Tafuta

Vatican News
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu kwa watu wote! Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu kwa watu wote! 

Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili XIV: Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu!

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanafundisha kuwa Kanisa limetumwa na Mungu kwa mataifa yote ili liwe Sakramenti ya wokovu kwa wote. Nalo kwa asili ya ukatoliki wake na kwa kulitii agizo la Kristo mwanzilishi wake, linafanya bidii ya kuitangaza injili kwa watu wote ili Neno la Mungu liendelee na kutukuzwa na Ufalme wa Mungu utangazwe na kusimikwa duniani kote.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunatafakari Masomo ya Liturujia ya dominika ya 14 ya mwaka C wa Kanisa. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unafundisha kuwa Kanisa limetumwa na Mungu kwa mataifa yote ili liwe Sakramenti ya Wokovu kwa wote. Nalo kwa asili ya ukatoliki wake na kwa kulitii agizo la Kristo mwanzilishi wake, linafanya bidii ya kuitangaza injili kwa watu wote ili Neno la Mungu liendelee na kutukuzwa na Ufalme wa Mungu utangazwe na kusimikwa duniani kote (Rej. Ad Gentes 1).

Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Is 66:10-14c ) ni kutoka katika kitabu nabii Isaya. Nabii anaandika kuwapa moyo wote wanaolia pamoja na Yerusalemu. Yerusalemu, mji wa Mungu unalia kwa sababu umeharibiwa na wavamizi. Kuta zake zimevunjwa na hekalu limebomolewa wakati wa vita na uhamisho wa watu. Watu wanalia kwa sababu baada ya kurudi kutoka uhamishoni hawauoni tena mji wa Yerusalemu katika utukufu uliokuwa nao mwanzo. Hata hivyo, Nabii anawaandikia wafurahi, wafurahi kwa sababu Mungu yuleyule aliyewatoa utumwani sasa anawaahidi kuwa mji wa Yerusalemu utajengwa upya: amani yake itarejea, utukufu wake utarudi nao wataufurahia mji wao kama mwana anavyomfurahia mamaye anayemfariji.

Somo la pili (Gal. 6:14-18 ) ni kutoka waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia. Katika waraka huu, Paulo amepambana vikali sana na wahubiri wa Kiyahudi waliosisitiza uyahudi wao kuliko imani kwa Kristo. Katika barua hii nzima kwa Wagalatia Paulo anaonesha kuwa mtu anakombolewa kwa imani kwa Yesu Kristo na wala si kwa matendo ya sheria au mila za kiyahudi na mapokeo ya wazee yao. Katika somo hili ambalo ni sehemu ya mwisho ya waraka kwa wagalatia, Paulo anahitimisha waraka kwa akisisitizia kwa mara nyingine tena kuwa yeye haoni fahari juu ya kitu chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Japokuwa naye ni Myahudi lakini haoni kuwa utu wake wa sasa kama mkristo unajipambanua kwa uyahudi wake: katika tohara au mila za kiyahudi, bali katika kile ambacho msalaba wa Kristo umempa, yaani ukombozi na neema.

Somo hili linatualika tutafute kuweka uwiano sahihi kati ya imani na mila zetu  (pamoja na desturi na tamaduni). Mila zinatupatia utambulisho wetu katika jamii, imani inatupatia lengo letu na maana maisha. Vyote viwili hutoka kwa Mungu na hutusaidia kuishi vema kama anavyokusudia Mungu mwenyewe muumba wetu. Kwa sababu hii haviwezi kupingana isipokuwa kama mila zenyewe ni potofu. Mtume Paulo anajiweka leo kama kielelezo cha  kuitanguliza imani kama msingi wa kuzipembua mila njema za kuzifuata na zile zisizo njema za kutokuzipa nafasi.

