Tafuta

Vatican News
Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Changamoto na mwaliko wa kusoma na kutafakari Injili ya familia ili kuitolea ushuhuda katika uhalisia wa maisha. Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Changamoto na mwaliko wa kusoma na kutafakari Injili ya familia ili kuitolea ushuhuda katika uhalisia wa maisha. 

Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Injili ya familia

Familia ni Kanisa la nyumbani, ni shule ya sala, upendo, amani na mshikamano. Familia ni makao ya furaha na kitalu cha uhai. Kumbe, lengo kuu la Kanisa kuadhimisha sikukuu hii ya familia Takatifu, ni kuziombea familia zote zikue na kuishi kwa mshikamano zikimpendeza Mungu, zikidumu katika pendo lake, ziweze kujaa amani tele na baraka zake mwenyezi Mungu ziwe ndani yao milele yote.

Na Paschal Ighondo, - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika Tafakari ya Neno la Mungu, katika Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Mnamo mwaka 1921 Baba Mtakatifu Benedikto wa XV, aliiweka rasmi sikukuu hii iadhimishwe jumapili katika oktava ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo, au tarehe 30 Desemba. Katika Sherehe ya Kristo Mfalme mwaka 1981, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II aliandika barua ya Kitume inayoeleza wajibu wa familia ya Kikristo kwa Kanisa na ulimwengu. Baba Mtakatifu anasema kuwa familia ni Kanisa la nyumbani. Familia ni shule ya sala, shule ya upendo, amani na mshikamano. Familia ni makao ya furaha na kitalu cha uhai. Katika hitimisho la barua hii Baba Mtakatifu Yohane Paulo II aliziweka familia zote chini ya ulinzi na usimamizi wa Yesu, Maria na Yosefu. Kumbe kiini na lengo kuu la Kanisa kuadhimisha sikukuu hii ya familia Takatifu, ni kuziombea familia zote zikue na kuishi kwa mshikamano zikimpendeza Mungu, zikidumu katika pendo lake, ziweze kujaa amani tele na baraka zake mwenyezi Mungu ziwe ndani yao milele yote.

Familia ni muungano wa Mume na mke, unaofungamishwa na upendo na tunda litokanalo na Upendo wao ni watoto ambao ni zawadi toka kwa Mungu na ndiyo inayowafanya waitwe wazazi, yaani Baba na mama. Familia ni mpango wa Mungu. Tangu mwanzo aliwaumba mume na mke, Adamu na Eva akawashirikisha uwezo wake wa uumbaji na kuwapa kazi ya kuuendeleza kwa kuwaridhisha wengine tunu ya uhai. Ndiyo maana wajibu wa familia ni pamoja na kuishi pamoja kwa wanandoa, kuendeleza kazi ya uumbaji na kuwezesha mwendelezo wa tunu ya uhai kwa kuzaa watoto, kuwalea na kuwaridhisha tunu zilizo njema. Kanisa linajali familia kwani ndiyo ni kitovu cha uumbaji, shule ya kutambua mapenzi ya Mungu. Katika familia Injili inapaswa kusomwa na kutafakariwa, liturujia inapata msingi kwa njia ya sala, nyimbo, na sakramenti.

Katika somo la kwanza Yoshua Bin Sira anawausia watoto namna wanavyopaswa kuishi na wazazi wao, kwamba wanapaswa kuwa na heshima ya kina na upendo kwa wazazi wao, hususani wanapozeeka. Yoshua Bin Sira anasema watoto wanaowaheshimu wazazi wao kamwe hawatajuta katika maisha yao hata siku moja. Mungu lazima atawalipa kwa heshima na upendo wao kwa wazazi wao, atawajalia watoto wa uzao wao wenyewe, atawapa maisha marefu yenye fanaka hapa duniani, atawasamehe dhambi zao na mwisho kwa ukarimu wao atawapokea katika ufalme wake mbinguni. Hivi ndivyo wanavyopaswa kuwa watoto katika familia za kikristo. Kila mmoja anapaswa kujiuliza ndivyo alivyo kwa wazazi wake? Kama sivyo basi, tujichunguze ili tujue ni kwanini na tufanye mabadili tuweza kuzifaidi hizo ahadi za Mungu.

Mtume Paulo katika somo la pili la Waraka wake kwa Wakolosai, anatupa miongozo ya familia ya Kikristo kwa nyakati zote. Mtume Paulo anaongea juu ya familia za aina mbili, yaani familia asili ya baba, mama na watoto na familia ya kiimani, ndiyo Jumuiya ya Kikristo. Paulo anatambua fika kwamba mstakabili wa familia ya kiimani yaani jumuiya ya Kikristo hutegemea sana vile zilivyo familia asili ya baba, mama na watoto. Paulo anataka tutambue kwanza kabisa kwamba Mungu anatupenda, anatujali na kutupigania katika kila siku katika maisha yetu. Tukishatambua kuwa Mungu anatupenda basi turuhusu amani ya Kristo itawale mioyoni mwetu kwani ndiyo tuliyoitiwa katika mwili mmoja, tena tuwe watu wa shukrani. Paulo anatukumbusha kuwa adui wa kwanza katika maisha ya familia ni dhambi kwani ndiyo inayoleta mgawanyiko, mpasuko, malumbano na ugomvi katika familia. Umoja na mshikamano katika familia vitakuwepo kama tukijivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, moyo wa kuchukuliana na kusameheana kama Mungu anavyotusamehe sisi. Paulo anatuasa tuepuke ubinafsi na tujivike upendo ambao ndio kifungo cha ukamilifu wote.

