Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 30 ya Mwaka C wa Kanisa: Sala inamwilishwa katika imani, matumaini na unyenyekevu. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 30 ya Mwaka C wa Kanisa: Sala inamwilishwa katika imani, matumaini na unyenyekevu.  (Vatican Media)

Tafakari Jumapili 30 Mwaka C: Sala: Imani, Unyenyekevu na Haki!

sala inasimikwa katika imani, unyenyekevu, toba na wongofu wa ndani. Ombi la msamaha ni mwenendo wa kwanza wa Sala ya maombi kama anavyoshuhudia Mtoza ushuru katika Injili ya Jumapili hii. Huu ni unyenyekevu wa matumaini unaomrejesha mwamini katika mwanga wa ushirika unaofumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Sala inasimikwa katika: imani, matumaini na haki!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Tunatafakari leo masomo ya dominika ya 30 ya Mwaka C wa Kanisa. Sala ni maisha ya moyo mpya. Mababa wa Kanisa wanasisitizia umuhimu wa kumkumbuka Mwenyezi Mungu katika sala inayosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu. Kiini cha sala ni toba na wongofu wa ndani. Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa anafafanua kwa ufasaha mkubwa aina tatu za Sala ya Yesu katika maisha ya waamini kwa kusema kwamba, kwanza kabisa anasali kwa ajili yao kwa sababu ni Kuhani wao. Anasali ndani yao kwa kuwa ni kichwa cha Fumbo la Mwili wa Kanisa na hatimaye, waamini wanamkimbilia kwa kuwa ni Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kumbe, sala inasimikwa katika imani, unyenyekevu, toba na wongofu wa ndani. Ombi la msamaha ni mwenendo wa kwanza wa Sala ya maombi kama anavyoshuhudia Mtoza ushuru katika Injili ya Jumapili hii. Huu ni unyenyekevu wa matumaini unaomrejesha mwamini katika mwanga wa ushirika unaofumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Jumapili hii, Kanisa linahitimisha Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kwa Ibada ya Misa Takatifu. Sinodi hii imeongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”.

Somo la kwanza (YBS 35:15b-17, 20-22a ) ni kutoka katika kitabu cha Yoshua bin Sira. Kitabu hiki ni cha kipindi cha kihistoria ambapo dola ya Wayunani (Wagiriki) walitawala karibu dunia nzima. Katika uyahudi wayunani hawa walitawala kimabavu na walitafuta kila njia kufuta tamaduni za kiyahudi na kuleta tamaduni zao za kiyunani. Ni kipindi ambayo uyahudi ilitawaliwa kwa uonevu na kila aina ya uvunjifu wa haki. Ni katika kipindi hiki Wayahudi wanaikumbuka Torati na kujishikamanisha nayo. Kwa njia ya Torati wanalikumbuka Agano ambalo Mungu aliliweka nao. Katika Agano Mungu alijitambulisha kuwa Mungu aliye karibu na wote wanaomlilia. Ni Mungu ambaye huisikiliza sala ya mtu mnyenyekevu, mtu asiye na msaada, mtu ambaye kimbilio pekee alilonalo ni kwake. Walikumbuka kuwa Mungu wao ni Mungu wa haki na hata pale ambapo hawaoni matumaini yeye kwa wakati wake atawajibu. Hii ndiyo Hekima ya watu wa Mungu Israeli, hekima inayowavuta kumtumaini Mungu katika nyakati ngumu za maisha yao ya kijamii na ya kisiasa. Haikuwa hekima ya kimapinduzi kwani aliyekuwa na uwezo na nguvu za kuwapigania ni Mungu pekee.

Somo la pili (2 Tim 3:14- 4:2) ni kutoka katika waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Timoteo. Paulo yuko kifungoni Rumi na inaonekana anaandika sehemu ya barua hii akiwa tayari ameshasomewa hukumu yake ambayo ni hukumu ya kifo. Katika kipindi hicho kigumu cha maisha yake anatoa ushuhuda wa uthabiti wa imani kwa Timoteo. Anasema sasa “anamiminwa”. Hii ni lugha ya kikuhani. Na kilichokuwa kikimiminwa na kuhani ni sadaka aliyokuwa anaitoa. Paulo anaona kufa kwake kama ni sadaka ambayo kuhani anaiotoa kwa Mungu. Katika wakati huu Paulo anapiga picha ya maisha yake yote na jinsi alivyoishi anaona kuwa alikuwa katika mapambano makali ya kulinda imani. Na katika mapambano hayo anakiri kuwa amepambana vizuri na imani ameilinda. Na sasa anangojea taji ya haki, anangojea kukutana na mhukumu mwenye haki, Yesu Kristo ambaye ndilo taji lenyewe.

