Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 30 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Huruma ya Mungu ni zawadi inayofumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu, imani na mapendo! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 30 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Huruma ya Mungu ni zawadi inayofumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu, imani na mapendo!  (Vatican Media)

Tafakari Jumapili 30 Mwaka C: Huruma ya Mungu na kiburi cha binadamu!

Haki ni fadhila adilifu iliyo na utashi wa kudumu na thabiti wa kumpa Mungu na jirani iliyo haki yao. Haki ina tabia ya kuwaheshimu watu wengine, inajikita katika mawazo sahihi na unyofu wa mwenendo kwa jirani. Inaheshimu utu, sifa njema na staha kwa jina lake. Fadhila ya haki inasimikwa katika upendo! Jitahidini kuifahamu mizizi ya dhambi, ili kuweza kutenda kwa haki na upendo.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.

Wapendwa taifa la Mungu, karibuni sana katika tafakari ya neno la Mungu dominika hii ya leo. Dhamira inayotuongoza leo ni swala la haki na usawa na pia dhana ya utajiri, mali na umaskini. Mababa wa Kanisa wanafundisha kwamba, haki ni fadhila adilifu iliyo na utashi wa kudumu na thabiti wa kumpa Mungu na jirani iliyo haki yao. Haki ina tabia ya kuwaheshimu watu wengine, inajikita katika mawazo sahihi na unyofu wa mwenendo kwa jirani. Inaheshimu utu, sifa njema na staha kwa jina lake. Fadhila ya haki inasimikwa katika upendo! Ni vyema waamini wakajitaabisha kuifahamu mizizi ya dhambi, ili kuweza kutenda kwa haki na upendo kwa Mungu na jirani zao. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni zawadi inayofumbatwa katika unyenyekevu, toba na wongofu wa ndani! Kiburi na majivuno ni kaburi la utu na heshima ya binadamu!

Ndugu zangu dhana ya haki, usawa, utajiri, mali, umaskini, dhambi n.k inaweza ikapata maana na sura mbalimbali pengine kadiri ya tamaduni, mila, desturi, imani, mahali na wakati na pengine mahitaji ya watu.  Katika kitabu ‘Hadithi za Kiafrika” kilichoandikwa na Padre Joseph Healey tunakutana na simulizi hili – Padre Jack hakujisikia vizuri katika parokia yake kwani alijiona kuwa na vitu vingi kama umeme jua, tanki la maji, nyumba ya bati n.k. Yeye aliishi kati ya watu maskini na parokia yake ilikuwa ni moja ya parokia maskini huko Shinyanga. Siku moja alipokuwa anakwenda kigangoni na katekista Charles, padre huyu mmisionari alikiri jinsi alivyojisikia vibaya kwa kuishi kama tajiri miongoni mwa maskini. Katekista Charles alikunja uso wake kwa mshangao. Halafu akamwambia padre, wewe ni maskini zaidi yetu hapa kijijini. Padre Jack alishangaa sana. Katekista akamwambia wewe huna watoto wala wajukuu.

Habari juu ya haki, usawa, utajiri, mali, umaskini n.k una mtazamo tofauti kabisa katika Biblia na hasa katika Agano Jipya. Katika injili ya Mt. 5:1 …tunasikia juu ya heri, heri maskini wa roho. Katika Mt. 19:16-30 tunasikia habari jinsi ilivyo vigumu kwa tajiri kuingia mbinguni. Je, utajiri na umaskini wa kweli ni upi? Biblia yatuambia nini? Jibu la kibiblia kuhusu utajiri wa kweli liko wazi. Tajiri wa kweli na mwingi wa fadhila ni Mungu Baba peke yake. Yote tuliyo nayo yatoka kwake na ni mali yake. Pale kwenye lango la Hekalu kina Petro na Yohane waliombwa fedha na yule kiwete. Petro anajibu wazi kuwa hawana fedha wala dhahabu ila kwa jina la Yesu wa Nazareti wakamwamuru yule kiwete aamke. Naye mara akapona, akaingia hekaluni na pamoja na watu wegine anaingia hekaluni kumwabudu Mungu - Mdo. 3:1-10.

Katika Injili ya leo tunaona yule mfarisayo akijivuna. Anaorodhesha utajiri wake na mambo anayofanya…. Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi na wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma (sheria inasema mara moja kwa juma), mimi hutoa zaka katika mapato yangu yote …Ingawa anaanza na shukrani kwa Mungu, mwishoni anajisifu yeye. Tafsiri ya "The American Bible" inasema hakuinamisha kichwa. Tafsiri ya Kigiriki inasema alisimama n.k kuonesha kukosa unyenyekevu. Anamlazimisha Mungu abariki mambo yake. Yule mfarisayo anarudi kama alivyokwenda. Alilinda hadhi yake ya haki lakini bila kumtegemea Mungu. Yule mwingine alionesha unyenyekevu – aliinamisha kichwa, hahesabu mali yake na hali yake, pengine hana na hasa ile inayokubalika kwa Mungu.

