Tafuta

Vatican News
Watu wenye mapenzi mema wameshtushwa sana na mauaji ya kutishwa yaliyofanywa na Boko Haramu, tarehe 25 Desemba 2019. Watu wenye mapenzi mema wameshtushwa sana na mauaji ya kutishwa yaliyofanywa na Boko Haramu, tarehe 25 Desemba 2019.  (AFP or licensors)

Mauaji ya Kikatili nchini Nigeria yawashtua wapenda amani duniani

Askofu mkuu Ignatius Ayau Kaigama wa Jimbo kuu la Abuja anasikitika kusema, vitendo vya kigaidi nchini Nigeria vinalenga kuchochea chuki na uhasama kati ya Wakristo na Waislam. Kwa upande wake, Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria, amewataka wananchi wake kushikamana na kamwe wasikubali kutumbukia katika vurugu za kidini kwani madhara yake ni makubwa kwa mafungamano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

 Habari za mauaji ya kutisha dhidi ya Wakristo kumi na mmoja kutoka nchini Nigeria wakati wa Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2019 zimepokelewa kwa uchungu mkubwa. Haya ni mauaji yaliyofanywa na Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram huko Kaskazini Magharibi mwa Nigeria. Mauaji hayo ni ujumbe mahususi kwa Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Boko Haram pamoja na vikundi mbali mbali vya kigaidi vimeamua kulipiza kisasi baada ya mauaji ya kiongozi mkuu wa Kikundi cha Kigaidi Bwan Abu Bakr al-Baghdadi pamoja na msemaji wake mkuu bwana Abul Hasan Al Muhajir waliouwawa hivi karibuni wakati wa shambulizi lililofanywa na Jeshi la Marekani nchini Siria. Askofu mkuu Ignatius Ayau Kaigama wa Jimbo kuu la Abuja anasikitika kusema, vitendo vya kigaidi nchini Nigeria vinalenga kuchochea chuki na uhasama kati ya Wakristo na Waislam. Kwa upande wake, Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria, amewataka wananchi wake kushikamana na kamwe wasikubali kutumbukia katika vurugu za kidini kwani madhara yake ni makubwa kwa ustawi na mafungamano ya wananchi wa Nigeria.

Itakumbukwa kwamba, idadi ya watu nchini Nigeria inakadiriwa kuwa ni milioni 196 na kati ya wakristo ni milioni 91. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete ili kupambana na vitendo vya kigaidi, vita na misimamo mikali ya kidini inayohatarisha uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini. Ikumbukwe kwamba, uhuru wa kidini unafumbatwa katika mambo makuu matatu: Mosi ni umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali; Pili, ni kulinda na kudumisha amani na utulivu kama chachu muhimu ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Tatu, ni majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi; hii ni mbinu mkakati inayoweza kuleta suluhu ya migogoro mingi. Uhuru wa kuabudu na kidini ni nguzo ya haki msingi za binadamu na ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Uhuru wa kuabudu na kidini unaweza kusaidia kukuza na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu.

Hii ni chachu ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa na kwamba, ukweli na uwazi ni kanuni msingi katika majadiliano ya kidini na kiekumene. Kumbe, hapa kuna haja ya kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini umechambuliwa na kufafanuliwa vyema katika Tamko la Haki Msingi za Binadamu. Kwa kuheshimu, kuthamini na kutekeleza haki hizi msingi, Jumuiya ya Kimataifa itaweza kujizatiti zaidi katika mapambano dhidi ya ubaguzi unaoweza kufanywa kwa misingi ya kidini au imani ya mtu. Watu wanapaswa kukuza na kudumisha uhuru wa kujieleza kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi. Vyombo vya mawasiliano ya jamii vinaweza kusaidia kuchangia mchakato wa kuimarisha demokrasia shirikishi sanjari na mapambano dhidi ya mipasuko ya kidini na kiimani.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinabainisha kwamba, kumekuwepo na ongezeko kubwa la vitendo vya ukosefu wa uvumilivu wa kidini na kiimani, sehemu mbali mbali za dunia. Kwa bahati mbaya matukio kama haya yamepenyeza mizizi yake na kujikita hata katika vitendo vya uhalifu kitaifa, kikanda na kimataifa. Katika makundi yote, Wakristo ni kundi la kwanza katika orodha linalonyanyaswa na kudhulumiwa. Inakadiriwa kwamba, asilimia 61% ya idadi ya watu wote duniani, wanaishi katika nchi ambamo uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu hauheshimiwi wala kuthaminiwa. Katika kipindi cha mwaka 2018 kumekuwepo na matukio mengi ya uvunjwaji wa uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu sehemu mbali mbali za dunia, ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Mauaji Nigeria
28 December 2019, 15:07