Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Raphael S. Ndingi Mwana a'Nzeki, Askofu wa kwanza mzalendo nchini Kenya anaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu 31 Januari 1969 Askofu mkuu Raphael S. Ndingi Mwana a'Nzeki, Askofu wa kwanza mzalendo nchini Kenya anaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu 31 Januari 1969  (ANSA)

Barua ya Papa Francisko kwa Mapadre: Askofu mkuu Raphael Ndingi Mwana a'Nzeki: 50 Uaskofu

Askofu mkuu Mstaafu Raphael S. Ndingi Mwana a'Nzeki ndiye Askofu wa kwanza mzalendo kuwekwa wakfu nchini Kenya, mwakai 1969 na Mtakatifu Paulo VI. Katika maisha na utume wake, amewahi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Machakos, na Jimbo la Nakuru. Baadaye, Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Nairobi na kusimikwa rasmi tarehe 21 Aprili 1997. Yaani, hadi raha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney, Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia Mapadre wote duniani, barua ya upendo na mshikamano wa kibaba, akiguswa na furaha ya huduma inayotolewa na Mapadre sehemu mbali mbali za dunia, kila kukicha! Hawa ni mapadre ambao wengine wamechoka na kudhohofu kwa afya mbaya na changamoto za maisha; kuna baadhi yao wametumbukia katika mateso na mahangaiko makubwa ya ndani kutokana na huduma yao kwa familia ya Mungu. Ni katika muktadha huu, familia ya Mungu nchini Kenya inamwimbia utenzi wa sifa na shukrani kwa amana na utajiri mkubwa aliomkirimia Askofu mkuu Mstaafu Raphael S. Ndingi Mwana a'Nzeki wa Jimbo kuu la Nairobi, Kenya anaposherehekea Jubilei ya Miaka 50 tangu alipowekwa wakfu kama Askofu. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Mstaafu Raphael S. Ndingi Mwana a'Nzeki ndiye Askofu wa kwanza mzalendo kuwekwa wakfu nchini Kenya kunako tarehe 31 Januari 1969, wakati wa hija ya Mtakatifu Paulo VI, Barani Afrika.

Katika maisha na utume wake, amewahi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Machakos kuanzia mwaka 1969-1971; Jimbo Katoliki la Nakuru kuanzia mwaka 1996-1997. Baadaye Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Nairobi na kusimikwa rasmi tarehe 21 Aprili 1997. Tarehe 6 Oktoba 2007 Askofu mkuu Raphael S. Ndingi Mwana a'Nzeki akang’atuka kutoka madarakani. SHUKRANI KWA MAPADRE: Baba Mtakatifu Francisko anasema haachi kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wito wa Upadre kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambao si kwa mastahili yao wenyewe, bali wameitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kipindi cha shida na magumu ya maisha, iwe ni fursa ya kurejea tena katika zile nyakati angavu za sadaka na huduma kwa watu wa Mungu, ili kugundua tena neema za Mungu katika maisha na utume wao, ili kuwasha tena  na tena furaha inayokita mizizi yake katika unyenyekevu, ili kamwe majonzi na uchungu wa moyo, yasizime ile furaha na uungwana!

Huu ni wakati wa kusimama na kusema, Mimi hapa Bwana, nipe nguvu ya kusimama tena ili nitoe huduma kwa watakatifu majirani; tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Mapadre wazee wagundue tena ndani mwao, ile furaha waliyokuwa wanapata walipozitembelea familia za Kikristo; walipokuwa wanakwenda kutoa Sakramenti za Kanisa kwa wazee na wagonjwa. Askofu mkuu Mstaafu Raphael S. Ndingi Mwana a'Nzeki, kwa wakati huu, umri umekwenda sana, kwani alizaliwa tarehe 25 Desemba 1931 huko Mwala, Machakos nchini Kenya. Ni kiongozi aliyesimama kidete katika misingi ya imani, kanuni maadili na utu wema. Alipigania haki, amani, umoja wa kitaifa dhidi ya siasa na sera za ubaguzi wa kikabila sanjari na demokrasia nchini Kenya. Ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mapadre watambue kwamba, wamepakwa mafuta ya wokovu, ili kuwahudumia jirani zao na kamwe wasikate tamaa, ndiyo maana anasema, kamwe haachi kumtolea Mwenyezi Mungu shukrani kwa ajili yao.

