Tafuta

Vatican News
SECAM Jubilei ya Miaka 50: Dhamana na utume wa waamini walei katika sera na mikakati mbali mbali ya maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. SECAM Jubilei ya Miaka 50: Dhamana na utume wa waamini walei katika sera na mikakati mbali mbali ya maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. 

SECAM Jubilei miaka 50: Dhamana na Utume wa Waamini Walei Afrika

Wawakilishi wa waamini walei katika maadhimisho ya jubilei ya Miaka 50 ya SECAM, wamewataka Mababa wa SECAM kutambua dhamana na nafasi ya waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika; Kanisa liwajengee waamini walei sera na mikakati ya kuyatakatifuza malimwengu na kwamba, uinjilishaji mpya ukite mizizi yake katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dhamana na utume wa waamini walei ndani ya Kanisa kwa namna ya pekee, ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican unaobainisha: wito, utume na dhamana ya waamini walei katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu na Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa! Waamini walei ni mhimili wa Kanisa la Kristo wanaitwa kutekeleza: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo katika maisha yao, kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Kumekuwepo na uanzishwaji wa mashirika na vyama vya kitume Barani Afrika, ambavyo vimekuza na kudumisha ari na moyo wa kimissionari, kwa kusaidia malezi na majiundo makini ya maisha ya: imani na uadilifu, Sakramenti za Kanisa pamoja na maisha ya sala; mambo muhimu yanayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini, kama kielelezo cha imani tendaji!

Mababa wa SECAM wanasema, sasa umefika wakati wa kuangalia ya mbeleni kwa matumaini zaidi, ili kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa zinazoendelea kujitokeza miongoni mwa waamini walei Barani Afrika, ili waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Kanisa Barani Afrika linataka kutoka kimasomaso, ili kuinjilisha kama Jumuiya bila kuwatenga watu, huku waamini walei wakipewa kipaumbele cha pekee. Waamini walei wasimame kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai, ndoa na familia ili kupambana na utamaduni wa kifo. Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagscar, SECAM, imekuwa pia ni fursa ya kuwahamasisha waamini walei kuendelea kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika, kwa kutambua mchango wao mkubwa katika kulitegemeza Kanisa Barani Afrika kwa hali na mali.

Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, waamini walei wanapata majiundo makini, wanakuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo, baada ya wao wenyewe kukutana na huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! Jacinta W. Odongo, mwandishi wa habari wa AMECEA wakati wa maadhimisho ya Mkutano mkuu wa 18 wa SECAM amefanya mahojiano maalum na Bwana Thomas Adefolusho Adekoya, Rais wa Halmashauri ya Walei Kitaifa nchini Nigeria aliyekuwa amepewa mwaliko maalum kuhudhuria maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa SECAM. Pengine hii ni mara ya kwanza katika historia ya Kanisa Katoliki nchini Nigeria kuwa na mwakilishi wa waamini walei katika mkutano mkuu wa SECAM ambao umehudhuriwa na wajumbe zaidi ya 400 wakiwemo: Makardinali 9, Maaskofu wakuu 55, Maaskofu 106, mapadre 60 bila kuwasahau watawa na wawakilishi kutoka ndani na Nje ya Kanisa Barani Afrika.

Bwana Thomas Adefolusho Adekoya, Rais wa Halmashauri ya Walei Kitaifa nchini Nigeria anasema, Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican unalitaka Kanisa kutoa kipaumbele cha pekee kwa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa kwani wao ni sehemu kubwa zaidi ya watu wa Mungu, ikilinganishwa na idadi ya wakleri na watawa ndani ya Kanisa. Sera na mikakati mbali mbali inayoamriwa na kupitishwa na Mama Kanisa watekelezaji wake wakuu ni waamini walei, ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kulitegemeza Kanisa kwa rasilimali watu, vitu na fedha. Kanisa Barani Afrika liendelee kujiwekea sera na mikakati ya kuwashirikisha zaidi waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuzingatia ukweli na uwazi na kwa njia hii, kwa hakika Kanisa Barani Afrika litaendelea kucharuka zaidi katika mchakato wa uinjilishaji  mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Bwana Thomas Adefolusho Adekoya wakati alipokuwa akichangia hoja kwenye Mkutano wa SECAM amewaomba Mababa wa SECAM kuhakikisha kwamba, kuanzia sasa na kuendelea waamini walei kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar wanashiriki katika mikutano ya SECAM kama sehemu ya utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika, changamoto iliyovaliwa junga na Mtakatifu Paulo VI mara tu baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na kasi hii kwa sasa inaendelezwa na Baba Mtakatifu Francisko. Kama ilivyokuwa kwa vijana waliotoa Ombi la Kuanzishwa kwa Jukwaa la Vijana Barani Afrika, Halmashauri Walei nao wanataka kuwa na Baraza la Halmashauri Walei Afrika. Pili, Bwana Thomas Adefolusho Adekoya amesema, waamini walei wanao mchango mkubwa katika kuyatakatifuza malimwengu kwa chachu ya tunu msingi za Kiinjili sanjari na Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Kwa njia hii, waamini walei wakifundwa barabara wanaweza kuwa ni chachu ya uongozi bora, mashuhuda na vyombo vya upatanisho, haki na amani Barani Afrika. Waamini walei kwa hakika ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Waamini walei wakifundwa barabara na kuhamasishwa, wanaweza kuleta mageuzi makubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu Barani Afrika katika ujumla wake. Tatu, mchakato wa uinjilishaji mpya unapaswa kuwashirikisha waamini walei, ili kuchangia katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Mambo makuu yaliyobainishwa kwenye Tamko la Kichungaji la SECAM, Kampala, Uganda, 2019, yanapaswa kusambazwa na waamini walei kwa kushirikiana kwa karibu zaidi na wakleri pamoja na watawa. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Tamko la Kampala linawafikia waamini hata katika Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, utambulisho wa Kanisa kama familia ya Mungu Barani Afrika.

Ikiwa kama Mababa wa SECAM, watashindwa kutekeleza dhamana hii, waamini walei, wataendelea kuwa ni watazamaji na wasindikizaji tu wa maamuzi makubwa yanayofanywa na Mama Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto wake, lakini kwa bahati mbaya yanabaki yakiwa yamefungiwa kwenye Makabati! Bwana Thomas Adefolusho Adekoya, Rais wa Halmashauri ya Walei Kitaifa nchini Nigeria anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya SECAM pamoja na kupata nafasi ya kuhojiwa na vyombo vya mawasiliano ya jamii. Ni matumaini yake kwamba, mawazo yake yatakuwa ni changamoto na hamasa kwa waamini walei kuyakumbatia ya mbeleni kwa matumaini makubwa!

SECAM: Walei
29 July 2019, 11:28