Pengine kama angekuwa nayo ingekuwa ya wizi.  Yeye alijiweka katika mazingira ya unyenyekevu na upole na ikawa sala yake: hamdai Mungu abariki anayofanya bali anatafuta huruma ya Mungu. Anatambua hali yake, anataka neema ya Mungu ili kutengeneza hali yake – Mungu anampatia. Yule maskini anarudi nyumbani akiwa amepatanishwa na Mungu, amejawa haki. Ndugu zangu hatuna budi kutambua kuwa sala ina lengo la kumwabudu, kumshukuru, kuomba toba na kuomba neema zake Mungu. Yule mtoza ushuru alikosa misingi hii ya sala. Tunasoma kutoka Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, katika kipengele ‘Ufunuo’ kuwa Mungu, mwanzo na mwisho wa yote, aweza kufahamika kwetu kwa njia ya viumbe tukitumia mwanga wa akili ya mwanadamu. Hakika fundisho hili lamtaka mwanadamu kuutambua ukuu wa Mungu na uweza wake.

Hakika yule anayefahamu hilo basi katika maisha yake atakiwa kumchagua Mungu. Kwa kutumia akili aliyojaliwa na yenye uwezo wa kujua na kufahamu, basi anaweza kumchagua huyo ambaye ni asili na chanzo cha utajiri wote. Hapa tunaona changamoto kubwa sana. Yule farisayo ambaye ni mwelewa anakosa ufahamu huu. Alijitegemea yeye mwenyewe. Huyu mtoza ushuru na ambaye mbele ya mfarisayo ni mdhambi anaweza kutambua hili. Ndugu zangu, maisha yetu katika uhusiano na Mungu siyo swala la maelewano kama ilivyo katika biashara – nina hela kiasi hiki, mali yako yana thamani kiasi hiki. Basi lipa kiasi hiki. Pia siyo swala la kuishi au kutenda ili kupata zawadi. Sawa zawadi ipo. Katika somo la pili – Paulo anasema Bwana ndiye chanzo na sababu ya ushindi wake. Anasema atamwaga damu – imani kwa Kristo – imani ameilinda, vita ameimaliza – uhakika wa alichofanya, anapata taji.

Mtume Paulo aliishi maisha yake akibaki katika misingi ya sala. Aliwekeza na Kristo.  Hakika mbele ya Mungu hatuna budi kutambua mapungufu yetu, umaskini wetu, mipaka yetu, hatuna budi kuona soni kwa madhambi yetu. Tutafakarishwe na unyenyekevu wa nabii Isa. 6:5 - mimi ni mchafu na Mungu akamtakasa na akaenda kuhubiri. Hivyo tunaalikwa kufungua mioyo yetu kama ilivyo katika mwanzo wa ibada ya ekaristi – ungamo la dhambi tukitafuta huruma ya Mungu. Tutafakarishwe na mfano huu wa bibi tajiri aliyekuwa na vitu vingi sana hapa duniani. Alipofariki dunia alibahatika kuingia mbinguni. Alipokelewa na malaika na kupelekwa sehemu yake ya kukaa. Huku akiongozana na malaika wake aliona watakatifu wenzake wakiwa wamekaa katika ufahari mkubwa. Mwisho akafika katika sehemu yake na kumbe kulikuwa na vitu vidogo sana na vichache.

Malaika kwa unyenyekevu akamwonesha mahali pake pa kukaa. Mahali hapo hapakumfurahisha kabisa kwani hapakuwa na ufahari mkubwa kama alivyozoea duniani. Malaika akamwambia hana budi kuridhika na mahali hapa kwani vifaa vya ujenzi ulivyotuma toka duniani vilitosha kujenga hicho kibanda. Malaika akaondoka akaenda zake. Mtakatifu Jerome anasema ni tajiri wa kutosha yule aliye maskini katika Kristo. Ushuhuda huu ni mkubwa sana kwani Kristo ndiye mwana mrithi wa Mungu na yule amfuataye Kristo atapata yote yaliyo yake Mungu.  Hatuna budi kujiuliza sisi wakristo - utajiri wetu ukoje au ni upi? Je, tumewekeza katika nini au kitu gani au hali gani? Ni nini tunaomba au tunataka zaidi toka kwa Mungu? Sala zetu zinabeba kitu gani au aina gani ya maombi? Ni jinsi gani tunamshukuru Mungu? Tumsifu Yesu Kristo.

22 October 2019, 16:49