Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linaiomba Serikali ya Tanzania kutaza upya Sheria Namba 1 ya Mwaka 2015 kuhusu utaratibu wa wageni na ajira kwa wageni. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linaiomba Serikali ya Tanzania kutaza upya Sheria Namba 1 ya Mwaka 2015 kuhusu utaratibu wa wageni na ajira kwa wageni. 

Maaskofu Katoliki Tanzania: Wamisionari si watu wa mshahara!

Wamisonari wanapaswa kutofautishwa na wageni wengine wa kazi za mshahara na wawekezaji wa kibiashara na kiuchumi wanaotafuta pesa hivyo, amesema, umefika wakati sheria hiyo inayohusiana na vibali vya kuishi nchini Tanzania kwa wageni wakiwamo wamisonari, itazamwe upya. “Wamisonari wasitazamwe kama waajiriwa wa kigeni; wameajiriwa na nani?

Na Sarah Pelaji, - Dar es Salaam na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S, - Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limesema umisionari siyo mabaki ya ukoloni mambaoleo wala uwekezaji hivyo, sheria inayowatambua wamisonari kama vile ni waajiriwa na wawekezaji wa kigeni katika biashara inapaswa kutazamwa upya. Aidha, limesisitiza kuzingatiwa kwa Ibara ya 19 (1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasisitiza shughuli za uendeshaji wa taasisi za dini kuwa huru, bila kuingiliwa na mtu au chombo chochote ili kulinda uhuru wa kuabudu. Katiba hiyo inasema: “19.-(1) Kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake. (2) Bila ya kuathiri sheria zinazohusika za Jamhuri ya Muungano, kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari ya mtu ya binafsi, na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.” Sheria Namba 1 ya Mwaka 2015 inayohusu uratibu wa wageni na ajira kwa wageni inawatambua wamisionari kama vile ni wawekezaji wa kigeni jambo ambalo si sahihi.

Hayo yamebainishwa na Askofu mkuu Damian Denis Dallu, Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari nchini Tanzania, katika maadhimisho ya Kufunga Mwezi Maalumu wa Kimisonari na Kuwakaribisha Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimisionari kutoka nchi mbalimbali za Afrika zinazozungumza lugha ya Kiingereza (Ndesa). Maadhimisho hayo yamefanyika Msimbazi Center, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam. Amesema, kutokana na shughuli zake mbalimbali za kuwajenga, kuwaimarisha na kuwalinda watu kiroho na kimwili, Kanisa linaonesha wazi lilivyo tofauti na ukoloni ambao muda ulipotimia Desemba 9, 1961 uliondoka na Kanisa kubaki likikua na kukomaa hali inayodhihirisha wazi kuwa, shughuli za kimisonari siyo mabaki ya ukoloni. Kwa mujibu wa Askofu mkuu Dallu, Papa Benedikto wa XV aliwahi kusisitiza kuwa, shughuli za kimisionari lazima ziwe mbali na shughuli za mataifa na kiulimwengu hivyo, wamisionari wakatae kila namna ya kutafuta maslahi binafsi katika kazi zao na badala yake, wajikite kumtafuta na kumweneza Kristo Yesu kwa ajili ya utakatifu kupitia matendo mema yenye mvuto na mashiko!

Askofu mkuu Dallu anasema, “Kwa msingi huo, mpinzani mkuu wa umisionari ni yule anayefanya kinyume na lengo hilo la Kanisa akibadili na kupotosha kwa makusudi kuwa wamisionari ni waajiriwa na kwamba, bahati mbaya sana, sheria hii ambayo kwa yenyewe ni nzuri, inajumuisha wamisionari na wageni wengine waajiriwa…” amesema. Wamisonari wanapaswa kutofautishwa na wageni wengine wa kazi za mshahara na wawekezaji wa kibiashara na kiuchumi wanaotafuta pesa hivyo, amesema, umefika wakati sheria hiyo inayohusiana na vibali vya kuishi nchini Tanzania kwa wageni wakiwamo wamisonari, itazamwe upya. “Wamisonari wasitazamwe kama waajiriwa wa kigeni; wameajiriwa na nani; sisi Maaskofu kweli tutatoa wapi pesa za kuwalipa? Tutawalipa nini?... Sheria hii ikiondolewa, wamisonari hawatahusika kuomba vibali vya kazi hivyo, kuishi kwao na kufanyakazi hautakuwa na ukomo maalumu,” amesema Askofu mkuu Damian Denis Dallu.

Ameongeza kusema, “Hii ni sheria inayotuchanganya sana na kuihangaisha serikali…. Sheria hiyo inamtaka mmisionari kuomba kibali kila baada ya miaka miwili na pia, inamwekea ukomo mmisionari huyo kufanya kazi nchini na baada ya miaka mitano, lazima aondoke.” Kwa mujibu wa Askofu Mkuu Dallu, kutokana na hali hiyo, miito mbalimbali kupitia umisionari imekuwa hairithishwi ipasavyo kwa waamini na badala yake, mwenye wito huo huuishi na kuondoka nao muda wake unapoisha. Hata hivyo alisema licha ya changamoto hiyo, lengo la kutungwa kwa sheria hiyo lilikuwa zuri la kuhakikisha Tanzania inakuwa na wataalamu wake wa kutosha ifikapo mwaka 2025, hivyo changamoto zilizopo zinapaswa kuondolewa. Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amesema kwamba, hivi karibuni palitokea changamoto kwa wamisionari waliotakiwa kupata vibali ingawa, baada ya kwenda Serikalini na kujadiliana na wahusika suala hili lilishughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi. Amesisitiza kuwa, umisionari ni pamoja na kuishi maisha ya amani, upendo na mshikamano bila uhalifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania.

Ibada ya Misa Takatifu iliongozwa na Askofu mkuu Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na kuhudhuriwa na Askofu mkuu Giampietro Dal Toso, Katibu Mwambata, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, Askofu Mkuu Marek Solczynski, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, maaskofu na wasimamizi wa kitume wa majimbo mbalimbali nchini Tanzania. Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa pamoja na umati wa waamini kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Dar es Salaam Kwa upande wake, Askofu mkuu Giampietro Dal Toso amesema, Kanisa nchini Tanzania na Bara la Afrika kwa jumla linazidi kuwa la kimisonari kwa kuwa wamisonari wake sasa wanatumwa na kwenda kuinjilisha katika maeneo mbalimbali duniani. Wakati huo huo, Askofu mkuu Marek Solczynski, Balozi wa Vatican nchini Tanzania amesema katika maadhimisho hayo kuwa, anashangazwa namna nguvu ya Mungu yenye baraka inavyofanya kazi nchini Tanzania na Afrika kwa jumla.

PMS Tanzania
16 November 2019, 13:13