Tafuta

Vatican News
Shirika la Masista Waabuduo Damu ya Kristo, ASC, linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya uwepo na utume wake nchini Tanzania kuanzia mwaka 1969-2019 Shirika la Masista Waabuduo Damu ya Kristo, ASC, linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya uwepo na utume wake nchini Tanzania kuanzia mwaka 1969-2019 

Masista Waabuduo Damu ya Kristo, ASC : Jubilei ya Miaka 50! Utume!

Shirika la Masista Waabuduo Damu ya Kristo, ASC linaadhimisha Jubilei ya maisha na utume wake nchini Tanzania. Hili ni Shirika la Masista ambao wamejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Damu Azizi ya Kristo Yesu, mto wa rehema, unaowasukuma kushiriki katika kazi ya ukombozi.

Na Shirika la Masista Waabuduo Damu ya Kristo, - Dodoma, Tanzania.

Shirika la Masista Waabuduo Damu ya Kristo, tarehe 21 Septemba 2019 wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya uwepo na utume wao nchini Tanzania. Hiki ni kipindi muafaka cha “kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini.” Hii ndiyo changamoto changamani inayotolewa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake. Masista Waabuduo Damu ya Kristo wanamshukuru Mungu kwa zawadi ya masista wao wa kwanza, waliojisadaka bila ya kujibakiza ili kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Damu Azizi ya Yesu, chemchemi na amana ya wokovu wa mwanadamu. Masista wazalendo, Kanda ya Tanzania wanasema, wanayo ari na moyo mkuu wa kusonga mbele ili kuendeleza utume ulioanzishwa na masista wao sanjari na kuendelea kusoma alama za nyakati ili kusikiliza kwa makini na hatimaye, kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana hali yao ya maisha!

Shirika la Masista Waabuduo Damu ya Kristo, ASC., lilianzishwa kunako tarehe 4 Machi 1834 huko Acuto, Jimbo Katoliki la Anagni na Mtakatifu Maria De Mattias aliyezaliwa tarehe 4 Februari 1805. Katika maisha yake ya ujana aliguswa sana na mahubiri ya Mtakatifu Gaspar de Bufalo kuhusu tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo, chemchemi ya huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Akachomwa moyoni mwake kutaka kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika kazi ya ukombozi. Mtumishi wa Mungu Yohane Merlin alimsindikiza Mtakatifu Maria De Mattias katika maisha na utume wake. Mtakatifu Maria de Mattias aliishi wakati wa Mapinduzi ya Mfalme Napoleone Bonaparte wa Ufaransa. Katika hali na mazingira kama haya, kulikuwepo na umaskini mkubwa wa hali na kipato, bila kusahau kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema. Mtakatifu Maria De Mattias akajisadaka kwa ajili ya kusaidia upyaisho wa maisha ya watu wa Mungu nchini Italia kwa kutoa elimu makini na katekesi kwa wasichana, kama chachu ya ukombozi.

Mtakatifu Maria De Mattias alifariki dunia tarehe 20 Agosti 1866, akiwa na umri wa miaka 61. Kunako tarehe 1 Oktoba 1950 akatangazwa kuwa Mwenyeheri na Papa Pio wa XII. Hatimaye, Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 18 Mei 2003 akamtangaza kuwa Mtakatifu Mtakatifu Maria De Mattias anasema katika Shirika hili misaada itapatikana muda wote na mahali popote. Hii ni ndoto ya Mtakatifu Maria De Mathias, ambayo inaendelea kujidhihirisha kwa kuongezeka kuwa Masista Waabuduo Damu Takatifu, ambao wako tayari kutumwa na Yesu kukusanya mavuno yake ulimwenguni pote. Kuimarishwa kwa Shirika hili nchini Tanzania ni matokeo ya kujituma kwa bidii kwa wapendwa wetu masista wanne waliotoka Kanda za Roma na Acuto waliofika mwaka 1969.  Nao ni Sr. Nicolina Scattaglia Sr Angelina Palmigiani, Sr. Romana Sacchetti na Delfina Gnere. Ujio wao nchini Tanzania ulifuatia mwaliko kutoka kwa Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S., ambao ni Padri Joseph Montenegro, Padri Dino Gioia na Bruda Franco Palombi, ambao waliwasili Tanzania tangu mwaka 1967.

