Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili XXV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Upendo kwa ajili ya maskini: Mungu huwabariki wanaowajali na kuwasaidia maskini. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili XXV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Upendo kwa ajili ya maskini: Mungu huwabariki wanaowajali na kuwasaidia maskini. 

Tafakari Jumapili 25 ya Mwaka C: Mwenyezi Mungu na mali ya dunia

Mama Kanisa anafundisha kwamba, watu wanaokandamizwa na umaskini ni watu wanaostahili mapendo ya upendeleo kwa upande wa Kanisa, ambalo tangu mwanzo wake na licha ya mapungufu na udhaifu wa watoto wake, halikuacha kufanya kazi kwa ajili ya faraja yao, utetezi na ukombozi, kwa njia ya kazi nyingi za mapendo zinazobaki kuwa ni za lazima daima na popote. Mungu na Mali!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 25 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Leo Kristo anatufundisha kutumia vizuri: rasilimali fedha, vitu, muda, karama na kila tulichonacho hapa duniani ili vituasaidie kupata maisha na uzima wa milele. Mama Kanisa anafundisha kwamba, watu wanaokandamizwa na umaskini ni watu wanaostahili mapendo ya upendeleo kwa upande wa Kanisa, ambalo tangu mwanzo wake na licha ya mapungufu na udhaifu wa watoto wake, halikuacha kufanya kazi kwa ajili ya faraja yao, utetezi na ukombozi, kwa njia ya kazi nyingi za mapendo zinazobaki kuwa ni za lazima daima na popote. Somo kwanza kutoka kitabu cha Nabii Amosi linasimulia mahusiano kati ya matajiri na maskini yalivyokuwa wakati wa Nabii Amosi. Kipindi hiki matajiri waliwanyonya maskini na fukara hata wakithubutu kuwauza walioshindwa kulipa madeni yao kwa thamani ya viatu.

Nabii Amosi anawaonya matajiri na anatabiri adhabu yao akisema lisikieni hili, ninyi mnaopenda kuwameza wahitaji, na kuwakomesha maskini wa nchi, mkiipunguza efa na kuiongeza shekeli, mkidanganya watu kwa mizani ya udanganyifu, mpate kuwanunua maskini kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya viatu; na kuziuza takataka za ngano. Bwana ameapa kwa fahari ya Yakobo, Hakika sitazisahau kamwe kazi zao hata mojawapo. Amo 8:4-6. “Laana ya Bwana i katika nyumba ya waovu, Bali huibariki maskani ya mwenye haki,” Mit 3:33. Mtume Paulo katika somo la pili la waraka wake wa kwanza wa kwa Timotheo anatunahimizwa kusali kwa ajili ya watu wote kwani Mungu anataka watu wote waokoke. Kwa sala Mungu anatujalia ukombozi ambao umeletwa na Kristo, aliyempatanishi wa watu na Mungu. Ndiyo maana anasema kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu. Paulo anasisitiza nafasi ya Baba kama kiongozi akisema, nataka wanaume wasalishe kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano.

Katika Injili ilivyoandikwa na Luka Yesu anatuhimiza kuiga bidii ya karani dhalimu lakini mwerevu tupate kuingia katika ufalme wa Mungu. Pia anatuonya kutumia fedha kwa namna inayofaa ili tupate uzima wa milele. Kama ilivyokuwa kwa matajiri wa nyakati za nabii Amosi ndivyo ilivyokuwa kwa matajiri na mafisadi wa nyakati za Yesu hata nyakati zetu. Katika simulizi hili kuna mafisadi wa aina tatu. Fisadi wa kwanza ni karani dhalimu aliyetumia vibaya mali ya Bwana wake hata akabadilisha hati za mikopo na kupunguza kiasi walichodaiwa wakopaji ili wamkaribishe baada ya kuachishwa kazi kwani kulima, hawezi na kuomba, anaona haya. Wakopaji nao walikuwa mafisadi kwani walikubali kubadilisha kiasi walichodaiwa na kuandika kiasi kidogo baada ya kushauriwa hivyo na wakili dhalimu. Bwana wao naye alikuwa fisadi kwani alimsifu huyo karani dhalimu. Katika simulizi hili, Yesu anashauri kuiga mfano wa karani dhalimu. Maana yake nini? Je tuwe nasi wadhalimu?

Jibu ni hapana. Maana yake tutumie hekima na busara alizotujalia Mungu kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Katika maisha yetu kma mbinu na muda tunaotumia kutafuta pesa tungezitumia pia katika kutafuta utakatifu, kama mbinu na muda tunaoutumia katika kutunza nyumba ndogo na michepuko ungetumika katika kulinda ndoa na miito mitakatifu, kama muda na umakini tunaotumia katika starehe mfano kuangalia mpira ungetumika pia katika sala na kusikiliza neno la Mungu, kama watu wanavyoshirikiana katika kupanga uovu na kufichiana siri za ufisadi na udhalimu, wangeshirikiana hivyo hivyo katika kulihudumia Kanisa na mambo ya mbinguni hakika hakuna ambaye angeikosa mbingu. Tunafundishwa kwamba vile tulivyonavyo vitusaidie kufanya urafiki na watu na Mungu. Inawezekana hatuna mali au vitu vingi lakini hata kidogo tulichonacho kitusaidie kujenga urafiki na Mungu pamoja na watu kwa uaminifu. Ujumbe wa ukiwa mwaminifu katika madogo utapewa makubwa ni wa maana na muhimu sana, maana huwezi kupandishwa cheo kama hujafanya vizuri katika nafasi ndogo uliyopo. Katika kila tufanyalo lengo liwe ni kumtumikia Mungu. 

Tutambue kuwa lolote lile lililo ovu halina umilele ndani yake. Fumbo la umwilisho, Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu Yesu Krito, sadaka aliyoitolea Msalabani, na ufufuko wake, ndicho kikomo cha uovu wote. Hii ndiyo njia aliyoichangua Mungu kuushinda uovu. Na tunaushinda uovu tukiwa ndani na katika Kristo Yesu. Kristo ndiye mizani yetu katika kweli, upendo, haki, na amani. Msukumo wa kutaka zaidi kila kitu una misingi yake katika udanganyifu wa kuwa nikiwa na vingi nitakuwa na furaha zaidi, nitakuwa wa muhimu, na nitakuwa salama; lakini mawazo hayo yote si ya kweli bali ni ubatili mtupu kwani Paulo anasema, “Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu,” 1Tim 6:9. Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu,” 1Tim 6:7. Mt. Augustino anatuwasa akisema, "kuna furaha kubwa kuwa na vichache kuliko kuwa na vingi kwani mali huleta furaha ya muda mfupi tu. Basi wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole, ili katika hayo upate wokovu wa milele 1Tim 6:11. Tumsifu Yesu Kristo.

J25 Mwaka C
18 September 2019, 16:04