Tafuta

Vatican News
Kardinali John Onaiyekan anawataka Wakristo nchini Nigeria kusimama kidete kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! Kardinali John Onaiyekan anawataka Wakristo nchini Nigeria kusimama kidete kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake!  (AFP or licensors)

Kardinali Onaiyekan: Wakristo simameni kidete kutangaza Injili

Sakramenti ya Kipaimara isaidie kuimarisha mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda, tayari kusimama kidete, kulinda, kutetea na kueneza imani yao kwa Kristo Yesu, aliyetesa, akafa na kufufuka kwa wafu. Wadumishe majadiliano ya kidini na watambue kwamba, hata wao waamini wa dini ya Kiislam wanayo haki msingi ya kuendeleza imani yao nchini Nigeria! Hii ni haki msingi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Sakramenti ya Kipaimara ni zawadi ya umoja wa Kanisa; upendo na mshikamano katika kutangaza, kushuhudia; kulinda na kutetea imani ya Kanisa. Ni zawadi inayowawezesha waamini kuwa alama ya upendo, mashuhuda na vyombo vya amani katika jamii inayowazunguka! Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara, muungano wa wabatizwa na Kanisa hufanywa kuwa mkamilifu zaidi, kwani wanatajirishwa kwa nguvu tendaji  ya Roho Mtakatifu na hivi hulazimika kwa nguvu zaidi kuineza na kuitetea imani kwa maneno na matendo, kama mashuhuda wa kweli wa Kristo Yesu. Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara waamini wanampokea Roho Mtakatifu anayewawezeshwa kufanywa wana wa Mungu; kwa kuunganishwa zaidi na nguvu za Kristo pamoja na kupata mapaji ya Roho Mtakatifu na hivyo, kuwasaidia kukamilika zaidi kama viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa.

Kwa njia hii, waamini wanajitoa sadaka na kuwa ni zawadi kwa ajili ya jirani zao! Waamini wanapopakwa mafuta ya Krisma wanapokea mhuri wa Paji la Roho Mtakatifu kutoka kwa Askofu mahalia. Huyu ni Roho wa hekima na akili; Roho wa shauri na nguvu; Roho wa elimu na ibada na ni Roho wa Uchaji Mtakatifu. Mapaji yote haya yanapaswa kukua na kuzaa matunda kwa ajili ya jirani zao. Haya ndiyo maisha yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, anayewawezesha waamini kujisadaka kwa ajili ya jirani zao kwa kuondokana na ubinafsi; ili hatimaye, kufungua njia katika maisha ya jumuiya inayopokea na kutoa. Waamini wakumbuke kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa Roho Mtakatifu kwa ajili ya jirani zao.

Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara waamini wanapokea zawadi ya amani, wanayopaswa kuwashirikisha pia majirani zao; kwa kuendeleza Injili ya upendo na mshikamano, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu katika Kristo, huku wakitakiana mema! Wakristo wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya amani, umoja na mshikamano katika udugu wa kibinadamu. Sakramenti ya Kipaimara hutolewa mara moja tu na huchapa katika roho alama ya kiroho isiyofutika ambayo ni ishara kwamba, Kristo Yesu amemtia Mkristo alama ya mhuri wa Roho wake, kwa kumvika nguvu itokayo juu, ili aweze kuwa shuhuda wake kwa kutoa harufu nzuri ya utakatifu wa maisha unaobubujika kutoka katika tunu msingi za Kiinjili.

Kardinali John Olorunfemi Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, nchini Nigeria, hivi karibuni ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya Bikira Maria Msaada wa Daima, Gwarinpa sanjari na kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa waamini waliokuwa wameandaliwa. Amewataka Wakristo walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto, tayari kusimama kidete, kulinda, kutetea na kueneza imani yao kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu! Waendeleze na kudumisha majadiliano ya kidini na waaamini wa dini ya Kiislam nchini Nigeria wakitambua kwamba, hata wao wanayo haki msingi ya kuendeleza imani ya dini yao ya Kiislam.

Hapa, hakuna sababu ya kulalama kwamba, kuna baadhi ya watu wanaotaka kuigeuza Nigeria kuwa ni nchi ya Kiislam. Ni wajibu na dhamana ya Wakristo nchini Nigeria na sehemu yoyote ile ya dunia kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu na Kanisa lake, hata kama itawabidi kuyamimina maisha yao kama ushuhuda wa imani yao. Hakuna mtu anayeweza kulazimisha wongofu wa shuruti, ikiwa kama mtu mwenyewe hakuridhia. Kwa Wakristo legelege, hawataweza kusimama imara kulinda, kutetea na kushuhudia imani yao, pale wanapokumbana na magumu pamoja na changamoto za maisha. Ikiwa kama Wakristo wataridhia kurubuniwa ili wapandishwe vyeo, wapate upendeleo na hata wakati mwingine mke na mali, ikiwa tu, watakubali kuongokea dini ya Kiislam, watambue kwamba, wanaisaliti imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Jambo la msingi kwa Wakristo ni kuendelea kusimama imara na thabiti katika imani, maadili na utu wema na kamwe wasikubali kuyumbishwa kama “daladala iliyokatika usukani” kwa mambo mpito! Wakristo wanayo fursa kubwa ya kutangaza na kushuhudia imani yao nchini Nigeria, kwa kusimama kidete: kulinda na kutetea: misingi ya haki, amani, ukweli na maridhiano kati ya watu pamoja na kutambua kwamba, Msalaba ni utambulisho wa maisha na utume wa Mkristo mahali popote pale alipo! Msalaba wa Kristo ni chemchemi ya huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Mungu kwa ajili ya walimwengu wote na wala si kidani cha kupamba shingo!

Kipaimara: Abuja
17 July 2019, 15:23