Ombi la kuanzisha utume nchini Tanzania lilitolewa na waliokuwa wakuu wa Kanda za Acuto na Roma ambao ni Sr. Carolina Cataldi ns Sr. Pasqua Matei.  Ombi lao lilipata kibali kutoka kwa aliyekuwa mama mkuu wa Shirika kwa wakati huo, Sr. Catherine Girrens. Mama wakuu wa Kanda ya Acuto na ya Roma waliwatuma Masista wane (4) waliotajwa hapo juu. Masista hawa walifikia Moshi Mkoani Kilimanjaro mnamo tarehe 20/11/1969 na tarehe 22/11/1969 walifika Manyoni baada ya safari ndefu ya meli iliyowachukuwa takribani mwezi mzima kuanzia Bandari ya Brindis nchini Italia.

MUUNDO WA JAMII WAKATI HUO: Wakati huo wenyeji wote waliishi kwa ushirikiano, umoja, urafiki, udugu na amani.  Uhusiano huu wa kiafrika uliokuwepo, uliimarishwa zaidi na mtazamo wa kisiasa wa ujamaa na kujitegemea ambao Tanzania iliufuata mara baada ya kujipatia uhuru mwaka1961. Wakati huu watanzania waliishi katika mfumo wa vijiji vya ujamaa, ingawa wengi wao hawakujua kusoma na kuandika. Ndoa za mitara na mfumo dume ulitawala kiasi cha kuwanyima wanawake sauti.  Huduma za afya zilikuwa ni duni sana kutokana na uhaba wa miundo mbinu ya huduma ya afya. Miundo mbinu ya usafiri pia ilikuwa duni. Kiwango cha elimu kilichotolewa pia kilikuwa ni duni sana kutokana na uhaba wa shule za msingi, sekondari, vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu.

HALI YA JAMII KIUCHUMI, KISIASA NA KIIMANI: Kwa ujumla hali ya kiuchumi ilikuwa duni kufuatia teknolojia duni ya uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma. Mfano zana duni za kilimo ambacho kimsingi ni uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa.  Biashara ilitegemea zaidi ubadilishanaji wa vitu kwa vitu. Kulikuwa na viwanda vidogo vidogo ambavyo uzalishaji wake ulitegemea mikono.  Miundo mbinu ilikuwa duni, hivyo familia nyingi hazikuwa na uchumi bora. Imani ya kikatoliki ilikuwa imeanzishwa tayari na Mapadri wa Shirika la Mateso ya Yesu “Passionists” Jimboni Dodoma na maeneo ya Kusini mwa Singida hasa Wilaya ya Manyoni.  Mwaka 1967 Wamissionari wa Damu Azizi walikuja kuimarisha imani maeneo ya Manyoni baadaye, Masista wa ASC walikuja kuongeza jitihada za uinjilishaji Manyoni, ikizingatiwa kwamba, kiwango cha imani kilikuwa bado kiko chini sana. Hii ilitokana na ukubwa wa eneno pamoja na uhaba wa mihimili ya uinjilishaji. Kiuchumi Kanisa lilikuwa maskini kutokana na umaskini wa watu wake. Kwa kiasi kikubwa uchumi wa Kanisa ulitegemea zaidi michango ya wahisani kutoka nje ya Tanzania.  Pamoja na hayo Masista waliwahimiza waamini kufanya kazi kwa bidii ili waweze kujitegemea wenyewe. Wakati huo kulikuwepo na Wakristo, waamini wa dini ya Kiislam pamoja na dini asilia, walioshirikiana kwa mambo msingi katika maisha kwa amani na utulivu, huku wakiheshimiana na kuthaminiana.

MTAGUSO MKUU WA PILI WA VATICAN: Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulihimiza utimilifu wa upendo, kwa kukazia zaidi maisha ya kijumuiya. Masista kwa mara ya kwanza waliishi maisha ya kijumuiya Parokiani Manyoni na baadaye walifungua Jumuiya nyingine. Waliishi kwa kusaidia katika umoja na udugu kadiri ya mahitaji yao msingi.  Huu ulikuwa ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa jirani zao. Mtindo huu wa maisha ukachochea maisha ya umoja, udugu na upendo katika huduma, kiasi cha kuacha chapa ya kudumu katika maisha ya wale waliokuwa wanawahudumia. Waabuduo walijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania. Wakawa ni chachu ya uekumene wa huduma kwa maskini na vitalu vya kukuza miito mitakatifu. Waabuduo tangu walipoingia nchini Tanzania wakajifunga kibwebwe kupambana na changamoto zilizokuwa mbele yao kwa wakati huo yaani: Baa la ujinga, magonjwa na njaa. Hapa wakaamua kujikita zaidi katika uinjilishaji wa kina uliogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili!

