Tafuta

Tafakari ya Injili ya Jumapili ya 3 ya Kipindi cha Majilio inajadili kwa kina na mapana kashfa kuhusu maisha na utume wa Masiha anayefunua Uso wa huruma na upendo wa Mungu! Tafakari ya Injili ya Jumapili ya 3 ya Kipindi cha Majilio inajadili kwa kina na mapana kashfa kuhusu maisha na utume wa Masiha anayefunua Uso wa huruma na upendo wa Mungu! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 3 ya Majilio: Kashfa ya Masiha!

Yesu anajifunua kama Masiha wa Mungu, lakini tofauti na yule aliyetarajiwa na kutegemewa kadiri ya mantiki na mitazamo ya kibinadamu. Namna yake ilikuwa ni makwazo hata kwa Yohane Mbatizaji. Ndiyo maana Yesu anatangaza Heri kwa yule asiyekwazika na Sura ya Masiha. Katika tafsiri yetu tunasoma: Naye heri awaye yote asiyechukizwa nami’’. Neno sahihi ni kutokwazika nami.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Haijawahi kuwa rahisi kumtambua Masiha na hata nyakati zetu bado tuna changamoto kubwa za kuutambua uso na sura halisi ya Masiha! Kwa miaka mingi Taifa la Israeli kwa msaada wa mafundisho ya manabii waliandaliwa kumpokea Masiha wa Mungu lakini bado haikuwa rahisi kwao kumtambua, na ndicho anachokutana nacho pia Yohane Mbatizaji. Masiha aliyetegemewa alipaswa kuja katika hali ya kuogofya na kutisha, mwenye kila enzi na uwezo na nguvu na utukufu, hivyo kuendana na mantiki na matarajio yao na labda yetu pia leo hii. Vile kwetu Mungu anapaswa kujifunua sio katika hali duni na unyonge bali ya kila nguvu na uwezo na maajabu mengi ya kumstajaabisha mwanadamu. Katika sehemu ya kwanza ya Injili ya leo, tunaona mashaka makubwa kwa upande hata wa mtangulizi, mwandaaji wa njia ya Masiha, ndio kutoka kwake Yohana Mbatizaji.  Yohana Mbatizaji akiwa gerezani kwa shauri la kumwambia ukweli Herode kuwa haikuwa sawa kwake kumchukua mke wa ndugu yake. Kadiri ya Mwana historia Giuseppe Flavio, Yohane Mbatizaji akiwa gerezani alipata pia upendeleo maalumu wa kuweza kutembelewa na wanafunzi wake, hivyo ni katika muktadha huo bado alikuwa akimfuatilia kwa hamu kubwa yule aliyedhani kuwa ni Masiha, yaani Yesu wa Nazareti, na ndipo kutuma wanafunzi wake kwenda kwa Yesu na kumuuliza kuwa Yeye ndiye au la!

Ni katika mazingira ya mashaka si tu ya watu wengine bali hata ya Yohana Mbatizaji mwenyewe na ndio anasukumwa kuwatuma wanafunzi wake kwenda na kumuuliza Yesu: ‘’Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?’’ Labda tunaweza kushangaa iliwezekana kwa mtangulizi wa Masiha naye kujawa na mashaka kiasi kile. Kwa kweli jibu lake ni rahisi tu, Yohana Mbatizaji kama walivyokuwa wayahudi wengine wote, tangu angali mtoto alikuwa na kulelewa akimtarajia Masiha wa mantiki ile ya kibinadamu na si ya Kimungu. Ni mapokeo kutoka aidha kwa wakubwa wake lakini sana pia kutoka kwa viongozi wa kiroho katika jumuiya ya wayahudi. Akiwa gerezani naye anamtarajia Masiha wa kumtetea na kumpigania ili aweze kuachiwa huru kutoka kifungoni kama aliyotabiri Nabii Isaya miaka mingi kabla.  Isaya 61:1, anayekuja kurejesha haki na kweli duniani. Hivyo ni katika muktadha huo anabaki na maswali ya kujiuliza kama Yesu wa Nazareti ndiye Masiha wa kweli basi kwa nini hajali na hali ya kutabika na hasa kifungo chake mle ndani gerezani. Alimtarajia Masiha anayekuja kurejesha haki duniani hata kwa mabavu na nguvu.

