Tafuta

Vatican News
Wauguzi na wakunga wametakiwa kuhakikisha kwamba, wanatekeleza kwa vitendo viapo vyao vya kazi kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa! Wauguzi na wakunga wametakiwa kuhakikisha kwamba, wanatekeleza kwa vitendo viapo vyao vya kazi kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa! 

Askofu mkuu Nyaisonga: Wakunga na wauguzi tunzeni viapo vyenu!

Askofu mkuu Nyaisonga amewataka wauguzi na wakunga kufanya kazi kwa juhudi, bidii, maarifa, nidhamu, maadili na utu wema, kwa kutambua kwamba, mgonjwa wanayemhudumia ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusimamia vyema rasilimali na utajiri wa nchi na hivyo kuuelekeza katika huduma makini za kijamii.

Na Thompson Mpanji, Songwe na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibu alisema, maendeleo makubwa katika vifaa vya tiba ya afya kwa mwanadamu, yamewezesha kuwa na njia pamoja na teknolojia mpya ya kuchunguza na kutibu magonjwa, kiasi hata cha kuibua matatizo na changamoto za kanuni maadili na utu wema. Haya ni mambo yanayotishia maisha, utu na heshima ya binadamu. Kutozingatia uhuru wa dhamiri kunahatarisha utu na heshima ya binadamu! Majiundo makini kitaaluma yaende sanjari na majiundo ya maisha ya kiroho, ili kutambua na kuthamini utu, heshima, ustawi na mafao ya wagonjwa. Mgonjwa anapaswa kuonekana na kutambuliwa kuwa ni jirani anayeteseka.

Baba Mtakatifu anasema, changamoto zinazoendelea kujitokeza katika sekta ya afya zichambuliwe na kupewa ufumbuzi wa pamoja, ili kuwa na sauti moja. Wagonjwa wanatofautiana kwa mahitaji, kumbe, wahudumiwe kwa heshima, kwani hii ni dhamana tete, ambayo wakati mwingine haifahamiki vyema, wala kuthaminiwa na jamii! Wahudumu wa sekta ya afya, wanapaswa pia kuangaliwa kwa jicho la upendo na huruma kwa kutambua kwamba, ugumu wa kazi na changamoto zake, vinaweza kusababisha majanga makubwa kwa wafanyakazi wenyewe. Mazingira mazuri ya kazi, stahiki za wafanyakazi pamoja kuthaminiwa ni mambo yanayopaswa kuangaliwa na kupyaisha daima.

Chuo cha Uuguzi na Ukunga cha Mwambani, kinachomilikiwa na kuendeshwa na Jimbo kuu Katoliki la Mbeya, kilianzishwa kunako mwaka 2005 ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa kada ya wauguzi Jimboni humo na kama mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania. Katika hotuba yake elekezi, Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa jimbo Kuu la Mbeya ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amewataka wakunga na wauguzi waliohitimu masomo yao kuhakikisha kwamba, wanamwilisha kiapo cha utii waliochokitoa mbele ya umati wa watanzania katika maisha na huduma yao kwa wagonjwa, kama ilivyokuwa kwa Muasisi wa fani ya uuguzi duniani Florence Nightngale.

Askofu mkuu Nyaisonga amewataka wauguzi na wakunga kufanya kazi kwa juhudi, bidii, maarifa, nidhamu, maadili na utu wema, kwa kutambua kwamba, mgonjwa wanayemhudumia ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusimamia vyema rasilimali na utajiri wa nchi na hivyo kuuelekeza katika huduma makini za kijamii. Kanisa litaendelea kushirikiana na Serikali katika mchakato wa maboresho ya huduma ya afya kwa njia ya ruzuku, vifaa tiba na ushauri.

Kwa upande wake, Bwana Samweli Jeremiah, Mkuu wa Wilaya ya Songwe, amelishukuru Jimbo kuu la Mbeya kwa kuendelea kushirikiana na kushikamana na serikali katika huduma ya afya. Ni matumaini yake, mahafali haya ya tisa yatakuwa ni chachu ya mabadiliko ya maisha kwa wakunga na wauguzi wakitambua kwamba, wamesoma na kuhitimu katika Chuo kinachoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa. Kumbe, mambo makuu ya kuzingatia ni: uhai, utu, heshima na haki msingi za wagonjwa na familia zao. Huduma katika sekta ya afya ni sehemu ya mbinu mkakati wa uinjilishaji wa kina unaotekelezwa na Kanisa nchini Tanzania.

Mpango mkakati wa maboresho ya huduma ya afya ni changamoto ambayo inavaliwa njuga na Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli. Wakati huu, kuna hospitali zaidi 67 na vituo vya afya 350 vinaendelea kujengwa kwa viwango na ubora unaotakiwa. Vyote hivi vikikamilika vitakuwa ni chemchemi ya ajira kwa wanafunzi kutoka sehemu mbali mbali za Tanzania. Lakini, wale wanaohitimu kutoka katika vyuo vinavyoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa wanao wajibu mkubwa zaidi, kwani wanapaswa kuzingatia: sheria, kanuni na maadili waliyojifunza, ili hatimaye, waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo wa Mungu kwa watanzania, lakini zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kwa upande wake, Victoria Mwakigili, Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Songwe amewataka wauguzi na wakunga waliohitimu masomo yao kuzingatia: uadilifu, nidhamu na uwajibikaji; kwa kujikita katika mambo ya: sheria, kanuni na maadili ya wauguzi na wakunga. Wawe na lugha nzuri kwa wagonjwa watakaowahudumia, kwa kujali na kuthamini utu na heshima yao. Kimsingi wawe ni kioo kizuri kwa jamii ya watanzania katika huduma watakayokuwa wanatoa kwa wagonjwa na familia zao.

Wauguzi Mwambani

 

22 August 2019, 15:34