UJINGA: Kulikuwa na ujinga wa kiwango cha juu sana. Watu wachache sana walijua kusoma na kuandika, kulikuwa na shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu vichache kwa wakati huo nchini Tanzania. Rais Julius Kambarage Nyerere akatamka wazi kwamba, maadui wakuu wa Tanzania ni: Ujinga, umaskini na maradhi. Masista wakaunga mkono jitihada hizi kwa kuanzisha elimu ya ufundi kwa wanawake na wasichana Wilayani Manyoni kwa kutambua kwamba, kumwelimisha mwanamke ni sawa na kuelimisha jamii nzima! Kulikuwa na upungufu mkubwa wa wahudumu wa Kanisa, jambo lililopelekea wamisionari kuwekeza kwanza kwa makatekista vigangoni, ili kusaidia kuwaelimisha watu waliokuwa wanaongokea Ukristo.

MAGONJWA: Masista walijifunga kibwebwe kupambana na magonjwa ya Ukanda wa Joto kwa ujasiri, ari na moyo mkuu. Hii ilikuwa ni changamoto kubwa kwani kulikuwa na uhaba mkubwa wa hospitali, dawa na vifaa tiba. Masista wakajitahidi kuhakikisha kwamba, wanapata dawa kutoka ndani na nje ya Tanzania, ili kuwahudumia watu wa Mungu nchini Tanzania. Wakati mwingine, dawa na vifaa tiba havikuweza kuwafikia walengwa kutokana na ubadhilifu wa mali ya umma, ubinafsi na uchoyo. Kulikuwa na uhaba mkubwa wa miundo mbinu ya majengo. Mwishoni, Masista wakafanikiwa kujenga Zahanati ya kulaza wagonjwa pamoja na kutoa tiba mbali mbali. Masista walitembelea vijiji vyote vya Wilaya ya Manyoni ili kutoa huduma, ingawa miundo mbinu ya barabara pamoja na mawasiliano ilikuwa ni hafifu sana. Imani potofu, mila na desturi zilizopitwa na wakati ni kati ya changamoto ambazo Masista walipambana nazo kwa kipindi cha muda mrefu katika maisha na utume wao katika huduma ya afya. Walitoa sehemu ya nyumba yao ya kuishi ili iweze kutumika kama Zahanati kwa ajili ya wagonjwa. Hiki ni kielelezo cha hali ya juu cha imani inayomwilishwa katika upendo!

BAA LA NJAA: Baa la njaa na utapiamlo wa kutisha ni kati ya changamoto kubwa zilizovaliwa njuga na Masista Waabuduo katika maisha na utume wao, ikizingatiwa kwamba, Manyoni ilikuwa ni kati ya maeneo yaliyokuwa yanakumbwa na ukame kwa kipindi kirefu na hivyo kusababisha baa la njaa, hali iliyosababisha majanga makubwa kwa watu na mifugo yao. Changamoto hii, ilishughulikiwa kwa kujikita katika karama ya Shirika inayoongozwa na upendo na huruma ambayo ni fadhila kubwa kuliko nyingine zote. Masista walikuwa mstari wa mbele kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa njia ya elimu makini, sera na mikakati ya maendeleo fungamani ya binadamu. Wakasimamia utu, heshima, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu.

Wanawake na wasichana walifundishwa maarifa ya nyumbani, ili kuboresha hali ya maisha katika familia na hivyo kuongeza pia muda wa kuishi. Waliwasaidia wasichana walioolewa katika umri mdogo ili kuweza kukabiliana na changamoto za maisha. Chuo cha Maarifa ya Nyumbani cha “Amani Home Craft” kilichofunguliwa kunako mwaka 1976 ulikuwa ni ukombozi mkubwa kwa wanawake na wasichana wa Manyoni. Masista kwa kusoma alama za nyakati, Kituo cha Maarifa ya Nyumbani cha Amani, kunako mwaka 2002 kikageuzwa kuwa ni Shule ya Sekondari ya Wasichana Manyoni. Masista walijitahidi kutafuta chakula na kuwagawia wazee na maskini Wilayani manyoni kwa kushirikiana kwa karibu sana na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu.

