Tafuta

Vatican News
Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Singida, Tanzania inaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 30 ya huduma makini kwa maskini na watoto nchini Tanzania! Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Singida, Tanzania inaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 30 ya huduma makini kwa maskini na watoto nchini Tanzania!  (AFP or licensors)

Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar Itigi: Miaka 30 ya Huduma

Hii ni dhamana na wajibu unaopaswa kutekelezwa na kuendelezwa na viongozi wa Hospitali pamoja na wafanyakazi wote kwa kuzingatia kauli mbiu ya Hospitali: “Tibu, Fariji na Elimisha”. Askofu mkuu Nyaisonga ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na Hospitali Mtakatifu Gaspar, Itigi, ili kuhakikisha kwamba, watanzania wengi wanapata huduma bora zaidi ya afya.

Na Rodrick Minja, Benno Edward, Singida & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kumekuwepo na maendeleo makubwa sana katika huduma ya afya inayotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita. Licha ya maboresho katika sekta ya afya, bado Kanisa litaendelea kuwekeza katika huduma kwa wagonjwa, kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana na utume wake wa kinabii, kwa ajili ya maskini wapya katika sekta ya afya! Yaani: wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa sugu; magonjwa nasibu, wagonjwa wa afya ya akili, wazee na maskini wanaoteseka kupata huduma bora ya tiba. Katika mchakato huu, Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Kristo linalomiliki na kuendesha Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, iliyoko, Itigi, Manyoni, Singida nchini Tanzania katika kipindi cha Miaka 30 imejipambanua kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa huduma bora ya tiba kwa watoto wadogo, amana na utajiri wa taifa la Tanzania.

Huu ni muda muafaka wa kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini! Huu ni muda wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa wagonjwa na maskini! Ikumbukwe kwamba, utambulisho huu unapata chimbuko lake kutoka katika Injili ya huruma ya Mungu, “nilikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama”. Haya ni matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji. Hii ndiyo changamoto changamani ambayo imefanyiwa kazi na Mama Kanisa kwa kuanzisha vituo vya huduma kwa ajili ya wagonjwa na maskini, kama sehemu ya utekelezaji wake wa utume wa kinabii: kwa kusoma alama za nyakati, kusikiliza na hatimaye, kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii mintarafu mwanga wa Injili.

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga,  wa Jimbo kuu la Mbeya, Tanzania, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar ameyataka Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Tanzania kuhakikisha kwamba, yanaenzi kwa vitendo, ndoto za waasisi wa Mashirika yao sanjari na kuendelea kusoma alama za nyakati! Yale mambo mazuri na matakatifu yaliyoanzishwa na waasisi wa Mashirika yao, wayaendeleze kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Kwa namna ya pekee kabisa, Askofu mkuu Nyaisonga amewataka Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu kujipambua na kuwa tayari kupeperusha bendera ya Mtakatifu Gaspar aliyekuwa na upendeleo wa pekee kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii.

Hii ni dhamana na wajibu unaopaswa kutekelezwa na kuendelezwa na viongozi wa Hospitali pamoja na wafanyakazi wote kwa kuzingatia kauli mbiu ya Hospitali: “Tibu, Fariji na Elimisha”. Askofu mkuu Nyaisonga ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuwa bega kwa bega na Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, ili kuhakikisha kwamba, watanzania wengi wanapata huduma bora zaidi ya afya. Amewasihi watanzania kuendelea kupata huduma bora kutoka hospitalini hapo, kwa kuchangia mawazo yatakayoboresha zaidi huduma inayotolewa pamoja na kuwa macho na wajanja wachache wanaoweza kuwa na nia mbaya ya kuihujumu Hospitali hii. Wafanyakazi waendelee kutoa huduma bila ya upendeo wowote ule, kwa kuwapenda na kuwahudumia wagonjwa wote kwa ari, upendo na moyo mkuu!

Kwa upande wake, Bwana Roberto Mengoni, Balozi wa Italia nchini Tanzania amelishauri Kanisa kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania pamoja na kukuza umoja na mshikamano na Serikali ya Italia ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa ustawi, maendeleo na ubora wa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar Itigi, kwa rasilimali fedha, vifaa na nguvu kazi.  Kilele cha maadhimisho ya Miaka 30 ya utume wa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi kilipambwa kwa uwepo wa Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida, Madaktari na wawakilishi wa uongozi wa Bambino Gesù kutoka Roma, Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu kutoka Italia pamoja na baadhi ya Madaktari wakuu waliohudumia Hospitali hii kwa nyakati mbali mbali, bila kumsahau Dr. Majura Timoth Kaare.

