Tafuta

Vatican News
Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ulioandikwa na Askofu mkuu Damian Dennis Dallu kuhusu: Maadhimisho ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni kwa Mwaka 2019. Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ulioandikwa na Askofu mkuu Damian Dennis Dallu kuhusu: Maadhimisho ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni kwa Mwaka 2019. 

Siku ya Kimisionari Ulimwenguni 2019: Ujumbe: Maaskofu Tanzania

Tunawaalika na kusisitiza: Kukuza roho ya umisionari na ushuhuda wa imani. Papa pia anasititiza “Missio ad gentes”, yaani uinjilishaji kwa mataifa yote. Tunawaalika tuangalie katika maeneo yetu uwepo wa wale wote ambao hawajapokea Habari Njema. Tuwainjilishe kwa mifano na matendo yetu mazuri, yaani tutoe ushuhuda wa imani yetu. Pia tuwatembelee na kuwapelekea Habari Njema.

Na Askofu Mkuu Damian Denis Dallu, - Dar Es Salaam.

Ndugu Wapendwa, Baba Makatifu Francisko aliutangaza mwezi Oktoba mwaka 2019 kuwa Mwezi Maalum wa Kimisionari. Kwa tangazo hilo, Baba Mtakatifu analialika Kanisa zima lihuishe, lifanye majitoleo na kupyaisha mtazamo na wajibu wake wa Umisionari. Pia anataka lijikite katika uinjilishaji wa watu wote, yaani “Missio ad gentes”, na kufanya kumbukumbu ya karne moja ya Barua ya Kichungaji Maximum Illud ya Papa Benedikto XV (30 Novemba 1919). Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba barua hii ilikuwa sauti ya kinabii na yenye mtazamo wa mbali kuhusiana na utume wa Kanisa, kwa sababu ililenga kupyaisha na kuchochea Umisionari katika Kanisa, na hatimaye kuwasaidia watu kupata wokovu. Baba Mtakatifu ameona kaulimbiu ya Ujumbe ni “Umebatizwa na Kutumwa Kutangaza Injili. Kanisa la Kristo katika Umisionari ulimwenguni”. Baba Mtakatifu Francisko anasema kuwa kuadhimisha mwezi huu kutasaidia kutambua upya na kwa upana maana ya Umisionari na ya Imani yetu kwa Yesu Kristo, pia wajibu tuliopewa wakati wa ubatizo wetu.

Kwa njia ya imani hiyo tunamiminiwa huruma ya Mungu katika Sakramenti ya Ubatizo. Pia watu wataimarishwa kiroho kwa kuwa Mungu anataka watu wote waokolewe kwa kuutambua ukweli na kuionja huruma yake kwa njia ya Utume wa Kanisa, ambalo ni Sakramenti ya kiulimwengu ya wokovu (Rej. 1Tim 2:4, Lumen Gentium, 48). Ndugu wapendwa, Kanisa linalojiwekea lengo la kusonga mbele hadi miisho ya dunia linahitaji daima upyaisho endelevu wa kimisionari. Lengo la upyaisho huo ni kumwezesha kila mtu anayefundisha juu ya Mungu awe kweli mtu wa Mungu. Hata hivyo, Baba Mtakatifu anasifu kuwa kwa sasa waamini wakristo wanatumia vipawa vyao vya Ubatizo wakiitikia wito huu kwa ukarimu katika kulitetea Kanisa lao, na wengi wapo tayari kuliacha taifa lao na lugha yao na hata Makanisa yao mahalia na kujitoa kutumwa kwenda kokote kule, kwenye ulimwengu ambao haujapata mabadiliko yaletwayo na Sakramenti za Yesu Kristo na Kanisa lake takatifu.

