Tafuta

Vatican News
Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni fursa adhimu ya kutafakari kuhusu Mwaka wa Familia Tanzania kwa kupembua kwa kina na mapana changamoto mamboleo kwa familia! Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni fursa adhimu ya kutafakari kuhusu Mwaka wa Familia Tanzania kwa kupembua kwa kina na mapana changamoto mamboleo kwa familia!  (AFP or licensors)

Sherehe ya Familia Takatifu: Mwaka wa Familia Tanzania: Changamoto mamboleo!

Changamoto hizo ni kama vile: Talaka, Ndoa za utotoni, Uchumba sugu, Ndoa za mitaala, Kukosa uaminifu ndani ya ndoa, Ndoa za kurithi wajane, Ndoa za Jinsia moja, Ndoa baada ya ndoa ya kwanza halali, Ndoa zisizo na watot, Kubadili maumbile. Matatizo mengine ni pamoja na: Familia za mzazi moja, Familia zenye mchanganyiko wa Imani, Familia zinayoishi katika mazingira magumu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni fursa adhimu kurejea tena katika maadhimisho ya Mwaka wa Familia uliotangazwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kama matunda ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara. Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “Familia Kanisa la Nyumbani na ni shule ya imani na maadili”. Katika muktadha huu, Radio Vatican kwa leo inapenda kukushirikisha changamoto zinazoikabili familia katika ulimwengu mamboleo. Kazi kubwa ya Kristo ilikuwa ni kumkomboa mwanadamu dhidi ya dhambi na matokeo yake mabaya (Rej.Lk. 4:18-19; Lk. 5:20, 27-32). Kanisa kama mwili wa fumbo wa Kristo linao wajibu wa msingi wa kuendeleza kazi ya Kristo kwa wanadamu.  Mahali pazuri pa kufanya kazi hiyo ni kupitia familia ambapo mtu hupata uhai na malezi ya kiutu na kiroho. Kwa kuzingatia hali ya sasa na changamoto zake katika familia na ndoa jitihada zozote za kuelimisha jamii juu ya mpango wa Mungu kwa kila binadamu hapa duniani, lazima familia zetu zijipange kukabiliana na changamoto zile zinazoukabiri ulimwengu wetu wa sasa katika karne ya ishirini na moja na nchi yetu ya Tanzania ikiwemo.

Changamoto hizo ni kama vile: Talaka, Ndoa za utotoni, Uchumba sugu, Ndoa za mitaala, Kukosa uaminifu ndani ya ndoa, Ndoa za kurithi wajane, Ndoa za Jinsia moja, Ndoa baada ya ndoa ya kwanza halali, Ndoa zisizo na watot, Kubadili maumbile. Matatizo mengine ni pamoja na: Familia za mzazi moja, Familia zenye mchanganyiko wa Imani, Familia zinayoishi katika mazingira magumu ya uchumi, Familia zenye watoto walemavu, Familia zisizo na mzazi hata mmoja, Familia zisizoishi imani, Familia zisizo na maadili, Familia zilizopoteza uwezo wa kulea, Familia zisizo na kipato. Asili ya matatizo katika ndoa na familia ni pamoja na: Utamaduni na Mazingira: Tunaishi katika historia yenye mazoea, mila, desturi na mapokeo ya wazee wetu.  Iko sehemu ya utamaduni wetu isiyokubaliana na ukweli wa kimungu ambao ni wa lazima katika kuishi ndoa safi na familia bora. Mpaka sasa katika mazingira yetu zipo tamaduni zinazoruhusu talaka, ndoa za utotoni, uchumba sugu, ndoa za mitaala, “nyumba ndogo”, ndoa za kurithi wajane, ndoa za jinsia moja na ndoa baada ya ndoa ya kwanza halali. Ni jukumu la kila mkristu, ndani ya familia, kuchekecha utamaduni wake, kwani kumekuwa na chenga zisizopita katika chujio la Kristo aliye Mwanga wa maisha yetu.

