama mke wake na hivi kumuandalia mazingira mazuri ya kuwa mama wa Mungu na pia kumwandalia mtoto Yesu mazingira mazuri ya kuzaliwa na kukua katika familia.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

 

Amani na Salama! Mwana wa Bikira Maria ana majina mawili, la kwanza ni lile lililotumika katika maisha yake ya kawaida labda aliloitwa na wazazi, ndugu, jamaa na marafiki na hata sisi wafuasi wake mpaka leo ndilo Yesu, likiwa na maana mkombozi, na la pili ni lile tunalolisikia katika Somo la Nabii Isaya na pia linanukuliwa katika sehemu ya Injli ya leo maneno ya malaika kwa Yusufu ndilo Emanueli, yaani Mungu pamoja nasi. Uzushi mkubwa wa kwanza katika mafundisho ya kiimani au “heresia” katika karne ile ya nne yalifanywa na Apolinari wa Laodikea, ambaye alifundisha kuwa Yesu alikuwa na mwili wa kibinadamu ila hakuwa na moyo au roho ya kibinadamu. Ilikuwa ni hofu na mashaka yake kuwa kukiri kuwa Yesu ni mtu kweli kwa mwili na roho ni sawa na kutokukiri Umungu wake. Kwake Yesu hakuwa sawa nasi, hivyo kwake jina sahihi ni Emanueli, ni Mungu pamoja nasi ila si sawa nasi katika ubinadamu!

Mwinjili Yohane anamtambulisha Yesu katika “prolojia” yake kama Neno aliyefanyika mwili. Yohane 1:14. Neno mwili haliwakilishi tu mwili wa nyama, ila ubinadamu katika ukamilifu wake na hali zake zote iwe hata unyonge wake, na mipaka na madhaifu yake. Kwa Maria, Mwana wa Mungu anafanyika kweli kuwa mwanadamu sawa na sisi katika kila kitu isipokuwa hakuwa na dhambi. Hivyo alikuwa na hisia sawa na sisi, kuna nyakati alijawa na furaha na hata huzuni, hofu na uoga na mashaka yatokanayo na ubinadamu wetu. Si tu alitwaa mwili na kuonekana kama sisi bali alifanyika mwanadamu na kuwa sawa na sisi katika kila hali isipokuwa hakuwa na dhambi. Ni kwa sababu hiyo anabaki ni MUNGU PAMOJA NASI.

Katika sehemu ya Injili ya leo inaanza kwa kutualika kutafakari kuzaliwa kwake Yesu Kristo. Lakini badala ya kuzungumzia jinsi na namna alivyozaliwa Yesu kama afanyavyo Mwinjili Luka tunaona Mwinjili Mathayo anatupatia kupashwa habari kwake Yusufu juu ya Maria kupata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Mwinjili Luka kinyume chake ilikuwa ni kupashwa habari kwa Maria na hivyo Yusufu anatajwa kwa kupita tu na si kama anavyoandika Mwinjili Mathayo. Labda swali linakuja kwa nini wainjili hawa wanatupa masimulizi ambayo kwa kweli ni juu ya tukio moja ila kwa namna mbili tofauti? Siwezi kusema naweza kutoa jibu sahihi na kuridhisha kila mmoja wetu anapokutana na masimulizi haya mawili tofauti ya Injili ndugu zaidi ya kugundua kuwa wainjili wote wawili lengo lao la awali halikuwa kutoa tu masimulizi ya kihistoria bali kutoa katekesi zenye Teolojia ndani yake. Ndio kusema kila mmoja kwa namna yake na msisitizo wake anajaribu kufikisha ujumbe wa kiteolojia kwani ikumbukwe kuwa wanaandika Injili baada ya Mateso, Kifo na Ufufuko wake Yesu Kristo, hivyo ni baada ya kuelewa kwa undani nini maana yake na wao wanaona kuna kila aina ya sababu na ni haki kutoa katekesi ya kiteolojia juu ya simulizi hili la kuzaliwa kwake Yesu Kristo.

