Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XV ya Mwaka C wa Kanisa: Msamaria mwema ni kielelezo cha utimilifu wa Torati na Unabii! Wewe ni jirani ya nani? Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XV ya Mwaka C wa Kanisa: Msamaria mwema ni kielelezo cha utimilifu wa Torati na Unabii! Wewe ni jirani ya nani? 

Neno la Mungu: Jumapili XV ya Mwaka: Msamaria Mwema!

Kumpenda Mungu ni kuishika imani: kumkiri Kristo na kushikamana naye katika maisha ili kuufikia utimilifu wa upendo na upendo halisi ambao ni Mungu mwenyewe. Huu ni upendo unaovuka vikwazo vya utengano na matabaka ambayo jamii zetu wakati mwingine zinayaweka. Msamaria mwema ni kielelezo cha upendo unaojipambanua katika kiini chake cha kweli, huduma na wokovu.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunatafakari Masomo ya Liturujia ya dominika ya 15 ya mwaka C wa Kanisa. Upendo unajidhihirisha leo kama ndio msingi na kilele cha sheria na amri zote. Kama yanavyokazia pia maneno ya sala ya leo ya mwanzo kuwa Mungu ameziunganisha sheria na amri zote katika kumpenda Yeye na kumpenda jirani.

Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Kum 30:10-14 ) ni kutoka katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati na ni hotuba ya mwisho ya Musa kwa Waisraeli. Ni hotuba kwa Waisraeli waliochoka kwa mwendo jangwani na kwa magumu mbalimbali waliyokuwa wanapitia. Katika sehemu ya hotuba hiyo ambayo ndio somo la kwanza leo, Musa anagusia magumu yao kuwafanya waone kuwa wao bila Mungu si kitu. Hapo anawaalika kurudi kwa Mungu kwa toba na kushika Agano. Anawakumbusha kuwa maagizo ya Mungu katika Agano lao hayapo mbali nao hadi wahangaike kuyatafuta bali yamo mioyoni mwao. Hata kwetu Musa leo anatukumbusha kuwa Mungu tunayemtafuta katika kipindi cha magumu yetu hayuko mbali nasi bali yuko daima pamoja nasi na ndani yetu.

Somo la pili (Kol 1:15-20 ) ni kutoka waraka wa mtume Paulo kwa Wakolosai. Paulo katika waraka huu analenga kutatua tatizo ambalo moja kwa moja ni la kiimani, tatizo lililoletwa na mafundisho potofu juu ya nafasi ya Kristo katika ukombozi wa ulimwengu. Katika somo hili Paulo anaonesha kwa njia ya utenzi nafasi ya Kristo katika uumbaji na katika ukombozi. Ana nafasi ya pekee katika uumbaji kwa sababu ni katika Yeye vitu vyote viliumbwa na ni  mzaliwa wa kwanza (prototokos) kwa maana ya kuwa msingi wa vyote vilivyoumbwa. Hali kadhalika Kristo ndiye mkombozi wa pekee wa ulimwengu. Ni kichwa cha mwili wake yaani kanisa na ndiye mpatanishi wa vitu vyote na mkombozi kwa damu yake msalabani.

Injili (Lk 10:25-37) Katika injili ya dominika ya leo, Kristo anafundisha kwa njia ya mfano. Anatoa mfano wa mtu aliyekuwa anasafiri toka Yerusalemu kwenda Yeriko akaangukia mikononi mwa wanyang’anyi, wakamjeruhi na kumwacha karibu ya kufa. Ufunguo wa kuuelewa mfano huu upo katika swali alilomrudishia yule mwanasheria aliyemuuliza afanye nini ili niurithi uzima wa milele. Na swali lenyewe ni hili “imeandikwa nini katika Torati? Wasomaje? Swali hili lina maswali mawili ndani yake na tayari linamtahadharisha mwanasheria kuona kuwa katika upendo kwa Mungu na kwa jirani ni msingi kuanzia katika kilichoandikwa (imeandikwa nini) lakini kutokubaki hapo bali kwenda katika tafsiri ifaayo ya matakwa ya sheria kadiri ya mazingira (wasomaje). Kutoka hapa tunaona katika mfano kuwa kuhani na mlawi walipopita na kumwona aliyejeruhiwa walipita kando, kwa nini?

Kwa sababu sheria ya Musa iliwakataza kugusana na damu au kugusa maiti wanapokwenda katika ibada (Rej. Hes 19: 11-13, Walawi 21: 1-4, 11). Msamaria yeye ambaye kwanza hakuwa Myahudi na tena licha ya kuwa na uadui nao hakuyaangalia yote hayo bali aliliangalia hitaji yule aliyejeruhiwa akaenda akamwokoa. Mwishoni Yesu anauliza, kati ya hao watatu ni yupi aliyekuwa jirani yake yule aliyeangukia mikononi mwa wanyang’anyi? Tukiliangalia vizuri swali hili tunaona kuwa Yesu haulizi yule aliyejeruhiwa alikuwa jirani ya nani. Kumbe kwa swali la mwanasheria “na jirani yangu ni nani?” Yesu anatumia mfano huu kumuonesha kuwa kabla ya kujibu swali hilo, yule anayetaka kujua jirani yake ni nani anapaswa kwanza yeye mwenyewe kujiuliza “mimi ninataka kuwa jirani kwa nani?” Ni kwa nani niko tayari kutoa msaada na ni kwa nani napata kigugumizi; ni kwa nani naweza kumfikia kwa urahisi na ni kwa nani natafuta visingizio. Ni hapo nitajua jirani yangu ni nani.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Maandiko Matakatifu katika dominika ya leo yanatualika kutafakari juu ya upendo kama wajibu tulionao nao kwa Mungu na wajibu tulionao kwa jirani. Upendo unajidhihirisha leo kama ndio msingi na kilele cha sheria na amri zote. Kama yanavyokazia pia maneno ya sala ya leo ya mwanzo kuwa Mungu ameziunganisha sheria na amri zote katika kumpenda Yeye na kumpenda jirani. Kumpenda Mungu ni kulishika Neno lake na kukubali kuongozwa nalo katika maisha ya kila siku. Musa anawaeleza waisraeli kuwa Neno hilo haliko mbali nao. Mungu amekwishalipanda katika mioyo yao nao wanalisikia wanapozifuata dhamiri zao njema. Kumpenda Mungu ni kuishika imani: kumkiri Kristo na kushikamana naye katika maisha ili kuufikia pamoja naye ukamilifu wa upendo na upendo halisi ambao ni Mungu mwenyewe. Mfano wa Yesu katika injili ya leo ni mfano maridhawa wa kuulewa upendo kwa jirani: upendo unaovuka vikwazo vya utengano na matabaka ambayo jamii zetu wakati mwingine zinayaweka; upendo unaojipambanua katika kiini chake cha kweli, huduma na wokovu.

Liturujia J15
12 July 2019, 16:46