Tafuta

Vatican News
Frateli Frank John Gilagiza Jimbo la Kigoma Tanzania anathibitisha wito wake wa kikuhani kuchanua kwanjia ya kuongozana na baba yake kuimba kanisani akiwa mdogo Frateli Frank John Gilagiza Jimbo la Kigoma Tanzania anathibitisha wito wake wa kikuhani kuchanua kwanjia ya kuongozana na baba yake kuimba kanisani akiwa mdogo 

Shemasi wapya wa Kanisa:Wito wa Frateli Frank Gilagiza

Frateli Frank Gilagiza wa Jimbo katoliki la Kigoma,Tanzania,katika mahojiano na Radio Vatican anaonesha hatua zake za kugundua wito wa kikuhani,hasa tendo la kuongozana na baba yake kwenda kuimba Parokiani.Baadaye kuomba kutumikia,kuvutiwa mavazi ya kikuhani na hatimaye kujiunga na seminari.Mei Mosi 2019 anapewa daraja Takatifu la Ushemasi!

Na Sr. Angela Rwezaula–Vatican/Frt Frank Gilagiza,Chuo Kikuu cha Kipapa cha Msalaba Mtakatifu-Roma

Yesu alitaka kuchagua mitume wake, Mitume ambao watakuwa marafiki wake sana na watapata mazoezi ya aina ya pekee. Mazoezi hayo yalikuwa ni kuwalekeza nini watafanya, hasa katika kuimarisha zizi lake. Kanisa la Mungu tangu wakati wa Yesu halijakosa wafuasi wake. Yesu anaendelea kuita, kwa maana shamba la Mungu ni kubwa na watendakazi ni wachache,basi mwombeni Bwana wa mavuno atume wafanyakazi wavune mavuno yake (Mt 9,37-38). Na hii inahitaji imani mang’amuzi ya miito kama kauli mbiu iliyoongoza Sinodi ya Maaskofu 2018 kuhusu Vijana! Na Katika safari ya miito ya Kanisa, Mwezi Mei, unafunguliwa na neema kubwa ya kuwapata wafuasi wengine wapya ambao wanajiandalia ukuhani, kwa Kanisa la Tanzania kwa namna ya pekee, lakini hata katika Kanisa la  ulimwengu mzima, hasa hapa Roma, ambapo tarehe Mosi tunawapata mashemasi wawili wapya kutoka Tanzania, vile vile Jumamosi 4 Mei 2019 Mafrateli wengine Watanzania wakiunganika  na wenzao kutoka pande za Dunia, watapata daraja la ushemasi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro. Ni misa itakayoongozwa na Kardinali Ferdinando Filoni, Rais wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. 

Kati ya washemasi watarajiwa Mei Mosi 2019, ndani ya studio za Radio Vatican ni bahati kutembelewa na mmoja wao ambaye anajitambulisha yeye ni nani:

Mimi ninaitwa Frateli FRANK JOHN GILAGIZA, mzaliwa wa parokia ya Mt. Vicent wa Paulo, Katubuka, Jimbo katoliki la Kigoma, nchini Tanzania, Afrika Mashariki. Ni mtoto wa kwanza katika familia ya Baba John Nkuzugwa Gilagiza na Mama Moleni Bujiji Bazara, nikifuatiwa na mdogo wangu Maria John Gilagiza, Flora John Gilagiza na Damian John Gilagiza. Nilizaliwa 07.04.1990, Wilaya ya kigoma mjini, mkoani kigoma nchini Tanzania. Nilijiunga na masomo ya awali kabla ya shule ya msingi katika shule iliyoratibiwa na Jumuiya ya Mt. Magdalena, kigango cha Mt.Vicent wa Paulo- katubuka, nilisoma kwa miaka miwili,{1995- 1996}, kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi katubuka {1997-2002}, kisha kujiunga na shule ya Msingi kiezya {2003-2004}, ambapo nilimaliza darasa la saba, baada ya Shule ya msingi.

Frateli Frank suala la wito wakati mwingine ni gumu hasa namna ya kujua ni kwa jinsi gani unaitwa, unasikiliza au unagundua, je unaweza kuelezea historia yako ya  wito huu mtakatifu wa kikuhani kwa ufupi?

