Tafuta

Vatican News
Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA wanahudhuria mkutano wao wa 40 uliofunguliwa na Askofu Desiderius Rwoma, Mwenyekiti wa Idara ya Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA wanahudhuria mkutano wao wa 40 uliofunguliwa na Askofu Desiderius Rwoma, Mwenyekiti wa Idara ya Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. 

Mkutano wa 40 wa Wanawake Wakatoliki Tanzania! Haki na Amani!

WAWATA wanahudhuria mkutano mkuu wa 40. Hii ni nafasi ya kupembua taarifa za WAWATA kutoka Majimboni, Afya ya wanawake wa Tanzania hususan kuhusu ugonjwa wa Saratani ambao kwa sasa ni changamoto kubwa ya kiafya. Wajumbe wanashiriki pia semina kwa ajili ya wasichana. WAWATA inatarajia pia kuandaa mpango kazi pamoja na kupitia maazimio ya Semina ya wasichana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, (The Catholic Women Of Tanzania Association) ni chombo kinachowaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa kunako mwaka 1972 kwa lengo la kujitakatifuza na kutakatifuza malimwengu. Madhumuni makuu ya WAWATA ni pamoja na kuwaunganisha wanawake Wakatoliki nchini Tanzania katika juhudi zao zinazowahusu kama Wakristo, wanawake, na raia, wakiwa katika vikundi mbalimbali ambavyo hasa lengo lao ni kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Taswira ya Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA ni kuona kila mwanamke mkatoliki wa Tanzania anaelewa nafasi yake na wajibu wake wa Kikristo kuanzia ngazi ya Familia, Jumuiya, Kanisa, jamii na Taifa kwa ujumla, pia wanakuwa na maendeleo fungamani ya kiuchumi ili kukidhi mahitaji msingi ya familia na hivyo kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na Jamii, na kufanya maisha ya hapa duniani kuwa taa na nuru katika Ulimwengu kama mawakili wa Yesu Kristo.

Malengo: Jumuiya hii ilipoanzishwa kunako mwaka 1972, ilijiwekea malengo ili kupata mwelekeo utakaowafikisha mahali ambapo wanaweza kufanya tathmini ya Utume wao katika Kanisa na katika mchakato wa ukombozi mzima wa mwanamke katika suala la maisha ya kiroho, ujinga, umaskini na maradhi. Malengo haya yalijikita zaidi katika mchakato wa kumjenga mwanamke katika imani thabiti ya Kikristo, ili aweze kuishi maisha matakatifu na hatimaye ayatakatifuze malimwengu kwa ushuhuda wa maisha yake kama kielelezo cha imani tendaji. WAWATA inapania kumjengea mwanamke uwezo wa kujikomboa yeye na familia yake ili akomboe wengine wenye shida, yatima na wasiojiweza. Kumwendeleza mwanamke kielimu na kiujuzi ili aondokane na giza la kiroho, ujinga wa akili na aendeleze wengine. Kumwezesha mwanamke katika masuala ya kiuchumi ili kutegemeza familia, Kanisa na kuwategemeza wengine.

Tangu kuanzishwa kwa WAWATA, wanawake wamekuwa mstari wa mbele kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa. Wamekuwa ni wadau wakuu wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, kwa sasa wanashiriki kikamilifu katika maamuzi na utekelezaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji katika ngazi mbali mbali. WAWATA inaendelea kujielekeza katika malezi makini kwa vijana wa kizazi kipya. Jumuiya ya WAWATA, Alhamisi tarehe 5 Desemba 2019 imeanza mkutano wake wa 40 utakaohitimishwa hapo tarehe 9 Desemba 2019 kwa kuwashirikisha wajumbe wa WAWATA kutoka majimbo mbali mbali ya Kanisa la Tanzania. Hii ni nafasi ya kupembua kwa kina na mapana taarifa za WAWATA kutoka Majimboni, Afya ya wanawake wa Tanzania hususan kuhusu ugonjwa wa Saratani ambao kwa sasa ni changamoto kubwa ya kiafya kwa jamii ya watanzania. Wajumbe wanashiriki pia semina kwa ajili ya wasichana. WAWATA inatarajia pia kuandaa mpango kazi pamoja na kupitia maazimio ya Semina ya wasichana.

