Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu: Jumapili 19 ya Mwaka C wa Kanisa: Wazo kuu: Tendeni haki na kutoa sadaka! Tafakari ya Neno la Mungu: Jumapili 19 ya Mwaka C wa Kanisa: Wazo kuu: Tendeni haki na kutoa sadaka! 

Tafakari Jumapili 19 ya Mwaka: Tendeni haki na kutoa sadaka!

Hazina yetu inategemea tu kwa kutenda haki na ndio kuwajali wengine, kutumia mema au utajiri wa aina yeyote sio kwa ajili yetu tu bali kwa ajili ya kuwahudumia wengine. Na ndio wazo kuu katika Dominika ya leo. Tunaalikwa kuwa watumishi waaminifu na sio mabwana wakuu au wamiliki wa mema yanayowekwa mbele yetu na Mungu mwenyewe. Ni Dominika ya kuwa watumishi waamifu!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Msiogope nyie mlio kundi dogo kwani mmekabidhiwa Ufalme wa Mungu: Ni katika muktadha wa Kanisa la mwanzo lililokuwa linapitia mateso na madhulumu ya kila aina, hivyo walianza kukata tamaa na kuogopa kwa jinsi walivyokuwa wachache na mbaya zaidi wanachukiwa na ulimwengu: Mwinjili Luka anawaandikia sehemu ya Injili ya leo kuwaimarisha kuwa wasiogope hawa walio kundi dogo. Ni maneno ya faraja na tumaini si kwa Kanisa la mwanzo bali hata katika nyakati zetu tunaposafiri kama jumuiya ya waamini kwani daima tunaona bado yule mwovu na nguvu zake zikilishambulia na kulitesa Kanisa. Kanisa daima linahakikishiwa ufalme wa Mungu maana sio kazi ya mwanadamu bali ni ya Mungu mwenyewe, na hivyo hatuna budi kusonga maana ni Mungu anayeujenga ufalme wake ulimwenguni kwa kututumia sisi wanadamu dhaifu na wadhambi. Dominika iliyopita tulisikia juu ya mkulima tajiri mpumbavu kwani hakuweka akiba yake mbinguni kwa kujali wengine na hivyo Mungu akamchukua na akaacha mali zake zote ulimwenguni.

Jumapili iliyopita tulitafakari na kuona ujumbe kusudiwa kuwa katika maisha yetu mali tulizo nazo sio zetu bali sisi tunawekwa kuwa waangalizi tu wa mali hizo na hivyo hatuna budi kuzitumia kadiri ya maelekezo ya mwenye mali yaani Mungu mwenyewe. Wazo hilo linaendelezwa tena katika Injili ya leo. Injili ya leo inatualika nini tufanye ili tusifanye makosa kama ya yule mkulima tajiri mpumbavu. Sadaka ni kutenda haki, kuwapa wengine mastahili yao: Uzeni mlivyonavyo na mkatoe sadaka. Neno la kiebrania Tsadakha, halikuwa na maana ya kutoa sadaka kwa wenye dhiki na shida bali lilikuwa na maana ya kutenda haki. Kumpa mwingine mastahili yake, ndio kusema kila kitu ninachokuwa nacho mimi kwa ziada basi hicho ni haki ya yule asiyekuwa nacho. Ni sawa na wazo tuliloliona Dominika iliyopita kuwa sisi ni waangalizi tu wa kila mema tunayokuwa nayo bali mmiliki na mwenye mali ni Mungu mwenyewe hivyo hatuna budi kutenda haki ndio tsadakha.

Hazina yetu inategemea tu kwa kutenda haki na ndio kuwajali wengine, kutumia mema au utajiri wa aina yeyote sio kwa ajili yetu tu bali kwa ajili ya kuwahudumia wengine. Na ndio wazo kuu katika Dominika ya leo tunaalikwa kuwa watumishi waaminifu na sio mabwana wakuu au wamiliki wa mema yanayowekwa mbele yetu na Mungu mwenyewe. Ni Dominika ya kuwa watumishi waamifu! Viuno vyetu viwe vimefungwa na taa zetu ziwe zinawaka ndio mwaliko wa kuwa daima watumishi: Kanisa kama Jumuiya ya waamini ni nyumba ya Kristo Mwenyewe aliyetuachia utumishi hivyo kila mmoja wetu anapaswa kutumikia kiaminifu. Yesu anatumia ishara mbili viuno vyetu viwe vimefungwa na taa zetu ziwe zinawaka. Lugha hii ilieweka kwa watu wa tamaduni za Kiyahudi kwani kwa desturi mwenye nyumba alivaa kanzu ndefu na watumishi walipaswa kuvaa fupi au kujifunga viuno ili waweze kutumikia vema. Walijifunga viuno vyao walipokuwa safarini au walipopaswa kufanyakazi fulani.

