Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 19 ya Mwaka C wa Kanisa ni mwaliko wa kuyaangalia matukio mbali mbali ya maisha katika mwanga wa imani! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 19 ya Mwaka C wa Kanisa ni mwaliko wa kuyaangalia matukio mbali mbali ya maisha katika mwanga wa imani! 

Tafakari Jumapili ya 19 ya Mwaka C: Mwanga wa Imani & Matumaini

Katika Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, Mungu amefunua katika ukamilifu wake upendo unaookoa na kutualika sisi kwa uongofu wa maisha kwa njia ya maondoleo ya dhambi – Mdo. 5:31. Kwa Mtakatifu Paulo, upendo huu unatupeleka kwenye maisha na utu mpya kabisa, kwa kuuvua utu wa kale na kuanza kutembea katika mwanga wa imani kwa Kristo Yesu!

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.

Mtakatifu Augustino wa Hippo anasema ‘imani hufungua mlango wa ufahamu na kukosa imani huufunga’Ndugu zangu, somo la kwanza latoka kitabu cha Hekima ya Solomoni, katika sehemu ya tatu ya kitabu hiki. Hapa kazi ya Mungu inatukuzwa katika historia ya taifa teule, ikiangalia hasa uhuru wao toka utumwani Misri. Dhumuni na lengo la kitabu hiki ni kuwatahadharisha Wayahudi wenye elimu ya Mungu na hatari ya elimu dunia. Angalisho hili limetokea baada ya kujichanganya na watu na vitu vilivyo mbali na Mungu. Mwandishi anaandika ili kuwakinga na upotevu. Hekima ya kweli ni Mungu, kupitia njia ya sala. Hakuna hekima mbadala. Kwa ufupi, katika kitabu hiki tunapata habari juu ya sadaka ya Pasaka, juu ya habari ya kutoka utumwani – Kut. 12 – kama sadaka ya kwanza ya ukombozi wa mwanadamu. Ni sikukuu ya kukumbuka fadhila ya ukombozi.

Somo la pili linatoa fundisho kwa ajili ya wakristo wapya ili kuwatahadharisha juu ya imani yao mpya, mfano kutambua wazi tofauti kati ya sadaka ya wanyama na sadaka ya Kristo, tofauti kati ya ukuhani wa Kristo anayeondoa dhambi za watu n.k na viongozi wa kawaida katika taifa la Israeli. Somo la Injili latoka injili ya Luka na kwa ujumla injili yaongea juu ya wakristo wasio Wayahudi na tunaona habari juu ya huruma ya Yesu – aliwahurumia wakosefu – Lk. 15:1-2, anasamehe dhambi - Lk 15:11-32, mpole 1:51-53. Ni Injili iliyojaa shukrani kwa Mungu kwa mambo yote aliyofanya kwa ajili ya kuwakomboa watu na yaonesha furaha kubwa ya kiroho juu ya matendo ya wokovu - Lk. 2:14, 5:26. Katika somo hili tunasikia uzuri wa Neno la Mungu unaojengwa kwenye matumaini na mwanzo wa somo tunasikia msiogope enyi kundi dogo.

Halafu tena, Yesu anaongea juu ya hatari ya mali na haja ya uaminifu na mwaliko wa kujiweka tayari kwa wa ujio wa Bwana. Mwito wa Kikristo uko wazi hapa – tunao ufalme wa Mungu, msiogope. Kwa kifupi, ufahamu unatuwajibisha. Angalia masomo yetu yote ya leo na ujumbe uliopo unajirudia. Na ndiyo sababu baada ya kutufundisha, atukumbusha kuwa tayari na viuno viwe vimefungwa. Amani ya ufalme na uwajibikaji ni sifa zinazowekwa bayana na Yesu. Ndiyo maana Yesu anasema msiogope. Wito wa Yesu ni kutoa jibu na kuwajibika. Uelewa huo kama ulivyo katika somo la kwanza watafsiri maana ya sadaka ya ukombozi. Hivyo katika somo la pili tunaona jibu hilo, jibu la imani/mababu zetu katika Agano la Kale – angalia imani ya Abrahamu na Sara – aliamini na kuwa tayari kuondoka alipokuwa tayari kutoa sadaka ya mtoto wake wa pekee. Hata Mt. Paulo, Mtume na mwalimu wa mataifa anashangaa imani ya namna hiyo – Rom. 4:18. Sasa uelewa wa maisha ya imani utusaidie kuelewa kwanini Yesu asema msiwe na woga.

Tulipoadhimisha mwaka wa imani tulichagizwa na mwaliko wa uongofu wa kweli, uliofanywa upya na Bwana, Mwokozi pekee wa ulimwengu. Katika Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, Mungu amefunua katika ukamilifu wake upendo unaookoa na kutualika sisi kwa uongofu wa maisha kwa njia ya maondoleo ya dhambi – Mdo. 5:31. Kwa Mtakatifu Paulo, upendo huu unatupeleka kwenye maisha mapya ‘basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima – Rum. 6:4’. Kwa njia ya imani maisha haya mapya yanaunda uhai wote wa mwanadamu kadiri ya uhalisia mpya usiotetereka wa ufufuko. Kwa kadiri ile ambayo, kwa uradhi wote mtu anashiriki fumbo hili, mawazo ya mwanadamu na shauku zake, mtazamo na tabia zake zinaanza kutakaswa na kubadilisha taratibu katika safari ambayo kamwe haikamiliki katika maisha haya. Imani itendayo kazi kwa upendo – Gal. 5:6 inakuwa ni kigezo kipya cha uelewa na utendaji unaoyabadilisha maisha yote ya mwanadamu – Kol. 3: 9-10, Efe. 4:20, 2Kor. 5:17

Mlango wa Imani, Mdo. 14:27 – daima umefunguliwa kwa ajili yetu na kutuongoza katika muungano na Mungu na kutuingiza ndani ya kanisa lake. Inawezekana kuvuka kuzingiti hicho pale neno la Mungu linapotangazwa na moyo unapojiruhusu kuundwa kwa kugeuzwa na neema. Kupitia katika mlango huo ni kuanza safari itakayodumu kwa maisha yote. Safari hii inaanza na ubatizo – Rum. 6:4; ambao kwao tunaweza kumwita Mungu Baba, na inaisha kwa njia ya kifo kuelekea uzima wa milele, ulio tunda la ufufuko wa Bwana Yesu, ambaye shabaha yake ilikuwa kuwavuta wale wanaomwamini katika utukufu wake kwa njia ya Roho Mtakatifu – Yn. 17:22. Kukiri imani katika Utatu Mtakatifu – Baba, Mwana na Roho Mtakatifu ni kuamini katika Mungu mmoja ambaye ni upendo - 1Yn. 4:8. Baba ambaye katika utimilifu wa wakati alimtuma Mwanaye kwa ajili ya wokovu wetu, Yesu Kristo, ambaye kwa fumbo la kifo chake na ufufuko aliukomboa ulimwengu, Roho Mtakatifu ambaye analiongoza Kanisa katika karne zote tunaposubiri ujio mtukufu wa Bwana.

Hakika leo tunaalikwa kuitambua hekima hii ya Mungu, kutumia muda wetu kutambua imani hiyo vizuri na matendo ya imani na namna ya kuwekeza hazina yetu. Tukifanya hivyo tutaenzi neno la Mungu jumapili hii ya leo. Na hekima ya Mungu ni kumtambua yeye na mpango wake wa ukombozi kama ulivyotufikia kwa njia ya Mwanawe. Tumsifu Yesu Kristo

06 August 2019, 16:37