Ili kusogeza huduma ya maisha ya kiroho na kiutu kwa familia ya Mungu Wilayani Manyoni, Mkoani Singida, Waabuduo waliamua kufungua Jumuiya Parokia ya Chibumagwa na hapo wakasaidia huduma za katekesi na elimu ya awali kwa watoto wadogo. Kunako mwaka 1980 Masista Waabuduo Damu ya Kristo, walianza kupokea wasichana waliotamani kuendeleza karama ya Shirika kwa kuitamadunisha nchini Tanzania, kwa kumfuasa Kristo kwa ukaribu zaidi katika maisha ya kitawa pamoja na kuwahudumia jirani kwa upendo bila ya kujibakiza! Sr. Genesia Nave, akapewa jukumu la malezi kwa wasichana wazalendo walioanza kujiunga na Shirika. Tarehe 15 Agosti 1990, Sr. Anna John, Sr. Anastazia Floriani na Scholastica George waliweka nadhiri zao za kwanza. Shirika linapoadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya uwepo na utume wake nchini Tanzania lina watawa wazalendo 87.

HUDUMA KWA WAHITAJI: Masista walijitahidi kuwahudumia wasiojiweza kwa kuwapatia mahitaji msingi hapo Manyoni na maeneo ya jirani.  Wengine waliwajengea nyumba, wakati wa vita vya Uganda na Tanzania waliwasaidia waathirika wa vita kwa namna mbalimbali. Jumuiya mama ya Manyoni iliyofunguliwa tangu 1967 iliimarika na kuzaa jumuiya zingine ili kukidhi mahitaji. JUMUIYA YA CHIBUMAGWA: Ilianzishwa mnamo mwaka 1981 ambapo Sr. Delfina Gnere na Sr. Tullia Mandato walikuwa wanatoa huduma ya afya, mafundisho ya dini huduma parokiani, elimu kwa akina mama na watoto na huduma nyingine za kijamii. Baadaye masista wengine waliendelea kujiunga nao kama vile Sr. Santina, Maria Fiorilo na Sr. Carmina.  Masista walifanya haya yote kwa moyo wa majitoleo makubwa.  Upendo wa Kristo uliwasukuma kujitolea maisha yao kwa ajili ya mpendwa jirani. JUMUIYA YA DODOMA ilianzishwa mnamo mwaka 1991 eneo la Miyuji chini ya usimamizi wa Sr. Marisa Nardoni pamoja na wanovisi (5) na baadaye masista wengine waliendelea kuja.  Jumuiya hii ilikuwa mahususi kwa ajili ya malezi na kazi nyingine za kiutawala. Pia masista walitoa elimu ya dini kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

JUMUIYA YA DAR ES SALAAM: Hii ilianzishwa mwaka 1994 chini ya uongozi wa Sr. Theresa Sorrentino, Scholastica George na Sr. Angelina Palmigiani.  Hawa walitoa huduma kwa watoto na maparokiani, kufundisha dini, katekesi kwa watu wazima. mashuleni na kutembelea familia. JUMUIYA YA HEKA: Ilianzishwa mwaka 1995 na masista wafuatao: Sr. Delfina Gnere, Sr. Carmelina Gallo, Sr. Maria Rosaria Gargiulo, Sr. Oliver Clemence, Flaviana Alfred na Sr. Josephina Elias. Utume wao ulikuwa kutoa huduma parokiani, kutoa huduma ya afya na kufundisha dini mashulen i.JUMUIYA YA KIJIJI CHA MATUMAINI: Ilianzishwa mnamo 2002 chini ya usimamizi wa Sr. Maria Rosaria Gargiulo, Sr. Annastazia Floriani na Sr. Melania Joseph.  Hawa walifanya utume wa kulea watoto yatima na waathirika wa virusi vya ugonjwa wa Ukimwi.  Pia walikuwa wanatoa elimu kwa watoto wa Kijiji cha Matumaini kwenye shule za awali, msingi na sekondari. Lengo ni kuwapa watoto hawa mahitaji msingi mpaka wanapofikia umri wa kujitegemea wenyewe. Wanapewa huduma ya afya, mafundisho ya dini, huduma ya ushauri nasaha na huduma zingine. 

