Tafuta

Vatican News
Marehemu Askofu Gabriel Mmole, alikuwa ni tegemeo kubwa kwa maisha na utume wa Kanisa nchini Tanzania. Marehemu Askofu Gabriel Mmole, alikuwa ni tegemeo kubwa kwa maisha na utume wa Kanisa nchini Tanzania. 

Marehemu Askofu Mstaafu Gabriel Mmole alikuwa nguzo ya Kanisa!

Kanuni ya imani huhitimishwa na tangazo la ufufuko wa wafu siku ya mwisho na katika uzima wa milele. Kanisa lina matumaini kwamba, kama vile Kristo alivyofufuka kweli kutoka kwa wafu na anaishi daima, vivyo hivyo wenye haki, baada ya kifo chao, wataishi daima na Kristo Mfufuka, anaye atawafufua siku ya mwisho; kazi ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anafundisha na kuungama katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na katika tendo lake la uumbaji, la wokovu na lenye kutakasa. Kanuni ya imani huhitimishwa na tangazo la ufufuko wa wafu siku ya mwisho na katika uzima wa milele. Kanisa lina matumaini kwamba, kama vile Kristo alivyofufuka kweli kutoka kwa wafu na anaishi daima, vivyo hivyo wenye haki, baada ya kifo chao, wataishi daima na Kristo Mfufuka, ambaye atawafufua siku ya mwisho; kazi ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Askofu mkuu Damian Denis Dallu wa Jimbo kuu la Songea, Tanzania, Jumanne, tarehe 21 Mei 2019 ameongoza Ibada ya Mazishi ya Askofu mstaafu Gabriel Mmole wa Jimbo Katoliki Mtwara, alifariki dunia tarehe 15 Mei 2019. Askofu mkuu Dallu ameitaka familia ya Mungu nchini Tanzania kuishi katika misingi ya maadili na utu wema, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja licha ya tofauti zao msingi.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika salam za rambi rambi kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, amemmkumbuka Marehemu Askofu Gabriel Mmole ambaye katika maisha na utume wake, amekuwa ni kielelezo cha dhamira njema. Baraza la Maaskofu lilitegemea hekima na busara yake ya kichungaji.  Ni kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa, kumbe, ni wajibu wa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumuenzi kwa kumwombea ili aweze kupumzika katika usingizi wa amani na hatimaye, aweze kupata maisha ya uzima wa milele!

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania wote kumuenzi Marehemu Askofu Mstaafu Gabriel Mmole: kwa wema, upole  na utumishi mwema aliouonesha wakati wote wa maisha yake. Waziri Mkuu amesema enzi za uhai wake Askofu Mmole alitoa kipaumbele katika masuala muhimu ya maendeleo ya jamii ikiwemo elimu ambapo alisaidia sana watawa waliomaliza darasa la saba na kuwasaidia wajiunge na shule za sekondari. Waziri mkuu asema, “Hata uanzishwaji wa Chuo Kikuu cha STEMMUCO ambacho ni tawi la SAUT hapa Mtwara ni moja ya jitihada zake alizozifanya katika kuhakikisha anawapa elimu bora vijana na jamii.  Kifo chake ni pigo kubwa kwa Taifa kwa sababu tumepoteza kiongozi wa kiroho aliyesimamia kwa uadilifu ustawi wa jamii ya Kitanzania.”

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa aliwashukuru viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini mkoani Mtwara kutokana na ushirikiano mzuri anaopata unaomwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Mazishi hayo yamehudhuriwa na maelfu ya wananchi, maaskofu wa majimbo mbalimbali nchini, Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa na mkewe Mama Anna Mkapa, Waziri wa Nchi OR-Utumishi na Utawala Bora Mheshimiwa Huruma George Mkuchika. 

Itakumbukwa kwamba, Askofu Mstaafu Gabriel Mmole alizaliwa kunako Januari Mosi, 1939 katika Parokia ya Nangoo. Baada ya masomo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 14 Oktoba 1971. Kunako tarehe 12 Machi 1988, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mtwara na kuwekwa wakfu tarehe 25 Mei 1988. Akang'utuka madarakani mwaka 2015 na amefariki dunia, 15 Mei 2019. Amezikwa tarehe 21 Mei 2019.

Askofu Mmole: Mazishi

 

22 May 2019, 17:29