Kinyume chake ni mshangao hata kwake aliye mtangulizi na kumpelekea kujawa na mashaka juu ya Yesu wa Nazareti kuwa ni Masiha. Yesu wa Nazareti si tu hakuwa anawakaripia na kuwalaani wadhambi, bali alikuwa anakula na kunywa nao na zaidi kujitambulisha kama rafiki wa wadhambi. Luka 7:34. Hata hivyo kwa wale wanafunzi wake Yohana Mbatizaji Yesu anajifunua na kuwaalika kuwa Yeye ndiye Masiha kwa kuorodhesha ishara zile zinazomdhihirisha na kumfunua kama Masiha wa Mungu. Isaya 35:5-6 na 26:19 na 61:1 kama alivyoanisha Nabii wa matumaini kuwa hakuna mmoja atakayelalamika tena kuwa yu mgonjwa. Isaya 33:24. Yohane anaalikwa naye kutafakari juu ya ishara zile sita ambazo ni; Uponywaji wa vipofu, viziwi, viwete, wakoma, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa Habari Njema. Zote ni ishara za ukombozi, ishara za kuwaweka huru wana wa Mungu na hakuna hata moja ya kumwangamiza mwanadamu. Ni saa ya wokovu kwani aliyekuwa kipofu kwa kutembea katika giza, sasa nuru inamzukia na kumwangaza ili atembee katika nuru, aliyekuwa kilema kwa kushindwa kutoka na kwenda mbele ya Mungu na jirani sasa anajaliwa tena uwezo wa kumkaribia Mwenyezi Mungu na jirani, aliyekuwa kiziwi wa Neno la Mungu sasa anapokea uponyaji na kuanza kuongozwa na hilo Neno.

Aliyekuwa anajisikia unyonge wa ukoma wa dhambi na kujiona kutengwa na Mungu na jumuiya sasa anapokea utakaso na maondoleo ya madoa ya dhambi, aliyekuwa akiishi maisha yasiyo na uzima, sasa anapokea uponyaji na maisha ya kweli, na yule aliyekuwa maskini wa Habari Njema sasa anapokea Habari Njema na kuongozwa nayo, Habari ya Furaha na Matumaini kwa wale waliopoteza awali matumaini na furaha ya kweli. Hivyo Yesu anajifunua kama Masiha wa Mungu, lakini tofauti na yule aliyetarajiwa na kutegemewa kadiri ya mantiki na mitazamo ya kibinadamu. Namna yake ilikuwa ni makwazo hata kwa Yohane Mbatizaji. Ndiyo Yesu anatangaza Heri kwa yule asiyekwazika na Sura ya Masiha. Katika tafsiri yetu tunasoma: Naye heri awaye yote asiyechukizwa nami’’. Kwa kweli neno sahihi sio kuchukizwa bali ni kutokwazika nami. Neno kukwazika likiwa na maana kitu kinachonifanyika nianguke, kushindwa kuwa na muono sahihi juu ya mtu au jambo au kitu. Hivyo hata nasi leo ni vema kujiuliza katika tafakari zetu za Dominika ya leo kama ni mara ngapi tunakwazika kwa sura au uso wa Yesu unaojifunua na kujidhihirisha kwetu?  