Mwishoni Paulo anamweleza Timotheo kuwa katika mashitaka yake hayo hakuna aliyekuwa upande wake, wote walimwacha peke yake. Inawezekana alilenga kumaanisha kuwa hukumu haikuwa nzuri kwa upande wake lakini pia inawezekana alimaanisha kuwa wale walipaswa kutoa ushahidi wa kumtetea hawakumtetea na hivyo wakamwaacha ahukumiwe. Kwa namna yoyote ile Paulo haangalii doa hilo lililotokea bali anaangalia upande mzuri zaidi kwamba Mungu hakumwacha na alisimama pamoja naye akamtia nguvu. Somo hili linaonesha ushuhuda mkubwa sana wa ukomavu wa imani ya Paulo. Imani isiyotetereka hata katika magumu. Ni jambo la pekee sana kuona kuwa Paulo katika mashitaka yake yote hakusisitiza kuachiliwa huru bali alisisitiza zaidi wokovu wa roho yake. Alitamani kuona kuwa yote anayoyapitia kama magumu yapate kibali mbele ya Mungu yamfaidie kupata wokovu.

Injili (Lk 18:9-14) Katika Injili ya dominika ya leo ambayo ni kutoka kwa mwinjili Luka, Yesu anatoa mfano wa sala ya mfarisayo na ya mtoza ushuru. Kama ilivyo kawaida, mwinjili Luka kabla ya kuelezea mfano huo wa Yesu anatambulisha mfano unahusu nini. Na injili inaanza hivi “akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote”. Na hiki ndicho alichofanya mfarisayo katika sala yake, alitoa orodha ya mambo mema anayofanya na hapo hapo akataja na madhambi ya mtoza ushuru aliyekuwa Hekaluni akisali. Kwa Farisayo Yesu anawatahadharisha pia wanafunzi wake ili wasijikute nao wakimjingea Mungu kwa sala ya kiburi na majivuno, wakijihesabia haki hata kwa mazuri wanayofanya. Sala ya mtoza ushuru inasifiwa. Na Yesu anasema alishuka nyumbani amehesabiwa haki. Yeye alitambua udogo wake mbele ya Mungu. kiini cha sala yake kilikuwa ni majuto na uchungu kwa makosa yake. Alisali akijipigapiga kifua, alama ambayo nasi tumeichukua tunaposali “Nakuungamia Mungu mwenyezi” au sala nyingine za toba. Mwisho anatoa fundisho “kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa na ye ajidhiliye atakwezwa” kuonesha namna ifaayo ya kumjongea Mungu kwa sala.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News masomo ya leo yanatuonesha kwa namna iliyo wazi kabisa ni namna gani mkristo anapaswa kusali. Sala, matendo mema na mazoezi mbalimbali ya kiroho kama vile mafungo, hija na majitoleo mbalimbali ni mambo muhimu sana katika maisha ya mkristo. Pamoja na umuhimu wake katika maisha ya mkristo, mapokeo ya Kanisa yamesisitiza daima juu ya uhusiano wa matendo hayo na undani wa maisha ya kiroho ya mtu anayeyafanya. Kwamba matendo haya ni alama ya nje ya kuonesha kiu ya ndani ya mtu kutafuta wongovu na wokovu wake. Hayampi mtu uhakika kama wa kimahesabu kwa sababu wokovu si suala la kimahesabu bali liko daima mikononi mwa Mungu. Maandiko Matakatifu tunayoyatafakari katika dominika hii yanalenga kutuonesha kipengele hiki muhimu katika maisha yetu ya sala. Tusali kwa imani na kwa uhakika kuwa Mungu anatusikia ila tujisihesabie haki kuwa kwa kusali kwetu na kwa kutimiza matakwa ya nje ya imani zetu tunamuwajibisha Mungu kutuhesabia haki. Huko ni kuvuka mipaka ya ubinadamu wetu na kulazimisha kuingia katika uwanda wa kimungu. Ni masomo yanayotualika kuwa wanyenyekevu katika kuiishi imani yetu katika namna ya kujenga mahusiano yetu na Mungu kwa njia ya sala.

Liturujia 30
26 October 2019, 08:20