Tafuta

Vatican News
Umoja wa Mataifa unaipongeza Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kwa mchango wake katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, umoja na mafungamano ya kijamii duniani. Umoja wa Mataifa unaipongeza Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kwa mchango wake katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, umoja na mafungamano ya kijamii duniani.  (ANSA)

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio katika kukuza haki, amani na huduma!

Katibu mkuu katika mazungumzo yake na viongozi wakuu wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio amegusia kuhusu wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani; huduma ya kibinadamu kwa wakimbizi na wahamiaji; mchakato wa haki, amani, upatanisho na umoja wa kitaifa huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Wamezungumzia pia kampeni ya uragibishaji inayopania kufuta adhabu ya kifo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Professa Andrea Riccardi, akiwa kijana mbichi bado, hapo tarehe 7 Februari 1968 alianzisha Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao yake Makuu mjini Roma na kujikita katika  mambo makuu matatu yaani: Sala, Maskini na Amani duniani. Kanisa kuu la Bikira Maria wa Trastevere liliko mjini Roma, likawa ni makao makuu ya sala, maisha na utume wao sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio aliwataka wanajumuiya wake kukazia sana utambulisho wao. Alisema, Neno la Mungu ni huduma ya kwanza inayopaswa kutolewa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kuiwezesha kuchota nguvu inayobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, tayari kusonga mbele kwa imani na matumaini makubwa. Maskini hata katika umaskini wao wanaweza kusaidiana na hivyo kuunda jumuiya inayojipambanua kwa kuwasaidia maskini, wazee na watoto, kielelezo makini cha jamii inayojali na kuwajibika.

Wazee wanapokumbana na upweke hasi wanakata tamaa na hiki ni kielelezo hasi cha jamii, changamoto kwa vijana na wazee kuchangamana na kusaidiana kwa kutambua kwamba, sala zao ni kama uvumba na ni zawadi kubwa kwa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio. Jamii isiyotunza wazee na vijana, haina matumaini kwa siku za usoni. Sera na mikakati ya uchumi na maendeleo haina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki na mahitaji yake msingi. Wakimbizi ni watu wanaotoka katika maeneo ya vita na majanga asilia; ni watu wanaotafuta amani na usalama wa maisha yao, mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuwa kweli ni vyombo vya ujenzi wa misingi ya haki, amani na utulivu, kwa kujikita katika sala na majadiliano zaidi, kwa watu kutambua na kuthamini utambulisho wao pamoja na kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga umoja na urafiki kati ya watu wa mataifa. Ni katika muktadha huu, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres, Jumatano tarehe 18 Desemba 2019 ametembelea Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inayoendelea kujipambanua katika mchakato wa kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Katibu mkuu katika mazungumzo yake na viongozi wakuu wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio amegusia kuhusu wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani; huduma ya kibinadamu kwa wakimbizi na wahamiaji; mchakato wa haki, amani, upatanisho na umoja wa kitaifa huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Wamezungumzia pia kampeni ya uragibishaji inayopania kufuta adhabu ya kifo duniani kwa sababu inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu. Kwa namna ya pekee, wamezungumzia hali tete ya kisiasa, kijamii na kiuchumi nchini Sudan ya Kusini na umuhimu wa kuvihusisha vikundi vyote vya upinzani hata vile ambavyo havikutia saini kwenye Makubaliano ya Amani ya Addis Ababa. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres ameishukuru na kuipongeza Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kwa mchango wake mkubwa katika mustakabali wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, haki, amani na majadiliano ya kidini na kiekumene. Kwa hakika katika medani hizi, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio imekuwa ni mfano bora wa kuigwa.

