Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Gervas Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya kwa niaba ya Maaskofu wakuu wenzake, anamshukuru Mungu, Baba Mtakatifu na waandamizi wake, kwa kuwateua katika utume huu. Askofu mkuu Gervas Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya kwa niaba ya Maaskofu wakuu wenzake, anamshukuru Mungu, Baba Mtakatifu na waandamizi wake, kwa kuwateua katika utume huu.  (ANSA)

Askofu mkuu Gervas Nyaisonga: Shukrani za Maaskofu wakuu! Sala!

Maaskofu wakuu wanasema, wameupokea utume huu kwa moyo wa unyenyekevu mkubwa. Wanatambua kwamba, nguvu na jeuri yao kubwa ni waamini wanaotumwa kuwatangazia Habari Njema, kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na upendo, aliyewateua katika nafasi hii kama Maaskofu wakuu, aguse pia roho na nyoyo za waamini wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga,  wa Jimbo kuu la Mbeya, Tanzania, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, katika mahojiano maalum na Vatican News; kwa niaba ya Maaskofu wakuu 31 na kwa namna ya pekee Maaskofu wakuu kutoka Afrika anapenda kutoa shukrani zake za dhati kwa Mwenyezi Mungu, Baba Mtakatifu Francisko pamoja na waandamizi wake kwa kuwaamini na kuwateua kushiriki shughuli za kichungaji kwenye Majimbo makuu sehemu mbali mbali duniani. Maaskofu wakuu wanamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ndiye wanayemtumikia kwa njia ya Mama Kanisa chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na waandamizi wake.

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga anatambua na kukiri kwamba, kazi, dhamana, majukumu na utume huu ni mkubwa, mzito na mgumu na kwamba, hawawezi kujidai kwamba wanaweza kutekeleza yote kwa nguvu zao wenyewe! Lakini wanachojitahidi kujaribu ni kufanya vizuri wito na utume wao, huku wakimpenda Mwenyezi Mungu kwa njia ya huduma makini kwa watu wake. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, ndiye anayewawezesha kutenda yote anayotaka yatendeke. Maaskofu wakuu wanasema, wameupokea utume huu kwa moyo wa unyenyekevu mkubwa. Wanatambua kwamba, nguvu na jeuri yao kubwa ni waamini wanaotumwa kuwatangazia Habari Njema, kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza.

Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na upendo, aliyewateua  katika nafasi hii kama Maaskofu wakuu, aguse pia roho na nyoyo za waamini wa Majimbo haya makuu pamoja na majimbo yote ya kanda watakazozihudumia. Kwa njia ya umoja, upendo na mshikamano wa dhati, hakuna jambo lolote linaloweza kushindikana. Kwa njia hii, Kristo Yesu atatangazwa na kushuhudiwa sehemu mbali mbali za dunia na Ufalme wa Mungu unasimikwa katika misingi ya haki, amani, umoja na upendo utajengeka na kushamiri kama “Mtende wa Lebanon”. Maaskofu wakuu wapya wanao nia njema na sababu msingi za kutekeleza wito, dhamana na utume wao, lakini wanaomba neema ya Mwenyezi Mungu iwaguse wote ili washikamane na kazi ya Mungu iweze kutendeka kwa ufasaha zaidi.

Kwa mara nyingine tena, Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga kwa niaba ya Maaskofu wakuu waliopewa Pallio takatifu, Jumamosi, tarehe 29 Juni 2019 wanamshukuru Baba Mtakatifu Francisko pamoja na waandamizi wake, wanaomba kusindikizwa kwa sala na sadaka za watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili watekeleze vyema utume wao! Itakumbukwa kwamba, wafuatao ni majina ya Maaskofu wakuu kutoka Barani Afrika walioteuliwa katika kipindi cha Mwaka 2018- 2019. Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga,  wa Jimbo kuu la Mbeya, Tanzania, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania; Askofu mkuu Philip Arnold Subira Anyolo wa Jimbo kuu la Kisumu, Kenya ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya.

Wengine katika orodha hii ni: Askofu mkuu Zeferino Zeca Martins, S.V.D. wa Jimbo kuu la Huambo, Angola, Askofu mkuu Fridolin Ambongo Besungu, O.F.M. Cap. wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC., Askofu mkuu Antoine Kambanda wa Jimbo kuu la Kigali, Rwanda, Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, Askofu mkuu John Bonaventure Kwofie wa Jimbo kuu la Accra, Ghana.

Askofu Gervas: Pollo
30 June 2019, 15:54