Tafuta

Vatican News
Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga anawataka waamini kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Roho Mtakatifu katika kukuza na kudumisha lugha ya upendo, maadili na utu wema! Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga anawataka waamini kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Roho Mtakatifu katika kukuza na kudumisha lugha ya upendo, maadili na utu wema!  (Vatican Media)

Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga: Wakristo dumisheni lugha ya upendo!

Askofu Mkuu Nyaisonga amewataka waamini walioimarishwa kwa karama za Roho Mtakatifu, kuwa ni chachu ya utakatifu wa maisha na matendo adili, kwa kuanzia katika familia zao. Itakumbukwa kwamba, familia ya Mungu nchini Tanzania, kwa mwaka 2019, inaadhimisha Mwaka wa Familia unaongozwa na kauli mbiu “Familia kama Kanisa la nyumbani na Shule ya Imani na Maadili”.

Na Thompson Mpanji, Mbeya & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Mtakatifu Barnaba Mtume, 11 Juni 2019, amekazia umuhimu wa kudumisha moyo wa sadaka na majitoleo kwa kuambatana na Mwenyezi Mungu. Pili, neema na baraka ziwasaidie waamini kuboresha maisha yao ya kiroho na wala wasiwe ni watu wanaoelemewa na uchu wa fedha na mali. Waamini wanakumbushwa kwamba, wamepewa bure, watoe bure kama sadaka safi! Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujenga mazoea na utamaduni wa kusoma, kulitafakari na hatimaye kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yao.

Kwa njia hii, Neno la Mungu linakuwa ni chemchemi ya wema, furaha, amani, upole, huruma na hali ya kujiamini. Huu ndio mtindo wa maisha unaojinyenyekesha mbele ya Roho Mtakatifu, ili kulipokea Neno la Mungu na kulimwilisha ili liweze kuzaa matunda ya: huruma, wema, amani na mapendo, tunu msingi katika maisha ya Kikristo! Mitume waliposikia kwamba, Habari Njema ya Wokovu ilikuwa inazidi kuenea kwa kasi, walishikwa na hofu kidogo, lakini mkono wa Bwana ulikuwa pamoja nao, kiasi kwamba, watu wengi wakaamini na kumwongokea Mungu.

Wanafunzi wa Antiokia wakawa wa kwanza kuitwa Wakristo! Mtume Barnaba alitumwa kushuhudia hayo yaliyokuwa yanasemwa, alipoiona neema ya Mungu, akafurahi na kuwataka wote kuambatana na Mwenyezi Mungu katika maisha yao, kwani walikuwa kweli ni watu wema waliojaa Roho Mtakatifu na imani. Hii ni changamoto kwa waamini kumpokea Roho Mtakatifu ili aweze kuwakumbusha na kuwafundisha yote yaliyosemwa na kutendwa na Kristo Yesu! Barnaba alikuwa ni kati ya mashuhuda waliotumwa kuhudhuria kwenye Mtaguso wa kwanza wa Yerusalemu.

Habari kutoka Mbeya, Tanzania zinasema, Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Barnaba, Mtume, ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa waamini 88, katika Kanisa kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua. Katika mahubiri yake, amewataka waamini walioimarishwa kwa mapaji na karama za Roho Mtakatifu, kuwa ni kielelezo na chachu ya utakatifu wa maisha na matendo adili, kwa kuanzia katika familia zao. Itakumbukwa kwamba, familia ya Mungu nchini Tanzania, kwa mwaka 2019, inaadhimisha Mwaka wa Familia unaongozwa na kauli mbiu “Familia kama Kanisa la nyumbani na Shule ya Imani na Maadili”.

Katika maadhimisho haya kuna baadhi ya wanandoa ambao wamemshukuru Mungu kwa kuadhimisha pia Jubilei ya Miaka 25 ya Ndoa. Huu ni mwaliko kwa wanandoa wachanga, kuiga mifano bora ya wanandoa waliowatangulia! Wajifunze kusaidiana, kuongozana katika maisha; kutakatifuzana, kuchukuliana na kusameheana bure katika maisha, ili siku moja waweze kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25, Miaka 50 na wale watakaoweza, miaka 75 ya maisha ya ndoa na familia!

Askofu mkuu Gervas Nyaisonga anakaza kusema, tunu hizi msingi zinapaswa kumwilishwa na kushuhudiwa katika jamii na taifa katika ujumla wake, kama chachu ya kuyatakatifuza malimwengu, hasa wakati huu wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Halmashauri ya Walei nchini Tanzania. Amewataka waamini wa Jimbo kuu la Mbeya kuwa ni mashuhuda na vyombo vya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima:kiroho na kimwili. Amewataka waamini kukuza na kudumisha karama na mapaji waliyokirimiwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Mungu ndani na nje ya Jimbo kuu la Mbeya.

Askofu mkuu Gervas Nyaisonga,  amewataka waamini kufundisha kwa maneno na kutoa nafasi kwa matendo yao adili yaweze kuzungumza na kuwagusa watu. Roho Mtakatifu awawezeshe waamini kuzungumza kwa lugha mbali mbali zinazoeleweka na kuwaunganisha watu. Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.  Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.  Waamini wakiishi kwa Roho na waenende kwa Roho. (Rej. Wagalatia 5: 18-23). Askofu mkuu Gervas Nyaisonga amesema, Roho Mtakatifu awawezeshe waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati.

Wakristo walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara watambue kwamba, wamefanywa kuwa waana wa Mungu; wameunganishwa kwa nguvu zaidi na Kristo Yesu; wamekirimiwa vipaji vya Roho Mtakatifu kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Waamini watambue kwamba, wamepewa nguvu na sasa wanapaswa kutoka kifua mbele kutangaza, kushuhudia na kutetea imani kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, wakiwa tayari kukiri kwa ushujaa jina la Kristo na utukufu wa Fumbo la Msalaba. Wakristo walioimarishwa wamepokea mhuri wa kiroho; roho wa hekima na akili, roho wa shauri na nguvu, roho wa elimu na ibada, roho wa uchaji Mtakatifu; changamoto na mwaliko wa kulinda mapaji haya, kwani Mwenyezi Mungu amewatia alama na kuwajaza amana ya Roho wake, nyoyoni mwao!

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisongaa mbaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., amekazia umuhimu wa uekumene wa sala, kwa kumkumbuka na kumwombea Marehemu Mariam Nicodem Cheyo, mke wa Askofu Alinikisa Cheyo wa Kanisa la Moravian, Jimbo la Kusini Magharibi aliyefariki dunia hivi karibuni kwenye Hospitali ya Ocean Road, Jijini Dar es Salaam.

Jimbo Kuu la Mbeya
12 June 2019, 10:09