Tafuta

Vatican News
Katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Hospitali ya Rufaa ya Mt. Gaspar, Itigi, Tanzania, kama sehemu ya kumbu kumbu hii, inawekeza katika michezo kwa afya! Katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Hospitali ya Rufaa ya Mt. Gaspar, Itigi, Tanzania, kama sehemu ya kumbu kumbu hii, inawekeza katika michezo kwa afya!  (ANSA)

Hospitali ya Rufaa ya Mt. Gaspar Itigi: Inawekeza katika michezo

Mradi wa Ujenzi wa Uwanja wa Michezo Itigi, unapania pia kukuza na kudumisha vipaji vya wanamichezo ndani na nje ya Mkoa wa Singida. Ni uwanja utakaokuwa na uwezo wa kubeba mashabiki zaidi ya elfu ishirini kwa wakati mmoja! Huu ni mchango wa Kanisa katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Michezo kwa afya!

St. Gaspar Referal Hospital-Itigi, 30 Years of Services: investement on sports

Na Rodrick Minja, Dodoma & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, michezo inayo nafasi muhimu sana katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Michezo ni nyenzo msingi katika kusimamia na kudumisha haki msingi za binadamu; ni njia ya mchakato wa utakatifu; ni mahali muafaka pa kuonja uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji, umoja, udugu na mshikamano wa kweli unaovunjilia mbali ubinafsi kwa kukazia umoja katika ukweli wake! Baba Mtakatifu anaendelea kusema, kwamba, michezo ni muhimu sana katika ujenzi wa jamii na ushiriki mkamilifu katika kudumisha: haki, amani na utulivu bila vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuendelea kuwafunda vijana wa kizazi kipya kwa njia ya michezo, umuhimu wa kujikita katika urafiki, udugu na haki, mambo muhimu sana katika ulimwengu mamboleo.

Lakini, Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kuandika ukurasa mpya wa michezo katika ulimwengu mamboleo kwa kujikita katika: ushirikishwaji; ukweli, uwazi na uaminifu pamoja na kuwa na upendeleo kwa maskini. Huu ni ushauri uliotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko katika kampeni kuhusu umuhimu wa michezo, ambayo sasa imeandikiwa kitabu kijulikanacho kama “Sport una lettera alla volta” chenye kurasa 144 na kimechapishwa na Malcor D’ na kwa sasa tayari kiko kwenye maduka ya vitabu. Ni katika muktadha huu, Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Manyoni, Singida, Tanzania, inayomilikiwa na kuendeshwa na Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, katika kipindi hiki cha kumbu kumbu ya miaka 30 ya uwepo na utume wake, inapenda kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini!

Hospitali imeamua kuwekeza katika ujenzi wa uwanja wa michezo wa kisasa, kama sehemu ya maboresho ya afya kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Singida. Padre Serafini Lesiriamu, C.PP.S., Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar anasema, mradi huu licha ya kuboresha afya ya wananchi wa mji mdogo wa Itigi na viunga vyake, unapania pia kukuza na kudumisha vipaji vya wanamichezo ndani na nje ya Mkoa wa Singida. Ni uwanja utakaokuwa na uwezo wa kubeba mashabiki zaidi ya elfu ishirini kwa wakati mmoja! Huu ni mchango wa Kanisa katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Uwanja huu wa kisasa utakuwa na viwanja vya mpira wa miguu, kikapu, pete, wavu pamoja na viwanja viwili kwa ajili ya michezo ya watoto.

Familia ya Mungu Kanda ya Kati nchini Tanzania licha ya kufurahia huduma ya afya, elimu, maji, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu, sasa itapata fursa pia ya kuendelea kunufaika na huduma zitakazotolewa baada ya uwanja huu unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa Mwaka 2019. Tangu awali, uwanja wa michezo wa Parokia ya Itigi, Jimbo Katoliki Singida, umekuwa ukitumika kama daraja la kuwakutanisha wananchi wa Itigi na viunga vyake wakati wa mashindano mbali mbali kwenye mji huu mdogo unaoendelea kukua kwa kasi kutokana na maboresho ya huduma mbali mbali za kijamii, dhamana inayotekelezwa kwa namna na Wamisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu, ambao tangu mwaka 1967 wamekuwa ni chachu ya maendeleo fungamani ya binadamu Kanda ya Kati, licha ya changamoto zinazoendelea kujitokeza kila kukicha!

Maadhimisho ya kumbu kumbu ya Miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi ni wakati uliokubalika wa kuwashirikisha watu wa Mungu, ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Michezo ni wakati muafaka wa kuonja: uzuri, furaha na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Mfufuka wanapokuwa uwanjani. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hata wanamichezo wanaweza kuwa ni watakatifu, kwani daima wanaitwa na kuhamasishwa kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao kila kukicha! Michezo inapania kujenga na kuimarisha urafiki na udugu kati ya watu; maelewano na amani; kuheshimiana, maridhiano na utulivu, kwa kuthamini tofauti zinazojitokeza kati ya watu. Tunu msingi za michezo zinapaswa kusisitizwa miongoni mwa vijana na watoto, ili kuwasaidia kutambua kwamba, kila fursa iliyopo inaweza kutumika kwa ajili ya maboresho ya maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Michezo Tanzania

 

06 August 2019, 14:46