Tafuta

Vatican News
Alhamisi Kuu: sakramenti ya Ekaristi Takatifu! daraja Takatifu ya Upadre! Amri ya Upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa maskini na wanyonge! Alhamisi Kuu: sakramenti ya Ekaristi Takatifu! daraja Takatifu ya Upadre! Amri ya Upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa maskini na wanyonge!  (Vatican Media)

Alhamis Kuu: Daraja Takatifu: Wasifu wao! Ekaristi & Upendo

Kanisa linaadhimisha Alhamisi kuu kwa Mwaka 2019 kukumbuka Siku ile Kristo Yesu alipoweka Daraja Takatifu ya Upadre: Wahudumu wa Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma. Mwaliko kwa wote ni toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Hii ni Siku Yesu alipoweka Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa! Ni Siku ya Amri ya Upendo kwa maskini!

Na Padre Alcuin Maurus Nyirenda, OSB. – Vatican.

Viongozi wote wanao wajibu wa kuwaongoza raia au waumini wao na kuwaletea maendeleo ya kiroho na kimwili. Wanafanya hivyo kwa maneno lakini inafaa zaidi kwa mfano na ushuhuda wa matendo ya maisha yao. Watawala na viongozi hao wakiwa kama binadamu hawana watu wa kuwanyooshea vidole wanapopotoka. Bwana wetu Yesu Kristo aliwakosoa Makuhani (mapadre) na wakuu wa nchi. Aliwatahadharisha pia mitume wake (mapadre wake wa kwanza) dhidi ya watawala wabadhilifu: “Jihadhalini na Waandishi na Mafarisayo. Mambo yote wanayowaambia ninyi, yafanyeni na kuyashika, lakini msifanye kulingana na matendo yao, kwa maana wao husema lakini hawatendi.” (Mt. 23:3).

Kuna viongozi wachache sana wenye maadili na wacha Mungu wanaoweza kujikosoa wenyewe na kuchukua tahadhari ya kujirekebisha tabia zao potofu. Nchi ya Tanzania imebahatika kupata baadhi ya viongozi waadilifu na wacha Mungu wanaodiriki kujikosoa na kujiasa wenyewe wanapokosea. Mathalani mtumishi wa Mungu na mhasisi wa Taifa aliandika kitabu kiitwacho: “Tujisahihishe”. Humo anaonesha baadhi ya makosa ambayo viongozi wa taifa na raia wake inabidi waepukane nayo. (Hayati Mwl. Nyerere). Kiongozi mwingine mwenye kumcha Mungu alipojiona yeye na viongozi wenzake wamepotoka mno kimaadili akajikemea bila aibu kwa kauli mbiu ya: “Kujivua magamba.” (Mhe. Kikwete). Kiongozi wa sasa anarudia mara nyingi kusema: “Ndugu zangu mniamini mimi: Nchi hii imejaa madudu mengi sana. Tumwogope Mungu. Tukifanya kazi na kumtanguliza Mungu tutafika tu. Mniombee sana.” (Mhe. Magufuli). Kadhalika viongozi wa juu wa kanisa Katoliki daima wameonesha mfano wa kuomba radhi kwa ulimwengu kutokana na makosa yanayotendwa na kanisa (Baba Mt. Yohane Paulo II).

Papa Francisko mara baada ya kuchaguliwa kwake aliwaomba waamini wote wamwombee. Sasa hivi anaomba radhi kwa makwazo yote yaliyotendwa na yanayotendwa na Makuhani wake ikiwa ni pamoja na kuwalawiti watoto wadogo na kuwaharibu masista. Aidha hafumbii macho kasoro za viongozi wa Kanisa kijumla. Anawakosoa na kuwapa adhabu hata ya kuwafungia huduma kuanzia makardinali, maaskofu hadi mapadre na watawa.  Kumbe, Mapadre na Maaskofu wanao mwanya mkubwa sana wa kuwafundisha na kukemea maovu ya waamini wao. Lakini bahati mbaya wao wenyewe hawasikiki kamwe wakijikosoa na kuomba radhi kwa makosa wanayotenda. Kuna waamini na raia wengi wanaowapenda viongozi wa dini. Waamini hao wanaumia sana wanapowaona viongozi wao wanapotoka na kukosolewa hadharani. Lakini kwa vile wanakosa pahala pa kutolea rai zao wanakaa kimya na hivi kutenda dhambi ya kutotimiza wajibu wao. Hali hiyo inawapelekea viongozi hao kujibweteka na kujidhani watakatifu.

Ndugu zangu ulimwengu wa leo wa utandawazi, hauna siri. Kila anayetaka kutangaza habari zake anajirusha mtandaoni na ujumbe unasambaa mara moja kama moto wa kiangazi. Waumini waliochoka kuona tabia mbovu ya wachungaji wao wanajitokeza hadharani na kuwakosoa kwa kutumia mitandano ya jamii. Mathalani, mwanzoni mwa kwaresima ya mwaka huu, nilirushiwa tangazo la nabii mmoja aliyekuwa anahubiri sokoni kwa sauti kubwa iliyosikika wazi wazi kwa watu mbalimbali akiwakosoa mapadre wakatoliki:  “Muwaambie mapadre wenye watoto: Nabii anasema ya kwamba hakuna kuadhimisha ibada tena kuanzia wiki ijayo hadi waje niwaelekeze. Wanaingiaje namna gani kwenye toba? Toba ikoje kwao? Nyie wadada chukueni namba ya simu ya nabii wanitafute niwaelekeze! Ninyi wadada wenye watoto wa mapadri ninyi...”   Lafudhi ya mtangazaji ililinichekesha lakini ujumbe ulinifikirisha sana. 