Harakati za kila mmoja ambazo zinalenga moja kwa moja kuibomoa familia: Harakati hizi zinatangaza na kupigia upatu uhuru usio wa kweli kwa mwanadamu.  Zinapotosha ukweli kwa kutenganisha ukweli wa maisha na ukweli wa asili katika viumbe na maumbile yao.  Maisha ya kiroho, maisha ya ndoa na familia, yanakuwa ni jambo binafsi na la faragha bila kuhusisha jamii na wala kumhusisha Mungu.  Uhusiano wa mtu na jamii unahuishwa katika sheria tu ambazo jamii inazitunga na kuzibadili mara kwa mara. Matokeo mabaya ya harakati  hizi ni kukithiri kwa ubinafsi, kuenea na kuzagaa kwa matukio yenye kuchochea waziwazi tamaa za ngono kati ya watu wa rika zote. Wimbi kubwa la maisha huria, bila malengo wala kanuni na nidhamu ya kukataa malengo mema. Kuongezeka kwa mifarakano ya ndani ya nafsi na hivyo mifarakano kati ya mtu na mtu ndani na nje ya familia kunakoshuhudiwa na matatizo ya msongo wa mawazo, hali ya kukata tamaa.

Harakati hizi zimejaa kwa wengi, na pia mtazamo potofu kuhusiana na maadili katika ndoa na familia. Na hivi mtu kufikia mahali kujiaminisha kwamba maisha yanawezekana bila Mungu na bila utu. Msimamo huu haumwezeshi mtu kupokea na kudumisha tunu njema za maisha ya ndoa na familia, ambazo kuasisi tunu hizo huzifanya ndoa na familia zifanyike katika kweli na zidumu na kusitawi na kuzaa matunda. Changamoto za ndoa na familia kimsingi ni changamoto za kukubali na kupokea tunu za maisha ya ndoa na familia. Tunahitaji kujihoji mbele ya Kristo juu ya wito wa kuwa wavumilivu, wasamehevu, wenye kiasi na wenye subira Rej. 1Kor.13:1-8). Tunahitaji kujipima tena kama tunazithamini na kuvutiwa nazo zile heri nane alizozitangaza Bwana wetu Yesu Kristo ambazo ni usafi wa moyo, upole, unyenyekevu, upatanisho, kuudhiwa kwa ajili ya haki, kukubali kushindwa/kudhulumiwa kwa sifa na utukufu wa Mungu (Mt.5:3-12).

Tunahitaji kujithamini mbele ya Mungu, kuona thamani ya upendo wa Kristo kwetu na wa yule aliyetupatia Kristo.  Maana “Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye” (Rum.8:32). Hakuna anayeweza kututenga na upendo wa Kristo (Rum.8:35-39). Utatuzi wa matatizo mengi katika ndoa unajikita kimsingi katika changamoto ya kurudisha sura njema ya maagano kati ya Mungu na katika utakatifu kati ya Kristo na Kanisa lake (Rej.Waefeso 5:21-25). Wakristo wenye ndoa na ni wazazi kwa njia ya ubatizo wao wanawajibika kutoa mchango wao wa pekee kwa ajili ya kufafanua mafundisho na tunu za kiinijli katika mazingira na tamaduni mbalimbali za leo ambamo kwazo wanafamilia huishi maisha ya familia. Wanandoa kwa namna ya pekee wamestahilishwa jukumu hilo kwa sababu ya karama yao na jukumu lao la kisakramenti hasa sakramenti ya ndoa.

Wanandoa kwa kuheshimu mpango wa Mungu hubeba jukumu kuu la kuwa wazazi ambapo hukubaliana na wito wa Mungu kuwaleta duniani watoto. Mungu huendeleza kazi yake ya uumbaji na kuendeleza uhai wa kimwili na kiroho kwa kuwatumia wazazi. Hivi kukubali kuwa mwanandoa ni kukubali jukumu la kuuweka uhai wa binadamu kuwa ni jukumu la kimungu linalomtaka mtu amsikilize Mungu Muumbaji na anayetakatifuza.

Mwaka wa Familia Tanzania

 

27 December 2019, 16:38