JUMUIYA YA ITIGI: Ilianzishwa 2006 na Sr. Maria Theresa Fiorillo na Radegunda Hilary.  Masista wengine walifika baadaye.  Hapo mwanzoni jumuiya hii ilikuwa chini ya jumuiya ya Manyoni kwa sababu haikukidhi kiwango cha kuitwa au kupewa hadhi ya jumuiya kulingana na katiba ambayo ni lazima jumuiya iwe na idadi ya masista 3.  Baadae jumuiya ilijitegemea, masista walipoongezeka.  Walitoa huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mt. Gaspari Itigi pamoja na kuendesha Moteli. JUMUIYA YA MAFUYANE – MSUMBIJI: Hii ilianzishwa 2006 na Sr. Scholastica George Nyongo, Yohana Amu na Sophia Michael ambao utume wao ni kufundisha katekesi kwa watoto, vijana na watu wazima. Walianza kutoa huduma katika kituo cha wazee, elimu ya awali na kuendelea kujikita katika utume kwa vijana; huduma ya afya na kutoa huduma Kanisani kutokana na uhaba wa mapadri. JUMUIYA YA WANOVISI MIYUJI, DODOMA: Ilianzishwa tarehe 7/08/2007 na Sr. Anna John kama mlezi wa wanovisi nane. Wanovisi hawa walijifunza kwa nadharia na vitendo upendo wa Mungu na mpendwa jirani.

JUMUIYA YA MOROGORO: Ilifunguliwa 2008 na Sista Martha Joseph, Magreth Silvery, Maria Goreth Joseph.  Utume wao ulikuwa ni kuhudumia wasichana maskini, kuwapa mahali pa kuishi wakiwa masomoni. Huduma nyingine ni kutoa elimu ya dini kwa watoto na watu wengine kwa makundi yote parokiani na kutembelea wagonjwa. JUMUIYA YA VIKAWE: Ilifunguliwa 2014 na masista Anastazia, Sr. Stella Joseph na wengine walijiunga baadae.  Jumuiya hutoa huduma ya afya, elimu kwa watoto, mafundisho ya dini kwa watoto na watu wazima, pamoja na kuelimisha wasichana na akina m ama.JUMUIYA YA CESENA: Mnamo tarehe 30/04/2015, Masista Waabuduo Damu ya Kristo, “Region ya Tanzania” walionesha moyo wa upendo na utayari wao wa kufungua jumuiya mpya   nchini Italia, katika Parokia ya MT. EGIDIO ABATE, Jimbo la  CESENA lililoko nchini Italia. Masista wanatoa huduma Parokiani, kufundisha dini kwa watoto, kazi za kichungaji kwa vijana, kutembelea wagonjwa na kutoa huduma katika kituo cha Caritas cha Jimbo.

MATUKIO MUHIMU: Jubilee miaka 25 – Uwepo wa ASC Tanzania: Mwaka 1994 ulikuwa muhimu sana kwa ASC, uwepo wao hapa Tanzania ulitimiza miaka 25. Huo ulikuwa ni mwaka wa kumshukuru Mungu na kufanya tathimini ya miaka iliyopita, kuishi vizuri na kuweka mikakati ya baadae.  Ndani ya miaka 25 masista walikuwa wachache ila walifanya mambo mengi kwa nguvu ya Damu ya Kristo na maisha ya kitume ya kujituma ya kila siku.  Kwa ujumla masista hawa wa mwanzo na wale waliokuja baadaye wamejitahidi sana kuleta maendeleo fungamani ya binadamukwa familia ya Mungu ndani na nje ya Tanzania. Wamekuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huruma, upendo na uhai. Wamesaidia katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaopania kumkomboa mtu mzima: kiroho na kimwili na hatimaye, kuwapatia watu wa Mungu uhuru wa kweli!