Baba Mtakatifu Francisko anatutafakarisha kuwa wokovu wa watu ulimwenguni aliotujalia Mungu kwa njia ya Yesu Kristo ulimfanya Papa Benedikto XV kutoa wito wa kukomesha mambo haya: utaifa na ukabila, udhalilishaji na udhalimu, chuki na fitina miongoni mwa jamii ya kimataifa au upotoshaji wa ufundishaji Injili unaolenga maslahi binafsi, vitendo vya unyanyasaji kimabavu, kiuchumi, kijeshi na utawala wa kikoloni. Katika ujumbe huu pia, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wajumbe wa Sinodi Maalum ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuwa sinodi hiyo iwe kwao kama Pentekoste mpya, inayofungua wazi milango ya Kanisa kwenye tamaduni zitakazobaki zimefungwa na kutenga watu na Imani ya Kikristo. Pia anawaasa wavunjilie mbali vikwazo vya aina yoyote ile vya dunia, dini na tamaduni zinazomfanya binadamu awe mtumwa wa dhambi. Kupokea imani ya Kikristo kuwe kwao njia ya kumjua na kumkaribisha Kristo waliyempokea katika Ubatizo, Mungu asiyejulikana ambaye mababu zao walimtafuta, bila kumtambua, aweze sasa kutambulikana nao katika uenezaji wa Injili.

Baba Mtakatifu pia analialika Kanisa kufuata mfano wa Mama Bikira Maria, wa kumtangaza Kristo na kuongeza waamini wapya katika Kanisa lake. Baba Mtakatifu anayataja Mashirika ya Kipapa kama alivyofanya Mtangulizi wake kwenye barua ya “Maximum Illud”. Anasema Mashirika ya Kipapa ni rasilimali ya Umisionari na ni mtandao wa dunia nzima wa kumuunga mkono Baba Mtakatifu katika majukumu yake ya Kimisionari: kwa Sala, Roho ya kimisionari, na Ukarimu kutoka kwa wakristo duniani kote. Michango hiyo humsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro katika juhudi zake za Uinjilishaji kwa baadhi   ya Makanisa yenye uhitaji maalum yaani: Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambalo hujikita katika uenezaji wa imani duniani kote; Shirika la Mtakatifu Petro Mtume - hufanya utume wa kuwaandaa waseminari wa makanisa mahalia na nyumba za malezi za mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume; Shirika la Umoja wa Kimisionari, hilo huhamasisha na kutia moyo ukuzaji wa Imani ya Kikristo kwa watu wote; mwisho ni Shirika la Utoto Mtakatifu ambalo husaidia kuwalea watoto katika imani ili watoto hao wawasaidie wenzao.

Baba Mtakatifu anasisitiza kuwa kwa kutoa msukumo mpya kwa Mashirika ya Kipapa hasa mwezi wa Maalum wa Oktoba 2019, utume wa Mashirika ya kipapa na umisionari kwa ujumla utazaa matunda maridhawa. Baba Mtakatifu ametoa maeneo muhimu ya kufanyia kazi kama ifuatavyo: Kila mtu binafsi aweze kukutana na Bwana wetu Yesu Kristo aliyepo katika Kanisa lake, katika Ekaristi Takatifu, katika Neno la Mungu na katika Sala binafsi na ya jumuiya. Ushuhuda: watakatifu wamisionari, wafiadini na waungama imani kama taswira ya kujipambanua na Kanisa lililoenea popote duniani. Malezi ya kimisionari, kibiblia, kikatekesi, kiroho na kitaalimungu. Upendo wa kimisionari, hasa kuongeza ukarimu kwa wahitaji na kwa Baba Mtakatifu aweze kuyategemeza makanisa yanayohitaji zaidi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania nalo limeongeza maeneo mengine ya kufanyia kazi. Mojawapo ya sababu za Baba Mtakatifu Francisko kutoa maeneo haya ni kujibu hoja za wale Wakatoliki wanaobadili madhehebu, wanatoka dhehebu la Kikatoliki na kwenda kwenye madhehebu ya Kipentekoste. Wanasema kwamba wanakwenda huko kumtafuta Kristo. Kuna msemo maarufu unaotumiwa na wahubiri wa Makanisa hayo: "have you found Christ- come to us and meet Christ" –maana yake,  umekutana  na  Kristo  njoo  kwetu  ukutane na Kristo. Sasa Baba Mtakatifu anawaambia katika Mwezi wa pekee na wakati mwingine kwamba hata katika Kanisa letu wanakutana na Kristo katika Ekaristi Takatifu, yaani Misa Takatifu: humo kuna Kristo ambaye ni mponyaji wa makovu na magonjwa yote.