Itoshe leo tutafakari sehemu ya Injili ya Mathayo kama tulivyoisikia na kuisoma. Mwinjili Mathayo kiujumla ni mwaminifu kutuonesha Yesu anazaliwa katika mazingira ya Kiyahudi na hivyo mara zote anatuonesha katika Injili yake kuwa Yesu anazaliwa na kuishi na kutangaza Habari Njema katika mazingira ya Kiyahudi. Wakati wa Nyakati za Yesu, ndoa kati ya Wayahudi ilifanyika katika hatua kubwa mbili. Hatua ya kwanza ilikuwa makubaliano ya kuwa mume na mke yaliyofanyika katikati ya wazazi au ndugu na jamaa wa karibu wa pande zote mbili na hasa mbele ya mashahidi wao wawili. Ila wawili hawa hawakuruhusiwa kuanza kuishi pamoja kwani kwa desturi makubaliano yale yalikuwa yanafanyika wakati binti alikuwa na miaka kama kumi na mbili a una tatu na kijana labda miaka kumi na sita au kumi na saba, hivyo walipaswa kuishi bado mbali mbali kwa takribani ili waweze kufahamiana lakini hasa kutoa nafasi ya kupevuka na kukomaa kwa pande zote mbili zote, mume na mke. Hata familia zote mbili kupata nafasi ya kufahamiana na kuona kabla kama watoto wao wangeweza kuanza maisha ya familia ya mume na mke.

Hivyo ni baada ya kusubiri kwa muda wa mwaka mmoja, familia zingeandaa sherehe kubwa ya kumsindikiza mke kuanza kuishi maisha ya unyumba ya mume na mke. Ni katika kipindi hicho cha kusubiri mwaka mmoja ndipo Maria alipopata kupashwa Habari na Malaika na kupata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Kama nilivyoonesha hapo juu katika utangulizi juu ya majina yake Yesu, jinsi yalivyomtambulisha kama mtu kweli na Mungu kweli na ndio tunaona Mwinjili Mathayo leo anatoa mkazo anapotuonesha jinsi Malaika alivyomtokea Yusufu ndotoni baada ya Maria kuwa ni mjamzito. Roho Mtakatifu au kwa Kiebrania ‘’Ruah’’ ndio pumzi ya Mungu, nguvu ya Mungu kwayo aliumba ulimwengu kama tunavyosoma Zaburi 104 na Kitabu cha Mwanzo 1:2. Hivyo iwe katika Injili ya Luka au ya Mathayo kama tunavyoisoma leo tunaona lengo ni kuonesha kuwa mtoto anayezaliwa wa Maria si tu mwanadamu bali pia Mungu. Ni Mungu anayekubali kufanyika mwanadamu na kuwa mmoja nasi.

Mwinjili Matayo anatuonesha mashaka na wasiwasi kwa upande wa Yusufu, kwa kweli hapa tunaweza kuwa na mengi ya kusema na hata tukajikuta katika maswali magumu kupata majibu, ila itoshe kuona ni mashaka ya haki kwa upande wa Yusufu kuweza kukubali mpango wa Mungu katika maisha yake. Ni mashaka ambayo hata mimi na weye tunajikuta nayo mara kadhaa hasa pale tunaalikwa nasi kushiriki katika mpango wa Mungu katika maisha, jinsi gani tutaonekana na kueleweka na wengine na hasa wale wanaotuzunguka. Yusufu anakuwa na mashaka ya haki iweje na kwa jinsi gani atampatia jina mtoto asiye wake, tena ni Mtoto wa Mungu, hivyo ni Mungu anajifunua kwake na kumwalika jinsi ya kushiriki katika historia ya wokovu. Mtoto katika mazingira ya Kiyahudi ni sawa na kusema anabeba jina la baba, na si tu jina kusema mtoto ni kusema ni mali ya baba ila mama alionekana tu kumzaliwa mume mtoto, labda hata katika baadhi ya mila na mitazamo yetu ya Kiafrika utasikia mwanamama fulani amemzaliwa bwana fulani mtoto, hivyo mtoto anaonekana kuwa ni wa baba na mama ni mbebaji tu, ni chombo tu, hata kwa wayahudi nao walikuwa na mtazamo wa aina hiyo.