Injili (Lk 10:1-12, 17-20) Katika injili ya dominika ya leo, Kristo anawatuma wafuasi wake kumtangulia katika kila miji alipokusudia kwenda. Idadi ya wafuasi waliotumwa inatajwa kuwa 70 na wakati mwingine 72. Hii ni namba ya kibiblia inayomaanisha idadi ya mataifa yote. Yesu kutuma idadi hiyo anamaanisha kuwa utume wa wafuasi wake ni wa kwenda katika mataifa yote. Katika kitabu cha Mwanzo 10:1:1-30 yanatajwa mataifa yote ya dunia (yaliyojulikana). Biblia ya Kihebrania inayahesabu kuwa 70 na ile ya Kigiriki (Septuaginta, LXX) inayahesabu kuwa 72. Hii ndiyo sababu kuwa katika tafsiri iliyotokana na kiebrania inataja wafuasi 70 na ile iliyotokana na kigiriki inataja wafuasi 72, ila lengo ni lilelile la kuhusisha idadi ya wafuasi wanaotumwa na idadi ya kibiblia ya mataifa ya ulimwengu.

Wanatumwa wawili wawili ili kusaidiana wawapo safarini na utumeni. Lakini pia kadiri ya Kum 19:15 ushahidi unaoaminika si wa mtu mmoja bali wawili. Yesu anawatuma akiwaambia “mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache”. Katika mazingira karibu yote, kipindi cha mavuno ni kipindi kinachohitaji kazi  ya haraka vinginevyo mazao yataharibikia shambani na kazi ya msimu wote inakuwa imepotea. Manabii katika Agano la Kale walitumia pia lugha ya mavuno kumaanisha hukumu ya siku ya mwisho inayokuja upesi (rej. Yoeli 3:13, Mik 4:11-13). Vivyo hivyo Yesu anajulisha kuwa utume anaowapa ni utume unaohitaji daima kipaumbele: kupewa nafasi ya kwanza. Ndiyo maana anawaambia wasipoteze muda njiani na wla wasijishikamanishe na vitu vinavyoweza kuwaondoa katika lengo lao la msingi ambalo ni utume. Mwisho injili inaonesha kuwa wafuasi wanaojikita katika utume wao na kushika kiaminifu maelekezo ya Bwana wao hujaliwa furaha kama zawadi na tena furaha ya kuwa majina yao yanaandikwa mbinguni.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Kanisa linao utume ulimwenguni. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unafundisha kuwa Kanisa limetumwa na Mungu kwa mataifa yote ili liwe Sakramenti ya wokovu kwa wote. Nalo kwa asili ya ukatoliki wake na kwa kulitii agizo la Kristo mwanzilishi wake, linafanya bidii ya kuitangaza injili kwa watu wote ili Neno la Mungu liendelee na kutukuzwa na Ufalme wa Mungu utangazwe na kusimikwa duniani kote (Rej. Ad Gentes 1). Hata leo hii utume wa Kanisa unahitajika na utaendelea kuhitajika mpaka Kristo atakaporudi. Habari njema inahitaji kuhubiriwa, Kristo anahitaji kushuhudiwa na sakramenti za wokovu zinahitaji kuadhimishwa kwa ajili ya wokovu wa taifa lote la Mungu. Masomo ya leo yanatualika sote kama wanakanisa kuzidi kujikita kuuendeleza utume wa Kanisa katika changamoto za nyakati. Na kwa namna ya pekee yanatualika kutambua kuwa ujenzi wa amani na uundaji wa jamii bora ni mojawapo ya maeneo ya utume wa moja kwa moja wa Kanisa.

Kama kanisa tunaalikwa leo tuzidi kujibidiisha katika kujenga misingi ya haki,amani na maridhiano kati ya watu: kuweka amani kama mojawapo ya vipaumbele vya utume wetu, kuwa wajumbe wa amani na upatanisho na kuwa mstari wa mbele kulinda amani katika jamii zetu. Tunaona pia kuwa mwendelezo wa utume wa Kanisa haupingani hata kidogo na utambulisho wa watu katika mila na tamaduni zao. Vyote kama tulivyoona katika tafakari ya masomo, vyatoka kwa Mungu na vinamhusu mtu yuleyule hivyo haviwezi kupingana. Imani humsaidia mtu kuziishi vema mila na tamaduni zake kwa kuziendeleza mila njema na kutozipa nafasi zile zinazipingana na utu kama alivoukusudia Mungu muumbaji.

Liturujia J14
05 July 2019, 16:58