Jubilee hii iliambatanishwa na matukio ya ufunguzi wa Kituo cha Afya cha Mtakatifu Maria De Mattias cha Manyoni pamoja na Zahanati ya Kinangali kituo cha afya cha Mt. Maria De Mattias kilifunguliwa ili angalau kukidhi mahitaji ya afya Manyoni na vitongoji vyake.  Kujengwa kwa kituo hiki ni kutokana na udogo wa chumba cha kutolea huduma ya afya kilichokuwa ndani ya makazi ya masista kutokidhi mahitaji.  Kwa hiyo kituo hiki ni matunda ya Jubilee ambapo masista walitaka kuendelea kutoa huduma kwa maskini hasa wagonjwa na wazee, ili kudumisha utu na heshima yao; watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

UTOAJI HUDUMA YA AFYA KATIKA ZAHANATI YA KINANGALI: Masista walipowasili Chibumagwa walianza kuhubiri injili kwa watu wakishirikiana na mapadri wa Damu Takatifu, pamoja na hivyo waliendelea kutoa elimu ya dini hasa walipofungua kigango na zahanati ya kinangali. Pia masista waliomba kufungua kituo cha afya na kukubaliwa mwaka 1982 chini ya usimamizi wa Sr. Santina.  Kwa mara ya kwanza huduma ya afya ilitolewa mara moja kwa wiki na baadae mara tatu kwa wiki. Huduma hizi zilitolewa chini ya miti, kwenye nyumba za watu na kwenye vibanda vya muda. Kufuatia kutoa huduma ya afya katika mazingira haya magumu ilibidi masista kwa kushirikiana na wafadhili wajenge zahanati kinangali. Maombi ya msaada kwa wafadhili walihusika Masista Teresa Sorrentina na Sr. Santina Hospitali ya Kinangali ilifunguliwa rasmi 13/08/1994 ambapo ilikuwa mkombozi kwa akina mama, watoto na watu wengine.  Akina mama na watoto walipatiwa chanjo ya maradhi mbalimbali hapo.

KUKUA KWA ASC KAMA MISSION NA FOUNDATION: KAMA FOUNDATION: Tanzania ilikuwa “Foundation” rasmi mwaka 1994 masista wafuatao walitumikia katika nafasi ya uongozi kwa kipindi tofauti tofauti kama ifuatavyo:-

(a)  Sr. Marisa Nardoni 1994 – 1997

(b) Sr. Teresa Sorrentina 1997 – 2000

(c)  Sr. Marisa Nardoni 2000 – 2003

(d) Sr. Lucina John     2003 – 2006

(e)  Sr. Josephina Paul          2006 – 2009

(f)   Sr. Euphrasia Julius 2009 – 2011

Kwa kipindi cha miaka 13 Tanzania imekuwa foundation chini ya Provinsi ya Acuto kabla ya Provinsi nne kuungana pamoja na kuwa Region ya Italia.  Na miaka minne chini ya uongozi wa Region ya Italia.  Kwa hiyo ASC Tanzania imekuwa foundation kwa miaka isiyopungua 17.

ASC REGION YA TANZANIA KWA MAJARIBIO

Mbegu za karama yetu zilizoletwa na masista wamisionari kutoka Italia zilizaa matunda Miongoni mwa watu kupitia uwepo wa masista 69 wazalendo.  Ndio maana tuliomba Tanzania iwe Region. Tulifikia uamuzi huu baada ya kukidhi vigezo vya katiba na muundo wake kama: Idadi ya kutosha ya masista wazalendo ili kuendeleza karama. Pili ni kutoa kwa ukarimu na kujitegemea kiuchumi. Kujitegemea kiuongozi kwa kuwa na muundo thabiti wa uongozi Kikanda!  Kwa hiyo baada ya uchunguzi wa mama mkuu wa shirika Sr. Bernada Cristic na washauri wake, Tanzania tulithibitishwa kuwa Kanda kwa majaribio kwa kipindi cha miaka 3 mnamo tarehe 4/3/2011. ASC Tanzania wanamshukuru Mungu kwa ulinzi wake kupitia hatua mbalimbali za shirika na uwepo wa zawadi ya ASC katika Kanisa Takatifu. tunajiweka katika ulinzi wa Roho Mtakatifu na nguvu ya Damu Takatifu ya Kristo ili tuweze kueneza karama yetu sasa na katika kizazi kijacho.  Mtakatifu Maria De Mattias atuongoze ili tuendeleze zawadi ya karama aliyojaliwa na Roho Mtakatifu katika Kanisa.

ASC 50 Yrs
19 September 2019, 16:37