Tafuta

Vatican News
Padre Katunzi anasema kile kinachojaza moyo basi na mdomo unatangaza,tukijazwa upendo tutaishi upendo na watu watajua maneno ya upendo,maneno ya faraja yanayowapatia nguvu Padre Katunzi anasema kile kinachojaza moyo basi na mdomo unatangaza,tukijazwa upendo tutaishi upendo na watu watajua maneno ya upendo,maneno ya faraja yanayowapatia nguvu 

Pd.Deodatus Katunzi:umisionari wetu uanzie ndani yetu tulipo na kujiinjilisha!

Tunaalikwa kwenda mbali zaidi,umisionari wetu uanzie ndani,pale tulipo mtu mwenyewe ni kujiinjilisha maneno ya Kristo.Tukijazwa upendo tutaishi upendo na watu watajua maneno ya upendo na ya faraja yanayowapatia nguvu na tutakuwa tumekuza hali ya kimisionari.Ni Maneno ya Padre Katunzi Mkurugenzi wa Mawasiliano Jimbo katoliki Bukoba,Tanzania na Radio Mbiu alipotembelea Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Idhaa ya Kiswahili  Radio Vatican imetembelewa na Padre Deodatus Katunzi Kagashe, Mkurugenzi wa Mawasiliano Jimbo katoliki la Bukoba Tanzania akiwa katika hija yake ya kiroho nchini Italia na kwa namna ya pekee katika mji wa Vatican. Akizungumzia juu ya uzoefu wa hija hiyo hasa katika mji wa Roma ujulikanao tangu zamani  kama mji mtakatifu na pia mji wa milele, anathibitisha kuwa ni kweli mji wa Roma ni wa milele ( eternal city)” na kwamba jambo moja ambalo amefurahia katika uwepo wake ni kuona kweli mataifa mengi kutoka nchi mbalimbali na karibu wanakuja katika mji wa milele na ndipo, “nikakumbuka ule msemo kwamba, barabara zote zinaelekea Roma. Ni kweli watu wanakuja Roma kwa sababu mbalimbali, lakini kwa upande wangu wa kiinamani nimeguswa na mambo kadha”. 

Mtakatifu Paulo II na Mtakatifu Yohane wa XXIII

Padre Katunzi akijaribu kufafanua kuhusu yale yaliyo mgusa zaidi amesema: “nitataja mawili matatu: kwanza  kuona pale ambapo Kanisa nililoamini, Kanisa Katoliki, kiti cha Baba Mtakatifu, Kanisa la Mtakatifu Petro, lakini pia Kanisa la Laterano (yaani la Mtakatifu Yohane) ambapo tumejifunza katika historia, tumekuwa tukifuatilia, lakini sasa tumefika na kuona kile ambacho kinaendelea, hapo basi imani inaimarika. Lakini pia katika mji wa Roma kuna mambo mengi ambayo nimeyafurahia na kuguswa na Mtakatifu Yohane Paulo II na Papa Yohane XXXIII.  Kwa hiyo nilipata nafasi nzuri ya kufika na kuona pale ambapo hawa wamelala katika Bwana na kwamba sasa wametajwa watakatifu na imekuwa ni nafasi  nyingine ya kuendelea kuwaomba ili waliombee Kanisa, watuombee na sisi katika uinjilishaji wetu ili kufanya kazi kama ambavyo Bwana anatutaka…

Kuudhuria katekesi na matukio ya Baba Mtakatifu

Kuhusiana na fursa ya Fr. Katunzi aliyoipata akiwa mjini Roma hasa ya kusikiliza au kuudhuria baadhi ya matukio mbalimbali ya Baba Mtakatifu Franciko amesema kuwa: “ Nimepata fursa ya kuudhuria, tunaziita pope's audience (yaani katekesi zake za kila Jumatano) pamoja na Baba Mtakatifu,ambapo anafundisha, anatoa neno lake, na  katika mengi ambayo ninaweza kuchota anatukumbusha kwamba Mungu ni huruma yenyewe, katika utendaji wetu, basi tudhihirishe huyo Mungu mwenye huruma, hata katika kupeleka Habari Njema, tuipeleke katika muktadha huo na ili watu wamuone Mungu anayewahurumia, Mungu anayewagusa na kwa njia hiyo basi mawasiliano yetu ya Radio, mitandao mingine ya kijamii iweze kuwavutia katika Kristo”.