Askofu Desiderius Rwoma, Mwenyekiti wa Idara ya Utume wa Walei katika Baraza la Maasfofu Katoliki Tanzania, TEC, katika hotuba yake elekezi, amewashukuru WAWATA kwa kushiriki katika harakati mbalimbali za kujikomboa kiuchumi k.m: kuondokana na umaskini, unyanyasaji, maradhi ili kwa kujikomboa kwao waweze kushiriki pia kuwakomboa wengine na hivyo kuwa ni chachu ya maendeleo fungamani kuanzia ngazi ya familia hadi taifa katika ujumla wake. Kanisa limeshuhudia WAWATA ikianzisha na kutekeleza miradi mbalimbali katika vikundi, vigango, parokia majimbo. Uongozi unaowajibika, ukweli, uwazi na uaminifu katika kutekeleza hayo yote ni muhimu sana ili shughuli hizo zote ziweze kuwa fungamani na hatimaye kuleta mabadildiko makubwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utekelezaji wa miradi mbali mbali inayobuniwa na kuendeshwa na WAWATA inaweza kupata ufanisi mkubwa ikiwa kama itaendeshwa na wote, lakini hata katika ngazi ya mtu binafsi, jambo la msingi ni kujenga tabiaya uvumilivu na kwamba, mafanikio hayawezi kupatika kwa kufumba na kufumbua!

Askofu Desiderius Rwoma anasema, amani ni msingi wa wema, heshima na maendeleo endelevu ya binadamu; ni paji na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha na kumwajibisha binadamu. Amani ni tunda la upendo linalopaswa kuboreshwa kwa njia ya malezi ya dhamiri nyofu; ukweli na uhuru; usalama wa raia na mali zao; kwa kulinda na kuheshimu utu wa binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi. Amewataka WAWATA kujizatiti katika ujenzi wa amani dumifu, inayofumbatwa katika ukweli, haki, upendo na uhuru kamili. Changamoto za haki na amani zinapaswa kuanza kujadiliwa ndani ya familia kwa sababu watu wengi wana kiu ya amani. Ikumbukwe kwamba, familia ni shule ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati. Ni mahali pa kujifunza kupenda na kupendwa, kusamehe na kusahau.

Wasichana wajengewe pia mazingira yatakayokuza na kustawisha misingi ya haki na amani ili kuondokana na ubabe wa mfumo dume ambao kwa sasa umepitwa na wakati. WAWATA wawe ni sehemu ya mabadiliko katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuondokana na utumwa, nyanyaso na ukatili unaofanywa ndani ya familia kwa vipigo vya wanawake majumbani. WAWATA kuanzia kwenye familia wanaweza kuwa ni chachu ya mabadiliko katika jamii ya watanzania kwa kuweka uwiano sawa kati ya fursa za elimu kwa wanawake, kwani mwelekeo wa sasa ni kutaka kuwaendeleza wasichana zaidi ambao kwa hakika kwa miaka mingi walibaguliwa na kukoseshwa fursa za elimu. Pengine ni wakati muafaka sasa wa kuhakikisha kwamba, watu wa Mungu nchini Tanzania wanawekeza pia katika elimu na makuzi ya vijana wa kiume.

Wakati huo huo, Mama Evaline Malisa Ntenga, Mjumbe wa Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC, katika mkutano wake mkuu uliofanyika mjini Dakar, Senegal kuanzia tarehe 15-22 Oktoba 2018, uliazimia kutekeleza mambo makuu manne katika kipindi cha mwaka 2018 hadi mwaka 2022. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kadiri ya mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume: “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Wanawake Wakatoliki wanahamasishwa kujali na kuzisaidia familia zinazoishi katika mazingira magumu na hatarishi, kwa kulinda na kudumisha utu na heshima yao kama binadamu!

Wanawake Wakatoliki wanahimizwa kujifunga kibwebwe ili kutokomeza ubaguzi, nyanyaso na ukatili wanaofanyiwa wanawake majumbani kwa kuwa na maandalizi bora kwa wanandoa watarajiwa, ili kukuza na kushirikishana upendo wa dhati, ili kuwaimarisha wanandoa na hatimaye, waweze kutakatifuzana. Wanawake Wakatoliki wanahimizwa kujielimisha zaidi ili hatimaye, waweze kuitikia wito wa utakatifu wa maisha!

“Kwa Upendo wa Kristo Tutumikie na Kuwajibika”

WAWATA 2019

 

06 December 2019, 18:13