Katika mahojiano maalum na Vatican News, Padre Serafini Lesiriamu, C.PP.S., Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, amegusia kuhusu dira na dhima ya Hospitali hii inayofuata na kuzingatia kanuni, sheria, taratibu na Mafundisho ya Kanisa Katoliki katika sekta ya huduma ya afya, ili kuzima kiu na matamanio halali ya wagonjwa. Kauli mbiu ya Hospitali ni “Tibu, Fariji na Elimisha” pamoja na kufanya tafiti za kina makini ili kutoa huduma bora zaidi. Hii ni huduma inayozingatia misingi ya haki, usawa na haki msingi za binadamu kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Padre Lesiriamu ana mshukuru na kumpongeza Mama Mariella Enoc, Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican aliyetembelea hivi karibuni, Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, ili kujionea mwenyewe ushuhuda wa Injili ya maisha, huruma na upendo inavyomwilishwa  na Hospitali hii huko Itigi, Kanda ya Kati nchini Tanzania.

Hospitali ya Bambino Gesù itaendelea kushirikiana na kushikamana na Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar kwa kuzingatia kanuni auni katika kutoa huduma za kibingwa kwa magonjwa ya watoto; mafunzo ya kibingwa kwa Madaktari watanzania na tayari Padre na Daktari Oscar Siogopi, C.PP.S. yuko Hospitali ya Bambino kwa mafunzo kazini. Kwa pamoja wataendeleza huduma kwa njia ya mtandao ili kuwa na uhakika wa uchunguzi wa magonjwa ili hatimaye, wagonjwa waweze kupata tiba muafaka. Wataendelea kushirikiana katika huduma kwa tiba ya magonjwa ya watoto, lengo ni kuhakikisha kwamba, huduma hii inaboreshwa hata kwa watoto maskini. Padre Serafini Lesiriamu, C.PP.S. anakaza kusema, Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar ina jumla ya vitanda 320 na kati ya vitanda hivi kuna vitanda 150 kwa ajili ya watoto peke yao ambao pia wana chumba maalum cha upasuaji.

Lengo ni kujenga na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Changamoto kwa afya ya mama na mtoto ni kubwa katika Nchi Zinazoendelea Duniani. Watoto wengi wanafariki dunia kutokana na kukosa huduma bora za afya: kinga na tiba; umbali, gharama hata pengine na ubora wa huduma zinazotolewa. Ndiyo maana Hospitali ikasoma alama za nyakati na kuanza kuwekeza zaidi kwa ajili ya huduma bora na makini kwa watoto. Padre Serafini Lesiriamu, C.PP.S anasema, ushauri wake kwa wafanyakazi katika sekta ya afya ni kwamba, watambue kuwa wao ni vyombo na mashuhuda wa huruma, upendo na Injili ya uhai. Mikononi mwao wanabeba hazina na amana kubwa ambayo ni maisha ya binadamu, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wanapaswa kuilinda, kuitetea na kudumisha.

Padre Lesiriamu anapowashukuru wafanyakazi wote katika sekta ya afya, anapenda pia kuwatia shime ili waendelee kuwapenda, kuwafariji, kuwahudumia, kuwaelimisha kwa ari na moyo mkuu, bila upendeleo wala rushwa. Watambue kwamba, iko siku Mwenyezi Mungu atajibu sadaka na majitoleo yao! Anasema, gharama kubwa ya matibabu kwa watanzania maskini ni changamoto pevu. Anawashauri watanzania kujenga utamaduni wa kujiunga na huduma ya bima ya afya ili kuwa na uhakika wa matibabu yao. Hili ni kimbilio la wanyonge na maskini. Watanzania wajenge na kudumisha utamaduni wa kujali, kupima na kutibu afya. Uhaba wa madaktari na gharama kubwa ya vifaa tiba ni changamoto changamani. Ni matumaini ya Padre Lesiriamu kwamba, juhudi za Tanzania za kutaka kuimarisha uchumi wa kati siku moja zitazaa matunda. Jambo la msingi ni watanzania na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuunga mkono juhudi hizi.

Hospitali ya Itigi
10 July 2019, 16:48