Cerca

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili V ya Kipindi cha Pasaka: Upendo kwa Mungu na jirani! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili V ya Kipindi cha Pasaka: Upendo kwa Mungu na Jirani! 

Tafakari Neno la Mungu Jumapili V ya Pasaka: Amri ya Upendo

Upendo kwa Mungu na jirani ndiyo amri kuu inayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha kama kielelezo cha imani tendaji! Kristo Yesu anawataka wafuasi wake kuwa na upendo kiasi cha kujisadaka na kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa jirani zao kama alivyofanya kwa kuyamimina maisha yake juu ya Msalaba ili iwe ni fidia ya wengi!

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. - Dodoma

Katika sura ya 13 ya Injili ya Yohane tunaona mwanzo wa hotuba ya Yesu akiagana na wanafunzi wake. Tunapata habari juu ya ufunuo wa mwisho wa Yesu kwa wafuasi. Biblia inatuambia kuwa alama pekee ya uwepo wa ufalme wa Mungu ni upendo. Hii ndiyo amri mpya. Kadiri ya Yesu ni kwamba tunatakiwa tupendane sisi kwa sisi kama alivyotupenda sisi. Kiini cha sheria hii ni mapendo kwa Mungu na mapendo kwa jirani kama tunavyosoma katika Mt. 22:33-40. Mtakatifu Inyasi wa Antiokia anasema ‘ye yote kati yenu asiwe na hali ya kawaida tu kwa jirani yake isipokuwa muendelee kupendana ninyi kwa ninyi katika Yesu Kristo’. Naye Mt. Katharina Laboure anasema ‘ mmoja lazima amwone Mungu katika kila mmoja’.

Mwandishi Eugene H. Maly katika kitabu ‘THE WORD ALIVE’ anaandika hivi anapotakafakari Neno la Mungu dominika ya V ya Kipindi cha Pasaka. Anasema dhana ya uwepo wa Mungu kati ya watu wake kwa taifa la Israeli ipo tangu zamani. Tangu taifa la Israeli kuanzishwa pale mlimani Sinai watu hao walielewa hivyo. Sanduku la agano lilitambulika kama mahali ambapo Mungu anakaa na ilikuwa alama ya uwepo wa Mungu kati yao – 1Sam. 4:4 – ndipo wakawatuma watu Shilo kulileta sanduku la agano la Bwana wa majeshi akaaye juu ya Makerubi ..... Baada ya Daudi kuteka mji wa Yerusalemu akawa na mpango wa kwanza wa kumjengea Bwana nyumba – 2Sam. 7:2 – tazama, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, na sanduku la Bwana linakaa katika hema...... ili Mungu akae na watu  wake. Wazo hili au namna ya kuelewa juu ya uwepo wa Mungu kati ya watu lilirekebishwa na mwandishi wa kitabu cha Kumbukumbu la Torati.

Katika Kitabu cha Kumb. 12:11 tunasoma – mahali palipochaguliwa na Bwana Mungu wenu aweke jina lake, ndipo mtakapoleta yote niliyoaamuru, yaani sadaka zenu za kuteketezwa nazo sadaka nyingine, zaka zenu, zawadi za mikono yenu na vitu vyote vizuri mlivyomwahidia kumpa Bwana kwa nadhiri. Maana mpya hapa ni kwamba kuna badiliko la hekalu kuwa kama boksi ambalo Mungu amefungiwa ndani yake na ikieleweka sasa kwamba mahali ambapo jina la Bwana hukaa. Mwinjili Yoh. 1:4 anaboresha uelewa huu akiandika – ndani yake ulikuwamo uzima, na uzima ulikuwa ni mwanga wa wanadamu. Hivyo uwepo wa Mungu kati ya watu kadiri ya Mwinjili Yohani ukieleweka sasa kuwa ndani ya Kristo, katika hali ya mwili.

Kwa hiyo tangu Yesu kurudi kwa Baba, uwepo wake hapa duniani upo katika namna mbalimbali kama katika: Neno lake linaposomwa, wawili au watatu wanapokutanika kwa jina lake na zaidi sana katika Sakramenti ya Ekaristi. Mwandishi wa kitabu cha Ufunuo anaongea uwepo wa Mungu akifikiria hali ya mwisho – Mungu atakapofuta machozi yetu na kuweka mwisho wa mauti na kilio. Sisi sasa tuko katika dunia ya sasa. Hivyo wajibu wetu ni kushuhudia uwepo wa Kristo (Mungu) wakati wetu huu na tunaona hili katika somo la kwanza na la injili. Na ndicho Mtume Paulo na Barnaba wanachofanya katika Somo la pili – walienda huku na huko wakihimiza waamini wabaki imara katika imani.