Hivyo kila mara mtumishi alikuwa amejifunga kiuno tayari kutumika na kuacha taa ikiwaka ndio kusema kuwa tayari muda wote kufanya utumishi. Yesu anatuliaka leo kuwa na viuno vilivyofungwa na taa zinazowaka, yaani kuwa tayari kutumikia daima katika maisha yetu bila kujali saa wala nafasi au fursa au hali tunayokuwa nayo. Mfuasi wa Kristo hana saa wala majira bali daima yupo tayari bila kujibakiza katika kutumikia kwa upendo kila anayekuwa muhitaji. Anakuja kama mwivi sio kutuangamiza bali kutukomboa: Mfano wa pili unatushangaza kwani hatuuoni ukitumika katika Agano la Kale, Mungu anayekuja kama mwivi. Ni lugha hasi na yenye kuogofya na kukatisha tamaa. Ni katika Agano Jipya tunaona sura hii ya ujio wa Mungu kama mwivi inatumika kama tunavyosoma katika 1 Wathesalonike 5:2 na 2 Petro 3:10 na Ufunuo 3:3 na 16:15. Labda wengine tunapata picha kuwa Mungu anakuja kwa kutuvizia au ziara za kushtukiza kama tunavyosikia kwa baadhi ya wanasiasa wetu au viongozi fulani.

Kwa kweli hapana na Mungu wetu ni Baba mwema kamwe hawezi kufanya matendo ya kutukomoa au ili atukute tukiwe hatupo tayari. Ni vema kutafakari vema la sivyo wapendwa Injili inakoma kuwa Habari Njema, na inakuwa Habari ya kutisha na kukatisha tamaa na hilo sio lengo kwani haitakuwa Injili. Ujio wake daima ni neema kwetu, ni kairos kwetu. Natumai wale mnaofuatilia tafakari zangu mtakuwa mmekutana na tofauti ya kronos na kairos maneno ya kigiriki yote yakiwa na maana ya muda, ila kairos sio muda wa kupimwa kama tunavyoweza kusema sasa ni saa 1 au 2 au mchana au mwezi au mwaka fulani bali ni neema za Mungu kwetu. Kila tunapomzungumzia Mungu tukumbuke tunatoka katika kronos na tunazumzungumzia katika kairos tu. Mungu anakuja kwetu sio kwa nia na lengo la kuiba au kutuangamiza bali ili atukomboe na kutupa uzima wa milele. Kama mwivi ni wazi ni lugha inayoogofya bali ni kututaka tuwe tayari daima kwani kuwa mfuasi wa Kristo ni maisha ya daima na hivyo hakuna likizo ya kuishi imani yetu, Imani haina likizo! Imani ni maisha yetu ya siku kwa siku, Injili ni kuhusu maisha yetu ya kila siku.

Heri watumishi wale Bwana akiwakuta wanakesha: Mfano wa tatu ni jibu la Yesu kutokana na swali la Mtume Petro. Pamoja na kwamba sote kama wafuasi na rafiki zake Yesu tunaalikwa kuwa watumishi, bado pia kuna wale wenye nafasi maalumu zaidi katika jumuiya zetu na ndio leo hii makasisi na maaskofu kwa namna ya pekee kabisa. Ni angalisho kwao pia kukumbuka kundi si lao ila daima ni la Kristo na wao wamewekwa kuwa waangalizi tu na kamwe wasigeuke kuwa mabwana wakubwa na watawala bali wanapewa wajibu na Yesu mwenyewe. Ni angalisho kwetu makuhani kukumbuka kuepa kishawishi cha kudhani kuwa sisi ndio wenye kundi bali daima ni kundi la Kristo yaani Kanisa lilikokabidhiwa kwetu kwa kupakwa mafuta ili kutumikia watu wake. Hapa kuna mengi tunaweza kusema ila itoshe tukumbuke kuwa sisi sote ni watumishi labda katika ngazi mbali mbali bali mwenye kundi ni Kristo mwenyewe. Na hivyo tutumikie kila mmoja kwa nafasi yake aliyokabidhiwa na mwenye kundi yaani Kristo Mwenyewe.

Wapendwa, Kristo anatualika sote kila mmoja kwa nafasi yake kuwa mtumishi mwaminifu na anayekesha akiwa na taa inayowaka na ndio utayari wetu wa kumtumikia mwingine kwa upendo na kila wakati ninapohitajika kufanya hivyo kwani sijui siku wala saa. Tukumbuke tunakutana na Yesu kila siku kwa ndugu zetu wanaokuwa wahitaji wa upendo na utumishi wetu wa aina yeyote ile. Katika sura ya mwingine nakutana na Mungu muhitaji, naalikwa kutumikia bila kuweka masharti, kupenda bila kujibakiza. Upendo hauna likizo! Upendo hauna muda, ni wa daima! Basi tumuombe Mungu aliyeasili ya wema wote atujalie nasi neema zake za kupokea wito wake wa kuwa watumishi waaminifu katika maisha yetu ya ufuasi. Imani haina likizo, imani ni maisha ya daima, imani ni kujifunga kiunoni na kutumikia kwa upendo na hapo kweli tunaweka akiba yetu mbinguni, akiba isiyooza milele. Nawatakia tafakari njema na Dominika njema.

10 August 2019, 11:49