Familia ni shule ya sala hivyo, familia inayosali pamoja hukaa pamoja na kinyume chake ni kweli pia. Upendo wa kifamilia na mshikamano hutokomea mara tu familia inapoacha kukutana kwa sala na kutokusoma neno la Mungu. Ndiyo maana Paulo amesema: “Neno la Kristo likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi na nyimbo, na tenzi za rohoni, huku mkimwimbia Mungu kwa Neema mioyoni mwenu” Kol 3:16. Kumbe, tunaposoma Maandiko Matakatifu kwa moyo wa ibada, tunasali. Familia ya kikristo inapaswa kukusanyika pamoja kila jioni baada ya chakula, kusoma neno la Mungu na kulitafakari. Kwa kutafakari neno la Mungu, familia inashirikishana utajiri na tunu zilizomo katika neno la Mungu na sala yao inapata msisimko utokanao na mwangaza wa Roho wa Mungu. Sala ya familia inawaondolea wanafamilia roho ya ubinafsi. Katika familia ya Nazarethi hakukuwepo ubinafsi, hakuna aliyejifikiria mwenyewe.

Kila walichotenda na kufikiri kililenga kuwaimarisha katika mahusiano yao wenyewe na mahusiano na Mungu, wote walitambua kuwa Mungu anawapenda, walikuwa na moyo mmoja na roho moja katika sala. Kutokana na upendo wao familia yao ilikuwa ni ya furaha na amani. Katika familia baba anapaswa kuwa ni nguzo inayohakikisha ulinzi, ustawi, mahitaji na maendeleo ya kweli ya familia yanapatikana. Kwa upendo, Baba anapaswa kufanya kazi kwa bidii, huku akimcha Mungu, kuwapa watoto wake malezi bora kwa kuwaweka na kuwapa mipaka katika maisha yao ili waweze kujengeka katika utu wema, wakimpenda Mungu na jirani. Katika familia Mama ni jiwe la msingi katika kulea watoto, kulinda tunu za familia yaani utu, kazi, upendo, umoja, nidhamu na amani. Mama mwema wa familia siku zote atamheshimu mume na kuwapenda watoto wake, atamcha Mungu na kupigania ustawi na mafanikio ya familia yake kiroho, kimaadili na kiuchumi. Huyu ni mke mwema. Ataepuka majungu, "starehe feki", usaliti na uvivu.

Watoto ni zawadi toka kwa Mungu katika Familia, ni vyema basi kumtukuza Mungu kwa kuwalea vyema katika maadili mema ya jamii, kumwogopa Mungu na siku zote kuwaridhisha tunu za kiutamaduni na kidini. Watoto pia wanapaswa kuwaheshimu wazazi wao ambao ni wawakilishi wa Mungu duniani ili waishi vyema kama Yesu na wakue katika kimo na hekima. Tutambue kuwa majaribu na magumu katika familia yatakuwepo. Tujifunze kutoka kwa familia takatifu ambayo nanyo ilikumbana na kupambana na majaribu mbalimbali bila kukata tamaa maana walimtegemea Mungu. Simulizi la Injili linasema Malaika akamwambia Yosefu, “Ondoka umchukue mtoto na mama yake ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie kwa maana Herode anataka kumwangamiza mtoto” Mt. 2:13. Safari hii ambayo wanaambiwa waichukue ni safari ndefu na ngumu tena ni safari ya jangwani, ambapo mchana mchanga unachoma na kuumiza na usiku upepo mkali, wakiwa na mtoto wao mchanga ambaye hajafikisha hata miezi miwili.

Maria na Yosefu waliisikiliza sauti ya malaika wakaitii, wakamchukua mtoto, wakaondoka kwenda uhamishoni Misri. Baada ya kukaa kwa muda huko Misri, huenda miaka mingi, malaika alimtokea tena Yosefu na kuwaambia: “Ondoka umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli, kwa maana wamekufa walioitaka roho ya mtoto.” Mt 2:20. Yosefu anatii ile sauti ya malaika na kuanza tena safari ndefu kurudi nyumbani Bethlehemu, makazi ya mababu zao, karibu na Yerusalem, mji mtakatifu. Lakini njiani walipofika Israeli wanaambiwa waende Galilaya katika mji wa Nazarethi, maana Archileo mwana wa Herode alikuwa ni mtawala wa Bethlehemu angeweza kutimiza alichotaka kufanya Baba yake Herode. Tunajifunza kuwa ukimtumania na kumtegemea Mungu hakuna gumu lolote litakalokushinda katika maisha. Licha ya hatari zote zinazozikabili familia zetu, hatuna mashaka kwamba tukijiachilia kwa Mungu kama Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu hakuna tutakaloshindwa.

Yesu mzaliwa wa kwanza ni mfano halisi wa maisha ya watoto wanaompendeza Mungu na wanadamu. Kristo anapaswa kuwa kiini cha maisha yetu ya familia; neema na amani yake inapaswa kutawala mioyo yetu nyakati zote. Basi tuombe neema na baraka zake ili tuweze kuepuka moyo wa ubinafsi, tuuvae upendo, tuwe na ukarimu, wema, uvumilivu na msamaha. Tumwinulia Mungu mioyo yetu katika sala za shukrani azifanye familia zetu kuwa kweli kanisa la nyumbani, shule ya upendo, shule ya sala na shule ya amani na furaha. Tumsifu Yesu Kristo.

Familia ni Shule ya Sala

 

 

 

27 December 2019, 16:59