Mapadre watambue udhaifu wao wa kibinadamu, karama na neema walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu, ili kuweza kuamua na kutenda kwa ukarimu. Mapadre waendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, kwa sababu huruma ya Mungu yadumu milele. Moyo wa shukrani ni silaha madhubuti inayowawezesha kutafakari ukarimu wa Mungu katika maisha yao, mshikamano, msamaha, subira, uvumilivu na upendo, kiasi hata cha kuthubutu kusema kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro, “Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi”, lakini Kristo Yesu akamwambia “Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu” kwa sababu huruma yake yadumu milele!

Baba Mtakatifu anawashukuru Mapadre kwa uaminifu na sadaka wanayotoa kila kukicha, kielelezo cha utekelezaji wa Agano la Mungu lisilokuwa na kikomo. Ni wakati wa kusherehekea uaminifu wa Mungu usiokuwa na kikomo, kwani bado anaendelea kuwaamini licha ya dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu, kwa kutambua kwamba wanabeba wito huu mtakatifu katika vyombo vya udongo. Wanatambua kwamba, hata katika udhaifu wao, Mwenyezi Mungu anaweza kuonesha ukuu na ushindi kwa sababu huruma yake yadumu milele! Baba Mtakatifu anawashukuru Mapadre kwa kuendelea kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao katika shughuli mbali mbali za kichungaji. Kwa hakika Mapadre wamekuwa ni vyombo vya mshikamano na upendo wakati wa raha na shida; hata pale Mapadre walipokosa na kukosoana kwa upendo, kwani huruma yake yadumu milele.

Baba Mtakatifu anawashukuru kwa udumifu wao katika shughuli mbali mbali za kichungaji, kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea watu wao kama ilivyokuwa kwa Musa, Mtumishi wa Mungu, kwa sababu huruma yake yadumu milele. Mapadre wanashukuriwa kwa kuadhimisha Sakramenti za huruma ya Mungu; kwa kuwaongoza na kuwasindikiza waamini wao katika hija ya toba na wongofu wa ndani, kiasi cha kuruhusu ile ngazi ya huruma ya Mungu iweze kushuka katika udhaifu na dhambi zao, tayari kuonja utakaso, daima wakitambua kwamba, wanapaswa kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma, tayari kuwaongoza waamini wao kwenye mwanga angavu kwa sababu huruma yake yadumu milele!

Mapadre wanashukuriwa kwa kuendelea kuwa ni Wasamaria wema ili kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake wanaoteseka na kuogelea katika dimbwi la dhambi. Hali hii iwakumbushe Mapadre kwamba, wametwaliwa kutoka kati ya watu kwa ajili ya mambo ya Mungu, changamoto na mwaliko wa kuambata unyenyekvu pasi na makuu, kwa ajili ya Injili, kwani huruma yake yadumu milele! Baba Mtakatifu anawaalika Mapadre kumtolea Mungu sifa na shukrani kwa ajili ya utakatifu wa watu wa Mungu; awakirimie zawadi ya kutafakari dhamana na utume unaotekelezwa na watu wa Mungu katika hija ya maisha yao, katika hali ya mateso, mahangaiko na hata wakati mwingine wa kutoelewana. Baba Mtakatifu anasema, katika maisha ya waamini, anaona utakatifu wa Kanisa, katika ushuhuda wa maisha na utakatifu wao, watiwe shime kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu!

Katika shukrani za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mapadre wote duniani, tunamwona pia ndanimwe, Askofu mkuu Mstaafu Raphael S. Ndingi Mwana a'Nzeki, ambaye alichakarika usiku na mchana kufundisha katekesi; akawekeza nguvu na akili zake katika sekta ya elimu ili kuwakomboa watu wa Mungu nchini Kenya kutoka katika lindi la ujinga, umaskini na magonjwa. Licha ya shughuli zote hizi, lakini bado alikuwa ni mwana michezo wa kutupwa, ndiyo maana Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1999 akamteuwa kuwa ni mjumbe wa Baraza la Kipapa la Utamaduni. Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha watu wa Mungu kwamba, wazee kama Askofu mkuu Mstaafu Raphael S. Ndingi Mwana a'Nzeki wana ndoto lakini vijana wana utabiri!

Askofu Mkuu Ndingi

 

 

10 August 2019, 16:19