Tafuta

Jubilei ya Miaka 300 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle: Huduma ya elimu kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Jubilei ya Miaka 300 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle: Huduma ya elimu kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. 

Watawa Shule za Kikristo, FSC: Shule ni chombo cha ukombozi

Mwaka wa Jubilei ya miaka 300 imekuwa ni fursa ya kumwangalia tena na tena Kristo Yesu kama dira ya maisha, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini, kwa kutangaza Habari Njema kwa njia ya elimu inayomwambata mtu mzima: kiroho na kimwili. Kwa maongozi ya Roho Mtakatifu wamefanikiwa kupyaisha ari yao kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo, FSC, linaadhimisha Jubilei ya Miaka 300 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle. Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua dhamana na mchango wa Watawa hawa akautangaza Mwaka 2019 kuwa ni mwaka wa Jubilei ya Watawa wa Shule za Kikristo. Huu ni mwaliko wa kujenga utamaduni wa watu kukutana, ili kuwashirikisha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, amana na utajiri wa Habari Njema ya Wokovu!

Mwaka huu wa Jubilei ya miaka 300 imekuwa ni fursa ya kumwangalia tena na tena Kristo Yesu kama dira ya maisha, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini, kwa kutangaza Habari Njema kwa njia ya elimu inayomwambata mtu mzima: kiroho na kimwili. Kwa mfano wa maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle pamoja na maongozi ya Roho Mtakatifu, wamefanikiwa kupyaisha ari yao kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa kugundua pia njia mpya za maisha na utume wao! Hii ni sehemu ya hotuba elekezi iliyotolewa na Bruda Robert Schieler, Mkuu wa Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo walipokutana na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 16 Mei 2019 mjini Vatican.

Watawa hawa wanasema, wako huru, kuvuka mipaka inayotenganisha nchi hata mipaka ya kijamii na kisiasa. Wamekuwa ni watangazaji na mashuhuda wa maisha ya wakfu kwa njia ya elimu inayokomboa; kwa kuwaendea wale walioko pembezoni mwa jamii; waliosahauliwa na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, ili wote hawa waweze kushiriki furaha ya Injili na matumaini kwa wale waliokata tamaa! Bruda Robert Schieler anasema, wanaendelea kufuata nyayo za muasisi wao wa kuambatana na maskini kwa ajili ya maskini kama sehemu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaotekelezwa kwa njia ya elimu makini.

Katika utekelezaji wa huduma hii kwa watu wa Mungu, watawa hawa wanaendelea kushirikiana na watu mbali mbali wanaojisadaka kwa ukarimu na weledi ili kutekeleza utume huu katika sekta ya elimu. Ni watu wanaoshiriki pia amana na utajiri wa maisha ya kiroho, daima Kristo Yesu akipewa kipaumbele cha kwanza. Kwa njia hii, wanaendelea kuandika ukurasa mpya wa simulizi ya Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle. Wanaitwa na Kanisa pamoja na kusukumwa na tunu msingi za Kiinjili kugusa akili na nyoyo za watu, ili kuwaonjesha upendo hai wa Kristo Yesu kwa kuimarisha mafungamano kati ya mwalimu na mwanafunzi, ili kweli darasa liweze kuwa ni mahali pa ukombozi wa watu wa Mungu.

Hii ni tasaufi inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu; huduma makini kwa jirani na mshikamano na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, bila kuwasahau vijana wa kizazi kipya wanaohitaji msaada wao. Lengo ni kutangaza na kushuhudia uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Uwepo wao katika sekta ya elimu ni kama Sakramenti ya ufunuo wa Mungu, mahali pa kukutana na Kristo Mfufuka kwa kuendelea kusoma alama za nyakati. Watawa hawa wanasukumwa kujibu kilio cha watu ambao utu, heshima na haki zao msingi zinasiginwa.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, kwa njia ya elimu wanaweza kuinuka na kusonga mbele kama watoto wa Mungu. Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo, FSC, limehakikishia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wataendelea kuwa waaminifu kwa Roho Mtakatifu na Kanisa kwa kudumisha karama hii ndani ya Kanisa.

Shule za Kikristo 300
16 May 2019, 16:13