Vivyo hivyo wengine wanasema wanakwenda kwa Makanisa ya Kipentekoste ili kusikiliza Neno. Hivyo Baba Mtakatifu anawambia kwamba hata katika Kanisa Katoliki wanaweza wakakutana na Kristo katika Neno lake yaani Kristo mwenyewe anapoongea, wakapata mahubiri mazuri, malezi ya katekesi, kitaalimungu (yaani yenye ufafanuzi makini na mzuri) na kiroho kwa njia hiyo wanakutana na Mungu. Wengine wanasema wanakwenda kwa makanisa ya kipentekoste kupata ushuhuda wa watu wengine wanaoishi maisha ya ukristo. Baba Mtakatifu anawambia kwamba hata katika Kanisa Katoliki wanaweza wakakutana na Kristo katika Neno lake, yaani Kristo mwenyewe anapoongea, wakapata mahubiri mazuri, malezi ya katekesi, kiteolojia (yaani yenye ufafanuzi makini na mzuri) na kiroho; kwa njia hiyo wanakutana na Mungu.

Wengine wanasema wanakwenda kwa makanisa ya Kipentekoste kupata ushuhuda wa watu wengine wanaoishi maisha ya ukristo. Baba Mtakatifu anawaambia wakristo hao kuwa hakuna ushuhuda unaozidi ushuhuda wa watakatifu, yaani wale ambao tayari wameishi maisha ya ukristo hapa duniani na sasa wako huko mbinguni wakifurahia raha ya milele. Wale wanaoenda katika makanisa ya kipentekoste wanapata ushuhuda kwa watu wa kawaida ambao bado wapo hapa duniani na hawajui maisha ya kesho yatakuwaje, lakini katika Kanisa Katoliki wanapata ushuhuda wa watakatifu ambao tayari wapo mbinguni. Wapo wanaosema kuwa wanakwenda katika madhehebu ya kipentekoste kwa sababu huko waamini wanajaliana. Sasa Baba Mtakatifu anawaalika waamini wote wazidishe upendo wa kimisionari, yaani kujaliana wao kwa wao na kuwasaidia wenye shida.

MWEZI MAALUM WA KIMISIONARI (1919 – 2019) : Wapendwa, tunaadhimisha Dominika ya Misioni tukiwa katikati ya Mwezi Maalum wa Kimisionari. Tunawaalika na kusisitiza, kama mnavyoona katika ujumbe wa Baba Mtakatifu, kukuza roho ya Umisionari au ya Uenezaji   wa Imani katika majimbo yetu, parokia zetu, Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo, na hata katika utume wa familia. Baba Mtakatifu pia anasititiza “Missio ad gentes”, yaani uinjilishaji kwa mataifa yote. Tunawaalika tuangalie katika maeneo yetu uwepo wa wale wote ambao hawajapokea Habari Njema. Tuwainjilishe kwa mifano na matendo yetu mazuri, yaani tutoe ushuhuda wa imani yetu. Pia tuwatembelee na kuwapelekea Habari Njema. Kama mnavyojua, katika maeneo yetu wapo watu wengi ambao bado wamebakia katika imani za wazee wetu wa zamani; nao tuwatembelee na kuongea nao kuhusu kumwongokea Kristo.