Ni mara ngapi hata nasi tunataka Yesu ajifunua kama Mungu mwenye nguvu na mabavu ili awaangamize na kuwateketeza maadui zetu na wake? Ni mara ngapi tumebaki kuonekana wanyonge na tusio na nguvu kama wafuasi na rafiki zake Masiha Yesu? Kama ambavyo Yesu anamwalika Yohane Mbatizaji kutokukwazika na Yeye, ndivyo anavyotualika nasi leo kubadili mtazamo na namna zetu za kuuona uso wa Mungu Mkombozi wetu.  Mungu anayekuwa mwema kwa watu wote bila kujali kuwa ni wema au wadhambi bado ni kikwazo kikubwa hata kwetu wahubiri wa nyakati zetu. Mara nyingi tunashawishika kutaka Mungu ajifunue na atende kadiri ya mantiki na namna zetu za kibinadamu na ndio hapo tunapojikuta tunakwazika, ila leo Yesu anasema wa heri wale wasiokwazika na Uso wa Mungu kwetu. Heri kwa yule anayempokea Mungu jinsi alivyo na si kwa jinsi tunavyomtaka Mungu awe au atende kadiri yetu sisi. Yohana Mbatizaji abaki kuwa kielelezo cha kila muumini, kwani katika mashaka yake aliuliza maswali ila hakukana waziwazi kuwa Yesu wa Nazareti sio Masiha bali alihoji ili apate hakika ya mashaka na wasiwasi wake. Na ndio nasi pia yawezekana tuna mashaka mengi katika imani yetu hatuna budi kutuma maswali na mashaka yetu kwa Yesu Kristo mwenyewe hasa kwa sala na tafakari za ndani.

Sehemu ya pili ya Injili ya leo ni baada ya kuondoka kwa wanafunzi wa Yohane Mbatizaji, Yesu anauliza maswali yenye nia na lengo la kuwatafakarisha pia wanafunzi na wasikilizaji wake, pia nasi leo tunaalikwa kutafakari maswali hayo hayo. Yesu anamtambulisha Yohane Mbatizaji kama nabii na si kama unyasi unaofuata upepo ndio kusema kuathiriwa na namna za dunia hii, kiasi cha kutokutetereka katika kumwambia Herode ukweli, hakuwa mmoja aliyenufaika na matajamara ya wafalme kwani hakuwa na vazi mororo bali aliishi maisha ya kujitakatalia na sadaka kubwa. Na ndio mwaliko wa Yesu kwetu leo kuwa kama Yohana Mbatizaji kubaki manabii wa kweli hata katika nyakati ngumu na zenye kila aina ya vitisho na hatari, tujiulize kama bado ndani mwetu tuna ile sauti ya kinabii tuliyoipokea kwa namna ya pekee siku ile ya ubatizo wetu.

Yesu anamtambulisha kama Nabii ila anasema ni zaidi ya Nabii. Ndio kusema hakuna nabii mwingine yeyote kabla yake aliyefanya kazi kubwa na misheni muhimu kama yake, ni ndio ya kumwandalia njia Masiha wa Mungu, kuwa mtangulizi wa Masiha.  Aliye mdogo katika ufalme wa Mbinguni ni mkubwa kuliko Yohane Mbatizaji, hapa Yesu hataki kuonesha ngazi au kiasi cha utakatifu au ukamilifu wa mtu husika, bali anatualika kuangalia ufuasi wetu kwake. Anayekuwa katika ufalme wa Mungu ndio kusema anakuwa na muono sio ule wa kibinadamu bali unaoongozwa na kuangazwa na Mungu mwenyewe, hivyo kuweza kuutambua uso wa Masiha bila shida na mashaka. Ni yule anayeuona Uso wa Mungu kuwa amekuja duniani ili mwanadamu apate uzima wa Kimungu, ndiye anayekuwa katika njia sahihi na hapo anakuwa kweli mkubwa kuliko Yohana kwani haongozwi na mantiki ya dunia hii bali anakubali kuongozwa na mantiki ya Kimungu. Wapendwa naawalika katika Dominika ya leo ya Furaha ya majilio kukubali kubadili vichwa vyetu yaani mitazamo yetu ili daima tuweze kuongozwa na mantiki ya Kimungu na si ya dunia hii. Nawatakia Dominika na tafakari njema na maandalizi mema ya Sherehe ya Noeli.

14 December 2019, 16:05