Tafuta

Vatican News
Askofu Mkuu Justin Welby aonesha mshikamano wake wa dhati na familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini pamoja na DRC wanaoteseka kutokana vita na majanga asilia. Askofu Mkuu Justin Welby aonesha mshikamano wake wa dhati na familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini pamoja na DRC wanaoteseka kutokana vita na majanga asilia. 

Askofu mkuu Justin Welby: Yesu Kristo ni mwanga wa matumaini!

Askofu mkuu Welby katika ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2019 anapenda kuombea amani ya kudumu nchini Sudan ya Kusini. DRC ni nchi nyingine Barani Afrika ambayo imetikiswa sana na vita ya wenyewe kwa wenyewe pamoja na milipuko ya magonjwa ya kuambukiza kama vile Ebola. Analishukuru Kanisa kwa kuendelea kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu kwa watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sherehe ya Noeli ni ukumbusho endelevu wa Fumbo la Umwilisho, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Ni muda muafaka kwa watu wote kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu; ukomavu wa imani na mshikamano wa upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sherehe za Noeli, Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameungana na Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Canterbury ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikani pamoja na Mchungaji John Chalmers, ambaye aliwahi kuwa Mchungaji mkuu wa Kanisa la Presibiterian huko nchini Scotland, wanapenda kutoa salam na matashi mema ya Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2019 pamoja na Mwaka Mpya 2020 kwa viongozi wa kisiasa nchini Sudan ya Kusini.

Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Canterbury ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikani pamoja na Baba Mtakatifu Francisko wameonesha nia ya kutembelea kwa pamoja nchini Sudan ya Kusini ili kuwatia shime katika mchakato wa umoja na upatanisho wa kitaifa; ili watu wa Mungu waweze kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwamba, amani na utulivu ni kichocheo kikubwa cha maendeleo. Askofu mkuu Welby katika ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2019 anapenda kuombea amani ya kudumu nchini Sudan ya Kusini. DRC ni nchi nyingine Barani Afrika ambayo imetikiswa sana na vita ya wenyewe kwa wenyewe pamoja na milipuko ya magonjwa ya kuambukiza kama vile Ebola. Analishukuru Kanisa kwa kuendelea kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu kwa kuendelea kutoa huduma kwa waathirika wa vita na magonjwa hayo.

Kanisa linapenda kuwa ni chombo cha upendo na huduma kwa binadamu ambaye, Mwenyezi Mungu amekuja ili kumkomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Noeli ni sherehe ya imani, matumaini na mapendo miongoni mwa watu wa Mungu! Kristo Yesu ni mwanga angavu unaofukuzia mbali giza la chuki, kifo na uhasama. Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahimizwa kufukuzia mbali giza la maisha ya kiroho kwa kujivika utu mpya na kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Yesu, Njia, Ukweli na Uzima. Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa matumaini kwa wale waliokata tamaa, mwanga kwa wale wanaotembea katika giza na uvuli wa mauti. Wawe ni vyombo vya huruma na upendo; mwanga wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kwa hakika, Jumuiya ya Kimataifa inawahitaji mashuhuda wa mwanga wa maisha, upendo na matumaini kwa wale waliokata tamaa.

Askofu Mkuu Welby
28 December 2019, 14:52