Tafuta

Vatican News
Parokia ya Mtakatifu Nicholaus, Kunduchi Mtongani, tarehe 8 Desemba 2019 inaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwake! Ni Mama wa Parokia kadhaa Dar Es Salaam. Parokia ya Mtakatifu Nicholaus, Kunduchi Mtongani, tarehe 8 Desemba 2019 inaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwake! Ni Mama wa Parokia kadhaa Dar Es Salaam.  (ANSA)

Parokia ya Mtongani Kunduchi, Jimbo kuu la Dar es Salaam: Kumenoga!

Ilikuwa ni tarehe 6 Desemba 1999, Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam alipozindua rasmi Parokia ya Mtakatifu Nicholaus, Kunduchi Mtongani, Jimbo kuu la Dar Es Salaam na kumsimika Padre Dominico Altieri, C.PP.S kuwa Paroko wa kwanza na Msaidizi wake akiwa ni Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Parokia inayo mengi ya kumshukuru Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanabainisha: wito, utume na dhamana ya waamini walei katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati. Waamini walei ni wadau pia katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa! Waamini walei ni washiriki wa huduma ya Kristo kuhani, nabii na mfalme, wanayo nafasi hai katika maisha ya Kanisa na katika utendaji wake. Ndani ya jumuiya za Kanisa matendo yao yanahitajika sana, kiasi kwamba pasipo haya hata utume wenyewe wa wachungaji huwa hauwezi kufikia mafanikio kamili.  Maana walei wenye roho halisi ya kitume, kama wale wanaume na wanawake waliokuwa wakimsaidia Mtume Paulo katika kueneza Injili (Taz. Mdo 18:18.26; Rum 16:3), wanawakirimia ndugu zao yale waliyopungukiwa, na wanaburudisha roho za wachungaji na za waamini wengine wa taifa la Mungu (Taz. 1Kor 16:17-18).

Adhimisho la  Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa na hiki ndicho kiini cha maisha ya Parokia. Kimsingi, Fumbo la Ekaristi Takatifu linaadhimishwa Siku ya Bwana; Jumuiya ya waamini inapopata nafasi ya kusikiliza, kutafakari Neno la Mungu na hatimaye, kutumwa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao, kama kielelezo cha imani tendaji! Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa, mahali pa kuinjilisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, tayari kutoka kifua mbele kutangaza furaha ya Injili; huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Mababa wa Kanisa wanasema, sasa umefika wakati wa kuangalia ya mbeleni kwa matumaini zaidi, ili kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa zinazoendelea kujitokeza miongoni mwa waamini walei katika Parokia, ili waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu.

Ilikuwa ni tarehe 6 Desemba 1999, Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam alipozindua rasmi Parokia ya Mtakatifu Nicholaus, Kunduchi Mtongani, Jimbo kuu la Dar Es Salaam na kumsimika Padre Dominico Altieri, C.PP.S kuwa Paroko wa kwanza na Msaidizi wake akiwa ni Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Ni Parokia iliyoanzishwa kwenya mazingira magumu, lakini waamini wake walikuwa na ari na mwamko wa kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Tarehe 8 Desemba 2019 Parokia ya Mtakatifu Nicholaus, Kunduchi, Mtongani inaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwake. Mheshimiwa Padre Vedasto Ngowi, C.PP.S, anapenda kuchukua fursa hii kuwapongeza, kuwashukuru na kuwatia moyo watu wa Mungu Parokia ya Mtakatifu Nicholaus, Kunduchi, Mtongani. Anasema hata yeye ni sehemu ya watu wa Mungu Parokiani hapo, kwani kuanzia mwaka 2011 hadi mwaka 2013 alikuwa ni Paroko.

Padre Vedasto anaushukuru uongozi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu pamoja na waamini walei waliojisadaka bila ya kujibakiza kiasi cha kuweka msingi thabiti kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Parokiani hapo. Katika kipindi cha Miaka ishirini, Parokia ya Mtongani inayo mengi sana ya kujivunia. Hata katika umaskini wake, imewezesha baadhi ya vigango vyake kuwa ni Parokia kamili. Baadhi ya Parokia hizi ni Parokia ya Bikira Maria Mama wa Huruma, Tanki Bovu; Parokia ya Mtakatifu Gaspar, Mbezi Beach,  maarufu kama “Machakani”, Parokia ya Mtakatifu Domenico, Parokia ya Mtakatifu Augustino, Salasala; Parokia ya Mtakatifu Andrea, Bahari Beach, kwa kutaja tu kwa uchache wake. Bila shaka anasema Padre Vedasto Ngowi, Parokia zote hizi zina kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa maongozi yake wakati huu Parokia ya Mtakatifu Nicholaus, Mtongani Kunduchi inapoadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwake.

Padre Ngowi anasisitiza kwamba, katika kipindi chote hiki, Parokia imebahatika kuwa na waamini wenye ari na ushiriki mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Parokiani hapo. Shirika la Masista Moyo Safi wa Maria Afrika, IHSA, pamoja na Makatekista na kwa namna ya pekee Katekista Pius Kikonyi, wamechangia sana ukomavu wa imani Parokiani hapo. Viongozi wa Halmashauri Walei katika ngazi mbali mbali pamoja na viongozi wa vyama mbali mbali vya kitume, wamesaidia sana katika ukuaji wa Parokia hii hadi kupata mafanikio makubwa kiasi hiki. Kumbu kumbu ya Miaka 20 ni muda muafaka wa kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita kuna watu wamekwazika na kutopea katika malimwengu, kiasi cha kusahau mahali ulipo mlango wa Kanisa.

Kuna waamini ambao bado wana vikwazo katika maisha yao, kiasi cha kushindwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa. Lakini wote hawa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Parokia ni kitovu cha uinjilishaji wa kina. Kumbe, kuna haja ya kuweka mbinu mkakati wa kuwaendea na kuwatafuta waamini, mahali wanapoishi na kufanya kazi, ili kuwapatia tena nafasi ya kukutana na Kristo Yesu katika safari ya maisha yao. Waamini wawe tayari kuwashirikisha wengine uzoefu na mang’amuzi yao katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni sehemu ya mchakato wa uinjilishaji. Kila wakati waamini wanapokutana na watu wengine watambue kwamba, hapo wanatekeleza dhamana na wajibu unaoweza kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu. Watu wanavutwa kwa ushuhuda wa maisha na wala si wongofu wa shuruti. Waamini wawe na ujasiri wa kuwaonjesha jirani zao Injili ya upendo, huruma na matumaini.

Kwa kutekeleza yote haya watambue kwamba, wanamtendea Kristo Yesu ambaye amejitambulisha na maskini pamoja na wahitaji mbali mbali. Kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Mtakatifu Nicholaus Kunduchi, Jimbo kuu la Dar es Salaa iwe ni chemchemi ya umoja, upendo na mshikamano wa dhati katika mambo matakatifu! Parokia iwe ni mahali pa kusikiliza na kutafakari Neno la Mungu; Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na Majiundo endelevu katika Imani kwa njia ya katekesi makini na endelevu! Kwa hakika Mtongani kumenoga, Yaani, we acha tu!

Parokia ya Mtongani
06 December 2019, 18:33