Katika Injili tunaona kuwa kuna namna mpya ya kushuhudia uwepo wake. Yesu anatupa amri mpya – Yoh. 13:34-35 na hapa Yesu anatualika tupendane ili Yesu awepo kati yetu na watu wote watawatambua kuwa wafuasi wangu, mkipendana. Katika – 1Yoh. 4:11-12 tunasoma, wapendwa, kama Mungu ametupenda hivyo, imetupasa nasi kupendana. Hakuna aliyemwona Mungu. Lakini tukipendana, Mungu anakaa ndani yetu. Na upendo wake umekamilika ndani yetu. Padre Raniero Cantalamessa anaeleza neno upya akisema laweza kuwa na maana nyingi. Katika mojawapo ya maelezo yake anasema pengine tunachangamkia neno upya kwa sababu linatoa nafasi ya matumaini, mshangao, ndoto, mwanga mpya n.k.

Hakika furaha ni tunda lake. Anasema neno upya ni kinyume cha uzee (old) lakini si kinyume cha ukale/zamani (ancient) – Law. 19:18 .... umpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe. Ndimi Bwana. Na katika 1Yoh. 2:7-8... wapendwa, siwaandikieni amri mpya, ila amri ya zamani mliyokuwa nayo tangu mwanzo. Hiyo amri ya zamani ni neno mlilolisikia. Aidha ni amri mpya ninayowaandikieni, nayo ni kweli, imedhihirika ndani yake na ndani yenu, giza linatoweka, na mwanga wa kweli umeanza kung’aa. Hii ni amri ya zamani lakini kwake Kristo anaipa roho ya kimungu ili iwezekane kutendeka. Bila hii roho mpya amri hii ingebaki katika uzee wake, iliyochakaa.

Sheria ilitamka wajibu wa kupenda lakini haikutoa nguvu ya kufanya hivyo yaani tendo la kupenda liwezekane. Haikuliwezesha pendo kufanyika. Ndiyo hapa neema ilihitajika. Kwa kifo chake msalabani ametupatia roho ya kuweza kupenda na kupendana. Amri ya Bwana ni mpya kwa maana inahuisha, inafanya upya na upendo huo hutufanya wapya na warithi wa Agano jipya na waimbaji wa wimbo mpya kama asemavyo Mtakatifu Agostino. Kwa sababu hiyo Mtume Paulo katika somo la pili  anaweza kusema tazama wafanya yote mapya. Sisi waamini tunadaiwa upendo katika matendo mema ili kushuhudia huo uwepo wa Kristo.

Padre Munachi mhubiri maarufu anaandika huu mfano akielezea somo la leo; mchoraji maarufu Paul Gustave Dore alipoteza hati yake ya kusafiria huko nchi za Ulaya. Alipofika mpakani akamweleza askari kilichompata. Akataja jina lake akiamini kuwa askari atamtambua mara na kumruhusu aendelee na safari yake. Askari akasita akisema kuwa watu wengi hufanya hivyo wakidai kuwa ndo mtu mwenyewe au mhusika mwenye umaarufu huo. Dore alisisitiza kuwa ndiye mwenyewe. Askari akamwambia atampatia jaribio la kuchora. Akampatia penseli na karatasi achore kwa haraka picha za baadhi ya watu waliokuwepo pale. Dore alifanya zoezi hilo kwa haraka kabisa na kwa ujuzi mkubwa kwamba askari alijiridhisha kuwa ndiye Dore mchoraji maarufu. Akamrushu kuendelea na safari yake. Matendo yalimdhihirisha kuwa ndiye.

Anaendelea kutoa mfano mwingine. Mahatma Ghandi aliulizwa mawazo yake kuhusu ukristo. Akasema kuwa “ninauheshimu sana ukristo”. Mara kwa mara nimesoma hotuba ya mlimani, mutasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu, (Mt. 5:1..) na nimefaidika sana na hotuba hii. Sijawahi kumfahamu ye yote aliyetenda mema zaidi au kama mtu huyu Yesu Kristo. Hakika hakuna lo lote baya katika ukristo ila shida iko kwenu ninyi wakristo sababu hamuishi katika matendo hayo mnayofundisha. Upendo katika matendo mema ni uthibitisho wa ukristo wetu hivyo maneno, mawazo na matendo yetu hayana budi kulandana. Mtakatifu Francisko wa Assisi anasema ‘daima tangaza Injili muda wote kwa matendo na tumia maneno ikihitajika’. Tumsifu Yesu Kristo.

15 May 2019, 17:09