Yusufu anapewa mmlaka ya kumpa mtoto jina, na ndio kusema mtoto anatambulika kuwa ni wa ukoo wa Davide, ukoo wa Yusufu. Yusufu kwa kukubali mpango wa Mungu hata kama ilikuwa juu ya uwezo wake wa kibinadamu kuuelewa ndio sababu leo Mwinjili Matayo anatambulisha kuwa alikuwa mtu wa haki. Mwinjili Mathayo anamalizia sehemu ya Injili ya leo akionesha kuwa ni utimilifu wa Unabii wa Isaya. Mwinjili Matayo anaonesha kuwa unabii ule anatimia na kukamilika kwa kuzaliwa kwake Yesu, ni kwa ujio wa Yesu matumaini yote waliyokuwa nayo yanafikia ukamilifu wake. Mwinjili Mathayo anamtambulisha Yesu mwanzoni mwa Injili yake kama Mungu pamoja nasi, lakini pia hata mwishoni mwa Injili yake anapowatuma wanafunzi wake kuenea Habari Njema ulimwenguni mwote na kubatiza watu na kuwaahidi kuwa pamoja nao mpaka mwisho wa nyakati. Matayo 28:20. Hivyo ni kutuonesha kuwa Yesu ni Mungu pamoja nasi katika nyakati zote za maisha yetu, anayesafiri nasi iwe ni nyakati rahisi na hata zile ngumu, la muhimu tubaki na imani thabiti kwake.

Labda tutafakari na tuone upande wa pili kwa nini Mwinjili Mathayo bado anamtambulisha Maria kama Bikira. Labda leo tunaposikia huyu binti ni bikira basi linalokuja kichwani mwetu ni kumuona binti anayejitunza na mwenye staha na heshima mwili wake. Na kwa kweli kwa Wayahudi binti bikira aliheshimika kwa kuwa hivyo kabla ya kuolewa. Hivyo Ubikira haukuwa na maana tena mara baada ya maisha ya ndoa na ni hivyo hata katika mila na desturi zetu. Litakuwa ni jambo la kushangasha na tena fedheha kutambulishwa mke wa mtu na aliyeolewa kuwa bado ni bikira, kwa kifupi ni matusi na fedheha kwa mume na hata familia nzima, kwani sio kitu cha kujivunia na kuonea fahari mara baada ya maisha ya kuishi pamoja kama mume na mke. Kwa Wayahudi kama ilivyo kwetu leo mwanamke aliyeolewa anapata heshima yake kwa kuwa mama na hata kutambulishwa kwa majina ya watoto wake na sio jina lake au la mume wake.

Bikira linatumika katika Maandiko Matakatifu kuonesha hasa sio usafi na ukamilifu bali mapungufu na kudharaulika. Yeremia 31:4 na 14:13. Bikira Binti Sayuni, likimaanisha ni nchi maskini, iliyodharaurika na isiyokuwa na maisha. Nchi ya Israeli pia inaitwa Bikira na Nabii Amosi kumaanisha nchi iliyolaaniwa na kukosa kutimiza njozi zake za kuwa mama. Amosi 5:2 Hata Babeli inalaaniwa na kutambulishwa kama Bikira, Isaya 47:1. Na kwa Maria swali kwa nini basi anatambulishwa kama Bikira hata baada ya kuwa mjamzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu? Maria katika utenzi ule wa Magnificat anaiomba na kuonesha unyonge na uduni wake. Luka 1:48-49 Maria anakuwa ishara na kielelezo kuwa ni kwa Nguvu na Uwezo wa Mungu hata mambo madogo na yanayodhaurika yanapata heshima kuonesha ukuu wa Mungu.

Pia jina Bikira katika Maandiko Matakatifu linaonesha mmoja mwaminifu asiye na moyo uliogawanyika.  Kukosa uaminifu kwa Israeli kunafananishwa na umalaya. Yeremia 5:7 Kuanza kuabudu miungu ya uongo kunafananishwa na ukahaba, ni kugawanyika kwa moyo, sehemu kuwa kwa Mungu wa kweli na sehemu kuwa na miungu ila ya uongo. Hosea 2 Ubikira ni ishara pia ya upendo mkamilifu kwa Mungu usio na kugawanyika kwa namna yeyote ile. Mtume Paolo pia anatumia jina hilo la Bikira kwa Kristo anapowaandikia Kanisa la Korintho. 2Wakorintho 11:2. Hivyo Maria ni kielelezo halisi kwa maana zote za neno Bikira kama tulivyoona hapo juu. Ni kielelezo cha mfuasi mwaminifu kwa Yesu, hivyo anabaki kuwa mfano kwa kila mfuasi wa Yesu Kristo. Nawatakia Dominika na Tafakari Njema na pia maandalizi mema ya Noeli, ya Mungu Kufanyika mwanadamu na kukaa kati yetu.

21 December 2019, 08:16