Hapa tukumbuke kuwa mwanzoni tulisubiri wamisionari kutoka nje lakini sasa hivi sisi ndio tunapaswa kuwa wamisionari kwa wenzetu. Wapo pia wale waliobatizwa lakini kwa sababu ya udhaifu wao wamelegea na kuacha imani yao, hata wengine wamejiunga na makanisa ya kipentekoste au madhehebu mengine. Sisi tuangalie ni kitu kipi wanachokipata huko ambacho kwetu hakipo. Mwaka huu, pamoja na kuadhimisha Mwezi Maalum wa Kimisionari, sisi katika Kanisa la Tanzania tunaendelea kuishi dhamira ya familia. Tunapenda kuwatia moyo kuwa tuendelee kulifanyia kazi wazo hili maana kwa sasa tunayo mahitaji makubwa katika familia. Tunaendelea kuwaalika kusoma ujumbe wa Kwaresima wa 2019 uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuhusu familia. Tunawaalika kuwa ujumbe huo uendelee kuwa rejea mahususi katika familia na Jumuiya Ndogo Ndogo. Kanisa la Tanzania linapenda kutoa matashi mema na linaombea mafanikio ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Tunayatakia Makanisa hayo ya Ukanda Amazonia kuwa Sinodi hiyo isaidie kukuza umoja na mshikamano katika imani, na isaidie kuyaunganisha makanisa hayo na Kanisa lote la Mungu duniani.

Shukrani: Tunapenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru sana kwa ukarimu wenu mliotoa mwaka jana katika Dominika ya Misioni 2018. Ukarimu huo ulienda katika Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Tunazidi kuwatia moyo kuongeza ukarimu wenu kulingana na uhalisia wa kutoa kadiri ya Mungu anavyowajalia. Mkitajirishwa katika vitu vyote mpate kuwa na ukarimu wote, umpatiao Mungu shukrani kwa kazi yetu’’ (2 Kor 9:11). Maadhimisho ya MWEZI MAALUM WA KIMISIONARI yawe kichocheo muhimu kwa Kanisa la Tanzania kuongeza kiwango cha ukarimu wetu kwenye mfuko wa pamoja huko Roma, hususani Shirika la Uenezaji wa Imani, ambalo linaangalia mahitaji makubwa ya Kanisa zima. Tunawashukuru sana wote kwa kuendelea kutoa ukarimu mkubwa zaidi kila mwaka. Hilo tunaweza kuliona katika Jedwali  linaloonesha  uhalisia wa ukarimu wa kila Jimbo: Halmashauri za Walei, Vyama vya Kitume, Jumuiya Ndogo Ndogo, Mashirika ya Kitawa na Maisha ya Wakfu, Seminari kubwa na ndogo, Nyumba za Malezi ya Kitawa, Familia na Watu binafsi.

Tunawashukuru sana kwa namna ya pekee wadau au marafiki wa Mashirika ya Kipapa kwa kuchangia kwa ukarimu mkubwa sana kutoka kwa baadhi   ya majimbo yetu ya Tanzania, kama inavyooneshwa katika Jedwali letu. Shukrani nyingi kwa Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwa mwamko mkubwa wa ukarimu wenu mkubwa mlioutoa kupitia Bahasha kutoka Parokia zenu. Tunawashukuru sana pia watu binafsi na familia mbalimbali kwa ukarimu mkubwa mlioutoa kwa njia ya bahasha na M-Pesa. Tunawaalika tena kuchangia kwa ukarimu Jumapili ya Kimisionari Ulimwenguni kwa Mwaka 2019,  ili kutegemeza Kanisa lote la Mungu maana mahitaji ya Kanisa yanazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka. Tutoe kwa ukarimu tukiungana na Baba Mtakatifu Francisko katika kuimarisha utume wetu wa kimisionari katika ulimwengu, na hasa katika nchi zetu za misionari

Siku ya Kimisionari 2019
17 October 2019, 10:24