Karama ya huruma ya Baba Mtakatifu inajionesha

Fr Katunzi vile vile kaguswa kama karama ya huruma aliyo nayo Baba Mtakatifu Francisko ambayo anajaribu kuionesha, kuitoa na kufundisha  kwa wengine na kwa maana hiyo anasema: “Ndiyo mwaliko huo”. Kwani “Injili yenyewe ni mwaliko wa kutaka kusambaza Habari Njema. Injili ni Habari Njema na Habari Njema ni Kristo. Kristo ni Mungu. Mungu ndiye upendo. Mungu ndiye huruma, Mungu ndiye kila kitu”. Kwa maana hiyo, “ tunapoisambaza Habari Njema hiyo basi tunawiwa. Hatuna jinsi ni  labda kumtangaza yeye aliyetuhurumia na kutupenda; lakini pia tupo katika mwezi wa kumi. Mwezi wa kumi kama ambavyo mmekuwa mkitoa habari na kufundisha, hata katika Radio nyingine, wamekuwa wakitoa habari  juu ya Mwezi Maalum wa kimisionari na ambao Baba Mtakatifu Benedikto XV anatutaka kuutafakari umisionari, kwa  barua yake ya  Maximum illud na kama anavyoanza katika barua hiyo.

Ni jambo jema na heshima kuwa mtangazaji wa habari njema

Ni jambo la furaha, jambo la heshima, jambo zito na la kicho kuwa mtangazaji wa Habari Njema na kwa hiyo basi katika Mwezi huu nimeshuhudia pia watu kutoka mbali na karibu wanakuja, wanaionesha ile roho ya kimisionari, yaani katika nafasi ya kwanza ya kimisionari anayetumwa kutoka sehemu A kwenda B, kwa hiyo wamefika, lakini pia tunaalikwa kwenda mbali zaidi. Umisionari wetu uanzie ndani, pale tulipo, mtu mwenyewe ni kujiinjilisha, na kisha iva basi maneno ya Kristo kwamba kile kinachojaza moyo na mdomo unatangaza, tukijazwa upendo tutaishi upendo na watu watajua maneno ya upendo, maneno ya faraja yanayowapatia nguvu, na kwa namna hyo tunakuwa tumekuza ile hali ya kimisionari ambayo Baba Mtakatifu anatukumbusha kuwa watu wa sala, lakini pia kuwezesha kazi za kimisionari ziendelee mbele.

Upotoshaji wa habari katika mitandao ya kijamii

Padre Katunzi akifafanua juu ya utoaji wa habari njema na ya amani, kwa watu ambao wanapotosha habari zetu, za Baba Mtakatifu Francisko na habari nyinginezo anasema katika nafasi ya kwanza, “tukumbuke katika tasnia ya habari kuna miiko yake, na katika miiko hiyo ya  habari ambayo tunaitoa iwe kweli habari njema, katika mazingira yetu, tunatangaza habari njema. Sisi tunamhubiri Kristo na katika kumhubiri Kristo kwa kawaida  Kanisa Katoliki lina namna yake ya kutoa mafundisho ambayo yanajikita katika misingi yake. Kwanza kabisa ni katika Neno la Mungu, na  kwa namna hiyo tunapokuwa tunafundisha, daima turejee katika Neno la Mungu, lakini pia tukumbuke Mafundisho ya Kanisa na ambayo  yanajikita kwa kile tuitacho: “mapokeo hai ya Kanisa”. Na   humo kuna kweli ambazo tunazichota, na zimedumu kwa miaka mingi, katika  kwa karne nyingi na zinasaidia kuendelea kukuza ukweli na kusukuma mbele! Pamoja na hiyo pia kuna  mamlaka fundishi ya Kanisa yanayo mgusa Baba Mtakatifu, kwa maana hiyo katika hirakia  hiyo,  basi tuendelee kuvuta mnororo huo. Lakini kama  kuna kitu ambacho kinapaswa kusemewa, hapo kuna utaratibu, kama mtu hajaelewa jambo basi afuate taratibu ili apate kuelewa, hivyo kusudi anapotoa jambo hilo liweze kuwa kweli la furaha na kuwajenga watu.

