Tafuta

Vatican News
Jubilei ya Miaka 50 ya Utume wa Walei Tanzania: Benki ya Biashara ya Mkombozi ni matunda ya ushiriki mkamilifu wa waamini walei katika ukombozi wa watanzania kiuchumi! Jubilei ya Miaka 50 ya Utume wa Walei Tanzania: Benki ya Biashara ya Mkombozi ni matunda ya ushiriki mkamilifu wa waamini walei katika ukombozi wa watanzania kiuchumi!  (AFP or licensors)

Jubilei ya Miaka 50 Utume wa Walei Tanzania: Benki ya Mkombozi

Benki ya Mkombozi ni tunda na juhudi za Kanisa Katoliki nchini Tanzania kumwinua mtanzania mwenye kipato cha chini kwa kumwezesha kwa njia ya mikopo inayopania kumjengea uwezo kiuchumi. Lengo hili litaweza kufikiwa ikiwa kama kasi ya kupanuka kwa Benki ya Mkombozi sehemu mbali mbali za Tanzania. Haya pia ni matunda ya utume wa walei nchini Tanzania!

Na Rodrick Minja- Dodoma & Padre Richard A. Mjigwa, Vatican.

Benki ya Biashara ya Mkombozi ambayo ni tunda na juhudi za Kanisa Katoliki nchini Tanzania inalenga kumwinua mtanzania mwenye kipato cha chini kwa kumwezesha kwa njia ya mikopo inayopania kumjengea uwezo kiuchumi. Lengo hili litaweza kufikiwa ikiwa kama kasi ya kupanuka kwa Benki ya Mkombozi sehemu mbali mbali za Tanzania itandelea kama inavyojionesha kwa sasa. Haya pia ni mafanikio makubwa ya utume wa walei nchini Tanzania katika mchakato wa kulitegemeza Kanisa la Tanzania kwa rasilimali fedha!

Ni Benki inayojali na kuzingatia: weledi, maadili ya kazi, uwajibikaji, nidhamu na uaminifu, daima wafanyakazi wake wakihamasishwa kuchapa kazi kwa ajili ya: ustawi, mafao na maendeleo ya Tanzania katika ujumla wake! Benki ya Mkombozi imeendelea kuwa mdau muhimu wa maendeleo kwa kuunga mkono utekelezaji wa malengo ya taifa kwa kuwafikishia wananchi huduma za kifedha. Benki inaendelea kushirikiana na viongozi wa Serikali za mitaa na wajasiriamali wenyewe, jambo linalorahisisha upatikanaji wa mikopo na mitaji kwa vikundi mbali mbali.

Benki ya Mkombozi ambayo hapo tarehe 27 Agosti 2019 itakuwa ikiadhimisha miaka 10 tangu ianzishwe, hivi karibuni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu amezindua rasmi tawi jipya Jijini Dodoma, ili kuendelea kusogeza huduma ya Benki hii kwa wananchi wa Dodoma. Makamu wa Rais amesifia utaratibu wa kikundi kujidhamini chenyewe kupata mikopo utasaidia vikundi vingi kuchukua mkopo na hivyo kuongeza idadi ya wateja, kukuza zaidi mtaji wa Benki ya Mkombozi na hatimaye kufanikisha mzunguko wa fedha katika uchumi.

Lengo la Serikali ya Tanzania ni kufikia kipato cha kati, ifikapo mwaka 2025. Ili kufikia huko, wananchi hawana budi kuwezeshwa kiuchumi ili kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na huduma, ili kujipatia kipato wao wenyewe pamoja na serikali katika ujumla wake. Bado kuna changamoto ya kuwashawishi watanzania kutumia huduma za Kibenki, hivyo ameitaka Benki ya Biashara ya Mkombozi pamoja na Benki nyinginezo kuongeza juhudi za kuragibisha huduma za kibenki pamoja na kusoma alama za nyakati kwa njia ya tafiti makini, ili kuwavutia wateja wengi zaidi.

Takwimu za Benki ya Biashara ya Mkombozi zinaonesha kwamba, kiasi cha watu 33, 500 wamekopeshwa kiasi cha shilingi bilioni 2.27. Benki imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 3 kwa wakulima zaidi ya 500. Mikopo inaendelea kuwajengea watanzania uwezo wa kiuchumi sanjari na kukuza pato la taifa kwa kupitia kodi mbali mbali zinazolipwa. Watanzania wanahamasishwa kutumia huduma za Benki, ili kuwa na uhakika wa usalama wa fedha zaidi na kuondokana na hifadhi ya fedha zilizopitwa na wakati! Huu ni wakati wa kuambata mabadiliko ili kwenda na wakati!

Benki ya Biashara ya Mkombozi inatakiwa kuendelea kujikita katika mchakato wa ubunifu, kwa kuobresha huduma na kamwe wasibweteke na mafanikio yanayoendelea kujionesha kwa wakati huu. Watambue kwamba, kuna ushindani mkubwa wa huduma za kibenki, changamoto iwe ni kuboresha huduma, ili kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi na hasa wale wa kipato cha chini! Benki ya Biashara ya Mkombozi iendelee kukuza na kudumisha kanuni, sheria, taratibu na maadili ya kibenki, ili kamwe wasitumbukie katika kashfa ya kutakatisha fedha, hali ambayo itaifedhehesha sana Benki hii.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu, ameitaka Benki ya Mkombozi kuhimiza matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya mtandao ili kuokoa rasilimali muda, gharama pamoja na kuimarisha usalama wa fedha za wateja. Itakumbukwa kwamba, uzinduzi wa majengo ya Benki ya Biashara ya Mkombozi, Tawi la Dodoma ulifanywa na Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma, tarehe 11 Machi 2019, katika sherehe iliyohudhuriwa na viongozi mbali mbali wa serikali,  kidini na vyama vya kisiasa! Walikuwepo pia wafanyabiashara na wadau na wateja wa Benki ya Biashara ya Mkombozi.

Benki ya Mkombozi
22 June 2019, 16:10