Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki  nchini Nigeria katika harakati za kampeni za kisiasa, lawataka wananchi kuwa na umoja na mshikamano na kuheshimu haki za kisheria katika chaguzi za kisiasa. Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Nigeria katika harakati za kampeni za kisiasa, lawataka wananchi kuwa na umoja na mshikamano na kuheshimu haki za kisheria katika chaguzi za kisiasa.  (AFP or licensors)

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria: Umoja & Mshikamano

Maaskofu Katoliki nchini Nigeria wanaomba kuwa na umoja na mshikamano kati ya makabila, dini na vyombo vya siasa. Umoja huo uonekane katika upangaji wa safu ya uongozi, utumiaji wa lasrimali na kuruhusu uhuru na haki sawa za kuabudu. Maaskofu wamesisitiza tunu za uwajibikaji, uwazi, uhuru wa kisheria, kuheshimu haki za binadamu, na utawala wa sheria na kufanya chaguzi.

Na Padre Angelo Shikombe, - Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, CBCN, limefanya mkutano wa pili wa mwaka katika kituo cha huruma ya Mungu kilichoko mjini Ogun Nigeria. Mkutano huo uliofanyika kati ya tarehe 11 hadi 20 Septemba, 2019 umelenga kujadili mambo makuu yanayoliathiri Kanisa la Nigeria. Katika mkutano huo, Baraza la Maaskofu limeonesha msimamo wake unaoungana na mamlaka ya kipapa dhidi ya mashambulio yanayofanywa na baadhi ya viongozi wa Kanisa ya kumpinga Papa Francisko.  Baraza hilo la Maaskofu linayatambua mamlaka na limeahidi kuonesha ushirikiano wake wa kichungji. Aidha, Maaskofu wameeleza matatizo yanayowasibu ikiwemo mauaji ya vibaka, wizi wa kutumia silaha, uvamizi wa makazi ya watu unaofanywa na vyombo vya ulinzi na mmomonyoko wa maadili. Migogoro kati ya jamii ya wafugaji na wakulima, na matukio ya Bokoharam. Haya yote yanapelekea watu kupoteza maisha yao. Hatua za udhibiti zimechukuliwa na Serikali lakini bado jitihada zinahitajika zaidi.

Maaskofu wanasali kwa ajili ya amani na kuziombea familia zilizoathirika. Maaskofu wanatoa rai kwa raia wote kutii sheria za nchi na kushika amri za Mungu, aidha Serikali inapaswa kuwajengea mazingira ya amani wananchi pamoja na sekta binafsi. Serikali inatakiwa kuwakomboa mateka waliotekwa nyara na kikundi cha Leah Sharibu. Wakimshukuru Mungu, Maaskofu wanaomba kuwa na mshikamano kati ya makabila, dini na vyombo vya siasa. Umoja huo unapaswa kuonekana katika upangaji wasafu ya uongozi, utumiaji wa lasrimali na kuruhusu uhuru na haki sawa za kuabudu. Kwa kuzingatia haya haki, umoja, amani na maendeleo yatapatikana nchini Nigeria. Wakimshukuru Mungu kwa hatua waliyofikia katika mahusiano ya kisiasa, kiuchumi na kimaadili wamesisitiza tunu za uwajibikaji, uwazi, uhuru wa kisheria, kuheshimu haki za binadamu, kuheshimu utawala wa sheria na kufanya chaguzi za haki na amani. Haya yote yatafikiwa kama kila mmoja anazingatia mafao ya pamoja.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria limekemea vikali uvamizi na harakati za makundi ya vijana huko nchini Afrika ya kusini; ambayo  yaliyopelekea watu wengi kupoteza mali zao na wengine kukimbia makazi yao au kuuawa kikatili. Wamelishutumu Baraza la Maaskofu nchini Afrika kusini, SACBC, kwa kutochukua hatua za kukemea machafuko hayo.  Wamewakumbusha maaskofu wenzao safari ndefu ya kimahusiano iliyopo kati ya Nigeria na Afrika kusini. Wameongelea pia masuala ya ndoa ambayo kwa sasa yanazidi kuwa changamoto kubwa. Kutokana na hali ya kiuchumi ndoa za kikristo zinapungua na misingi ya familia inaanza kuyumba. Maaskofu wametoa rai kwa wazazi kuzingatia malezi ya familia na kulinda tunu za kifamilia kama vile uaminifu, heshima, uchaji, nidhamu, maadili na uwajibikaji. Aidha kutoutupa utamaduni wa kiafrika wa kuheshimu na kuwajali watu wazima. Maaskofu wamewapongeza mapadre na watawa wanaojituma katika wito wao.

Aidha Maaskofu wametoa wito kwa wakleri na watawa kutumia busara, kuwa na mahusiano chanya na vijana, kuwalea vijana katika utume wao, kukuza miito na kujitoa kikamilifu katika kumtumikia Mungu. Katika kuadhimisha miaka mia moja ya wosia wa kipapa uliotolewa na Papa Benedikto XV ujulikanao kama "Maximum Illud" yaani "Shughuli za kimisionari" juu ya umisionari wa Kanisa, Maaskofu wameungana na Baba Mtakatifu Francisko kuliandaa taifa la Mungu kwa sala na tafakari kwa mwezi wa kimisionari. Maandaliza tayari yametanguliwa na maadhimisho mbalimbali ya kitaifa na kimataifa likiwemo Kongamano la kimataifa lililofanyika huko Abuja Nigeria kati ya tarehe 30 Agosti na 10 Septemba 2019 likiwa na kauli mbiu ya “chukua hata sasa na hapa hapa” pamoja na hilo kati ya tarehe 19 hadi 29 Julai, 2019 imefanyika pia huko mjini Kampala Uganda Jubilei ya dhahabu ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar,  SECAM. Katika jubilei hii Kanisa lilipata fursa ya kutafakali mipango mkakati ya kusaidia maisha ya kifamilia.

Aidha, Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria pia waliweza kutumia fursa hiyo kuwapongeza Maaskofu wanaoadhimisha Jubilei pamoja na Parokia na Majimbo yaliyoadhimisha Jubilei mbalimbali.  Wamewatakia baraka na utume uliotukuka.  Katika kuhitimisha, Baraza la Maaskofu Nigeria limekiri wa kuwa nchi ya Nigeria ina lasrimali nyingi ambazo zinatumika kuwanufaisha wachache. Hivyo wito wa Baraza kwa Serikali ya Nigeria ni kutumia lasrimali za nchi kwa mafao ya wote. Ni pale Serikali inapotoa haki kwa wote katika kushirikishana fursa mbalimbali ndipo amani hutawala na maendeleo ya pamoja hupatikana.  

02 October 2019, 12:42