Mwishoni mwa mazungumzo yake, Katibu mkuu amepata nafasi ya kuonana na kusalimiana na baadhi ya wakimbizi na wahamiaji waliowasili hivi karibuni nchini Italia kwa kutumia njia za kibinadamu. Amewatakia mwanzo mwema wa maisha mapya pamoja na kuendeleza mchakato wa ujenzi wa jamii shirikishi. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, mara nyingi amekazia: umuhimu kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene. Anawataka watu wa Mungu kuangalia madhara ya vita na vitendo vya kigaidi; waamini watambue kwamba, wao ni vyombo na wajenzi wa amani duniani na kwamba kuna umuhimu wa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kusikiliza na kujibu kwa makini kilio cha amani duniani na kwamba, vijana wanapaswa kushirikishwa katika ujenzi wa amani duniani! Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa sasa dunia imegeuka kuwa kama tambara bovu kutokana na madhara ya vita yanayoendelea kujionesha sehemu mbali mbali za dunia, kumbe, mikutano kama hii inatoa changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kujikita katika kutafuta na kudumisha amani duniani bila kuchoka.

Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ambako mipasuko na migawanyiko inaonekana wazi kabisa, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga madaraja ya amani, ili kukuza na kudumisha umoja; kuganga na kuponya madonda ya kihistoria, ili kukoleza amani na utulivu duniani. Biashara haramu ya silaha, vita na vitendo vya kigaidi ni kati ya mambo yanayoendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya watu duniani, lakini waathirika wakubwa ni maskini na wanyonge ndani ya jamii. Kumbe, waamini wa dini mbali mbali wanaowajibu wa kujikita katika mchakato wa kutafauta na kudumisha amani duniani, kwani huu ni wajibu msingi wa dini zote duniani. Baba Mtakatifu anasema, anapenda kuungana nao kwa ajili ya kuombea amani duniani, ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa udugu na maelewano hasa katika maeneo ambamo mtutu wa bunduki bado unarindima! Waamini wanaweza kuwa ni wajenzi wa amani na kwamba, ni wajibu wa viongozi kuwa ni madaraja ya ujenzi wa amani duniani, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha amani kutoka sehemu mbali mbali za dunia, matumaini ya vijana wa kizazi kipya badala ya kugubikwa na uchoyo pamoja na ubinafsi.

Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha vijana wa kizazi kipya katika shule ya amani, ili waweze kuwa ni wajenzi na walezi wa amani duniani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa sasa dunia imegeuka kuwa kama tambara bovu kutokana na madhara ya vita yanayoendelea kujionesha sehemu mbali mbali za dunia, kumbe, mikutano kama hii inatoa changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kujikita katika kutafuta na kudumisha amani duniani bila kuchoka. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ambako mipasuko na migawanyiko inaonekana wazi kabisa, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga madaraja ya amani, ili kukuza na kudumisha umoja; kuganga na kuponya madonda ya kihistoria, ili kukoleza amani na utulivu duniani. Biashara haramu ya silaha, vita na vitendo vya kigaidi ni kati ya mambo yanayoendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya watu duniani, lakini waathirika wakubwa ni maskini na wanyonge ndani ya jamii.

Kumbe, waamini wa dini mbali mbali wanaowajibu wa kujikita katika mchakato wa kutafauta na kudumisha amani duniani, kwani huu ni wajibu msingi wa dini zote duniani. Baba Mtakatifu anasema, anapenda kuungana nao kwa ajili ya kuombea amani duniani, ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa udugu na maelewano hasa katika maeneo ambamo mtutu wa bunduki bado unarindima! Waamini wanaweza kuwa ni wajenzi wa amani na kwamba, ni wajibu wa viongozi kuwa ni madaraja ya ujenzi wa amani duniani, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha amani kutoka sehemu mbali mbali za dunia, matumaini ya vijana wa kizazi kipya badala ya kugubikwa na uchoyo pamoja na ubinafsi. Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha vijana wa kizazi kipya katika shule ya amani, ili waweze kuwa ni wajenzi na walezi wa amani duniani.

Umoja wa Mataifa

 

19 December 2019, 10:25