Ndiyo, kwanza nilipata Sakramenti ya Ubatizo kunako tarehe 25 Desemba 2000, Katika Kanisa la Mt. Vicent wa Paulo-Katubuka, kwa miaka yote nikiwa shuleni tokea darasa la awali, tayari nilishaanza mafundisho ya dini, parokiani katubuka, na kusali jumuiya kila juma, pamoja na wazazi wangu, tulisali sala za usiku kila jioni, hivyo tayari nilishaanza kuwa karibu na Mwenyezi Mungu kwa namna ya pekee. Kwa miongo kadhaa, Baba yangu amekuwa mwimba kwaya kwenye kwaya ya Yesu Kristu Mfalme-Katubuka, ambapo na mimi ni muimba kwaya, katika miaka hiyo nilikuwa nikimsindikiza Baba yangu akienda mazoezini, hivyo nikapata kuwa karibu na mapadri kidogo ukilinganisha na awali, kisha nilipofika darasa la tatu, nilimuomba Baba, nitakapopata kumunio ya kwanza aniandikishe katika kikundi cha watumikiaji wa pale parokiani kwetu na alifanya  hivyo, kwani nilikuwa mtumikiaji kwa miaka mitano (2000-2005), ni kipindi ambacho wito wangu wa Upadre uliimarisha na kuanza taratibu kuchanua kama ua dogo tu, kwani katika umri ule niliweza mara kadhaa kulinganisha maisha ya ndoa na ya wito wa upadri na kwa kufanya hivyo nikawa na uhakika kuwa Mungu ameniita kwa hakika nimtumikie na nijipatie njia yangu ya Utakatifu katika wito huu wa Upadre.

Nilivutiwa na mavazi ya mapadre bila kujua maana na majukumu halisi ya padre

Nilivutiwa na mavazi wanayovaa mapadri wakati wa maadhimisho ya Misa Takatifu, kwa wakati ule sikujua hasa nini maana na majukumu halisi ya padre, hivyo nilivutiwa na kwa namna wanavyohubiri kanisani, kiasi kwamba watu wote wanakaa kimya kuwasikiliza mapadri, nilipendezwa na upendo na heshima ambayo familia yangu ilikuwa nayo kwa mapadri, nikaamini hili litakuwa ni jambo jema pamoja na mapadre kuwaombea watu, pia watu wanakupenda. Wito wangu wa Upadre, uliimarishwa zaidi nilipojiunga na Seminari ya Mt. Yosefu Iterambogo, kwa kidato cha kwanza mpaka kidato cha nne (2005-2008), kisha nikajiunga kwa masomo ya High school, kwa mchepuo wa Sayansi( yaani Physikia, Chemia na Biolojia (PCB), katika Kwiro High School, wilayani ulanga, mkoani morogoro. (2009-2011). Baada ya kumaliza kidato cha sita, nikajiunga na malezi ya Upadre, katika nyumba ya malezi, ya Mtakatifu Petro na Paulo-Iterambogo (2011). Nilijiunga na Seminari Kuu ya Bikira Maria, Malkia wa malaika, Kibosho, Jimbo katoliki la Moshi, kwa masomo ya Falsafa, (2011-2014), baadaye  nikaelekea Jimboni Tabora katika Seminari kuu ya Mt. Paulo-Kipalapala, kwa masomo ya Taalimungu, ambapo nilidumu kwa mwaka mmoja (2014-2015). Kwa mapaenzi ya Mungu nikapata nafasi tena ya kuendelea mjini Roma-Italia, malezi katika Seminari ya Bikira Maria kikao cha Hekima, na ambapo pia kuendelea na masomo katika Chuo kikuu cha Kipapa Cha Msalaba Mtakatifu (Pontifical university of the Holy Cross), baada ya kuhitimu na Shahada ya Taalimungu, (2015- 2018), nimendelea na masomo ya uzamivu katika kitivo cha Taalimungu ya Maadili, ambapo ninamaliza mwaka wa kwanza 2019,na  nikitarajia kumaliza mapema mwakani 2020.

Baada ya kutaja haya masomo na ngazi zote ulizo pitia,inaonesha wazi ni kwa jinsi gani Bwana Mungu amekuwa msaada na nguzo ili uweze kufanikiwa hadi leo hii. Na hii ni shukrani ya pekee kwa Mungu!

Ni kweli kwani katika hija yangu nimeweza kupata fursa  nzuri zaidi ya kupata malezi imara na ya kudumu, pia  kuwa karibu zaidi na mapadre katika kuishi nao na kushirikiana nao kwa ukaribu zaidi katika shughuli za kila siku. Jambo hili limenifanya kuhisi zaidi na  wazi sauti ya Kristu Bwana akiniita kwa upole ili kushiriki kikamilifu ukuhani, ufalme na utawala pamoja nae. Hata hivyo ninapo elekea kulipokea daraja hili takatifu la Ushemasi napenda kwa nafasi ya kwanza kumshukuru Mungu Baba mwenyezi, kwa kuniteua kumtumikia japokuwa sisitahili, na ni kwa mapenzi yake tu. Bila yeye nisingeweza kufikia hatua hii ninayojitayarisha nayo. Aidha kutokana na kuwa mbali na nyumbani niliko zaliwa Tanzania, sina budni kumshukuru Mungu hata kuwaleta watu wote kwake ili wamtumikie, wapo watazania wengi wanaosoma hata Roma na wengine wanaotarajia kupata ushemasi baada yetu, lakini pia niwashukuru sana wazazi wangu kwa malezi na majitoleo yao makubwa ambayo yanaoneaka kwamngu leo hii.  Shukrani zimwendee Baba Askofu Joseph Mlola ALCP.OSS), kwa malezi ya kibaba, upendo na ukarimu wake hauna mfano, Mungu amjalie miaka mingi ya kuishi.