Tanzania imeshatimiza miaka 150 tangu kuingia kwa mara ya kwanza uinjishaji

Sehemu nyingine ni kuhusu umisionari, Tanzania  ambao tayari miaka 150 imeshatimizwa  ya uinjilishaji, na katika mantiki hiyo Padre Katuniza amesema: “Mwezi wa kumi ni Mwezi Maalum wa Kimisionari na kwa Tanzania bara, tumeadhimisha miaka 150  tayari na tupo sasa katika mwaka wa 151  wa Injili ilipoweka mizizi yake ya kwanza katika ardhi yetu”. Ameongeza: “ walio tuletea habari njema hiyo katika mazingira yao, walitoka jasho, walijinyima, wakaweza kutupa hiyo tunu njema. Ni zamu yetu sasa ili tuhakikishe kijiti hiki hakitufii mikononi, hasa wanza fuifahamu imani yetu. Ni lazima  mimi na wewe mpendwa msikilizaji (msomaji) wa Radio Vatican tujifunze imani. Akitumia hata msemo wa wahenga anasema “Hata hivyo jambo usilo lifahamu ni sawa na usiku wa giza, ukifahamu imani, utaishi kwa furaha, hautaishi kwa woga.

Na katika sehemu ya pili, Padre Katunzi anaendelea kusema kuwa wamisionari walijitolea rasilimali zao. Katika mazingira ya Tanzania, sehemu nyingi walijenga makanisa ya kudumu , walijenga shule, walijenga zahanati ili kumhudumia mtu katika nyaja zote. Kwa maana hiyo Padre Katunzi amesisitiza “Ni waalike watanzania wenzangu na wasikizaji wote (wasomaji) tulione hilo, tuguse maisha ya wenzetu kwamba tumeinjilishwa sasa kwa miaka 150 imepita  na tuone miaka mingine ijayo, tuweke urithi kwa hawa ambao mwenyezi Mungu amependa sasa sisi tu watangulizi wao wa imani, katika miaka hii na miaka mingine ijayo na ili tuwapatie jambo lililo jema, lakini pia na miundo mbinu iwepo ya kuweza kuendeleza habari njema kwa wote!

Tujue misingi mikuu ya uandishi wa habari

Kwa kuzingatia misingi mikuu ya uandishi wa habari ambayo imegawanyika katika vipengele vya usahihi, uhuru, kutopendelea upande wowote, ubinadamu, na uwajibikaji, utaona kwamba  hayo yote hayapo mbali sana na Tamko juu ya uhuru wa dini. Haki ya mtu binafsi na ya jumuiya  ya kuwa na uhuru wa kijamii na wa kiserikali katika masuala ya dini, ambapo Mtakatifu Paulo VI alitaka mambo hayo yakumbukwe daima kwenye  Waraka wa Dignitatis Humanae (heshima ya kiutu).

Na  katika utangulizi  Barua ya Dignitatis Humanae anasema, wanadamu wa nyakati hizi wanazidi kuwa macho sana kuhusu heshima ya kiutu (Dignitatis Humanae); na inaongezeka idadi ya wale wanaodai kuwa binadamu wafanye mashauri yao wenyewe na washike wajibu wao kwa uhuru katika vitendo vyao na wasiwe watendaji wa kulazimishwa, bali waongozwe na hisia ya wajibu wao. Wakati huohuo wanadai kikomo cha kisheria cha nguvu ya serikali ili kuzuia kubanwa mno kwa uhuru wa kila mmoja na jumuiya. Dai hili kwa ajili ya uhuru katika jumuiya za watu linahusika hasa na mema ya kiroho katika mtu, na hasa yale yanayohusu matendo huru ya dini katika jamii. Mtaguso Mkuu wa  II wa Vatican  unazingatia kwa uangalifu hamu hizo za moyoni na ukiazimia kutamka jinsi zinavyoendana na ukweli na haki, unachunguza Mapokeo matakatifu na mafundisho ya Kanisa ambako huchotwa vitu vipya ambavyo mara zote hulingana na vile vya zamani. Sikiliza mahojiano hayo kwa kirefu...

FR KATUNZI
24 October 2019, 15:21