Shukrani kwa Baba Askofu Mkuu Protace Rugambwa

Nimshukuru kwa namna ya pekee Baba Askofu Mkuu, Protase Rugambwa, aliyeniruhusu na kunipokea jimboni kigoma mwaka 2011, na hili kwangu naliona kama maajabu ya Mungu kwa leo hii, akiwa katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa la uinjilishaji wa watu Vatican  na ambaye inakuwa fursa kwetu kutoa daraja Takatifu ya Ushemasi! Kwa hakika mipango ya Mungu, haina mipaka na tukiri kwamba, kile anachopanga mwenyezi Mungu ndicho hicho, sisi ni wadogo tunahitaji kusikiliza, kutii na kufuata nyayo zake. Hakika Mwenye nguvu amenitendea makuu na jina lake ni Takatifu! (Lk 1,49). Nawashukuru kaka zangu mapadre, walezi, ndugu jamaa na marafiki, ambaye kila mmoja kwa namna ya kipekee wameweza kushiriki kwa namna moja au nyingine katika malezi na makuzi yangu ya wito kufikia hapa na kwa wote walio mbali na karibu, ninawakaribisha katika Daraja Takatifu ya Ushemasi hapa Roma tarehe Mosi 2019  kwa kutusindikiza kiroho na kimwili, ili kumtumia , maana ametuita.

Tunapofikia mwisho wa mahojiano yetu ndani ya studio hizi,unawashauri nini watu, hasa hasa vijana wa kizazi kipya?

Kwa upande wangu nafikiria kurudia maneno ya Mama Kanisa kwa njia ya  Sinodi ya Maaskofu wakiomba kukazia shughuli za kujielekeza zaidi katika utume kwa vijana, ili kujenga sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwaongoza kufanya maamuzi mazito katika maisha. Na zaidi kutafsiri matukio mbali mbali katika mwanga wa Maandiko Matakatifu ili baadaye wapate, kufanya maamuzi magumu ambayo watapaswa kuyatekeleza haraka kwa kushirikishana mang’amuzi yao baada ya kukutana na Kristo Mfufuka kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Emau. Na pia nikikumbuka maneno ya Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa vijana wa kizazi kipya  walipokuwa wakijiandaa na  maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama ilinigusa hasa kwa kutazama maneno ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa aliyesema  “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. (Lk. 1:38).

Vijana kama mimi wasiogope kukabiliana na changamoto ya kujisadaka maisha yao

Vijana kama mimi, wasiogope kukabiliana na changamoto ya kujisadaka katika maisha yao, kwa kuendelea kujiimarisha, kujiamini, kujadiliana na kusikiliza kwa makini kama alivyofanya Bikira Maria, Mama yetu aliyesikiliza kwa makini ujumbe wa Malaika Gabrieli na mwisho wake akatoa, jibu linalostahili na ndiyo huo ushuhuda wa ujasiri na ukarimu kwa mwamini aliyetambua siri ya wito wake, tayari kujaribu kuthubutu bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Hii ndiyo hata siri yangu katika maisha yangu ya wito,kusikiliza hasa waliotangulia na kuomba neema kwa Mungu,kutafakari neno la Mungu, kwenda kinyume na mantiki za kisasa. Huu ndiyo ushauri wangu kwa vijana lakini pia ninao jipyaisha mimi mwenyewe kila siki na hasa ninapokaribia kupewa hili daraja la ushemasi.

Nijalie mapaji ya Roho Mtakatifu kutimiza mapenzi yako ee Bwana

Na mwisho kabisa  ninapenda nimalizie na sala hii: Umeniita Bwana nikutumikie Nami nitafurahia, wito wangu kuwa mtumishi wako! Nimesikia sauti yako ninakuomba unipokee  kukutumikia. Haijalishi safari kama ni ngumu,yenye milima na mabonde maana wewe unanipa mkono wako na kunijalia nguvu ambazo naziona leo hii katika maisha yangu. Ninakuomba unitume popote utakako ili niweze kuchunga kundi lako utakalo nikabidhi. Mavuno ni mengi, unasema Bwana na watenda kazi ni wacheche… (Lk 10,2);  Ninapojongelea ushemasi, ninakusihi sana nipatie nguvu ili kuweza kufikia hatua nyingine ya daraja Takatifu la Upadre. Ni katika udhaifu wangu Bwana umeniita kimaajabu, kwa uhakika wa kunijalia mapaji ya Roho Mtakatifu yaniongoze niweze kutimizia mapenzi yako Ee Bwana Amina.

Shukrani Frateli FRANK JOHN GILAGIZA kwa ushuhuda wako na kwa niaba yako pia tunawatakia matashi mema na baraka tele katika wito huu mtakatifu wa kumtumikia Mungu kwa namna ya pekee. Asante sana!

Wito wa Frt Frank Gilagiza
29 April 2019, 14:21