Leo ni Alhamisi Kuu ni Sikukuu ya mapadre wote. Siku ya leo Yesu aliiweka Sakramenti ya Daraja Takatifu na ya Ekaristi Takatifu. Yesu mwenyewe aliwachagua mapadre wake (mitume kumi na wawili) akawapa uwezo wa kugeuza mkate na divai kuwa mwili na damu yake. Je, aliwachagua mitume (mapadre) wa aina gani? Je, Yesu mwenyewe anawaonaje mapadre wa leo wanaodhalilishwa hadharani? Je anaweza bado kuwachagua mapadre na kuwatuma kazi kama alivyowatuma mapadre wa kwanza? Basi ninawaalika kuziona sifa walizokuwa nazo wale mapadre wa kwanza waliochaguliwa na Yesu mwenyewe kisha tuwalinganishe na mapadre wa kizazi cha leo. 

Ndugu zangu endapo Yesu angewapeleka Mitume wake wote kumi na wawili kwenye hospitali za sasa za Saikolojia kabla ya kuwapa uongozi na kuwatuma kazi ya uchungaji angepata majibu gani? Baada ya kupita vipimo vyote na kuchunguza ubongo kwa mashine za kisasa yafuatayo ni majibu ya wataalamu wa Saikolojia: “Awali ya yote tunakushukuru Mkuu wa Taasisi (Bwana Yesu) kwa heshima uliyotupatia ya kuwapima watu hawa kumi na wawili uliowachagua kabla ya kuwatuma kushika nafasi nyeti za uongozi katika Taasisi yako mpya ya kidini. Umetupatia jukumu nyeti ambalo tumefanikiwa kulitekeleza kiumahili kadiri ya uwezo wetu tukitumia pia vifaa vya kitaalamu vya kisasa.

Kila mteule tumemwangalia mmoja mmoja na kumpima afya yake kinagaubaga hasa katika uwanja wa Saikolojia na kimaadili. Tulichunguza ubongo na akili ya kila mmoja. Matokeo ya vipimo vya kila mmoja tumevihifadhi kwa siri katika kompyuta na tume-backup. Wataalamu waliobobea katika uwanja wa Saikolojia waliketi pamoja na kumpima kila mmoja peke yake na kuhojiana naye kwa kipindi kirefu. Tukapata pia ushauri kutoka kwa mtaalamu mwenye mang’amuzi ya muda mrefu katika masuala ya miiko ya kazi kama inavyodaiwa na Taasisi kama hii yako. Hatimaye jopo la wataalamu walikaa pamoja kujadili matokeo yao. Sote kwa pamoja tumejiridhisha na matokeo ya vipimo tulivyochukua. Ripoti yao ya jumla kama kikundi tumeona kwamba wakandidati wako wanakosa sifa stahiki kwa kazi unayotaka kuwatuma. Sifa hizo ni pamoja na kukosa elimu ya msingi na ya kawaida kabisa ya ujuzi na uzoefu wa kazi unayowaitia. Aidha pamoja na sifa hiyo pia ndani yake kuna u dotcom yaani hali ya ufyaku usioweza kuanika kirahisi.

Jambo jingine la msingi zaidi ni kwamba watu wako kwa ujumla wao wanakosa sifa ya ushirikiano na mshikamano, yaani teamwork. Tumeona pia tukuchambulie tabia ya mmoja mmoja ili uone mwenyewe nani angalao anayo sifa na unaweza kumtegemea kwa kazi. Tukianza na Simoni Petro. Bwana huyu kwa kweli hana msimamo na ni mtu wa kuwaka hasira za ghafla ghafla.  Halafu mdogo wake Andrea kwa vyovyote “tunda halitui mbali na mti wake.” Huyu anakosa kabisa sifa za uongozi. Kuna ndugu wengine wawili mtu na mdogo wake nao ni Jakobo na Yohane hawa wanao ubinafsi zaidi.

Yaani wametanguliza mno masilahi binafsi badala ya kuweka kipao mbele uzalendo na Taasisi yako. Halafu Tomas, yeye ameonesha waziwazi tabia ya mashakamashaka na ya kutokuwa na uhakika wa mambo. Tabia hiyo inavunjisha moyo wa kundi na mdadi wa utendaji kazi. Kuhusu Mathayo kwa vile alikuwa mtoza ushuru tumefuatilia CV yake ya kazi kutoka ofisi ya forodha na ushuru hapa Yerusalemu. Tumekuta jina lake liko katika orodha ya mafisadi na wala rushwa wakubwa. Hivi siyo mtu wa kumtegemea na kumwaminisha shughuli nyeti za pesa.

Yakobo na Thadei watoto wa mzee Alphayo Wote wawili wana maelekeo mabaya ya siasa kali na wanaonesha dalili za ujasusi wa chini chini. Ila kuna bwana mmoja tu ndiye aliyeonekana anafaa na mwenye sifa stahiki za kufanya kazi katika Taasisi yako. Bwana huyu anao uwezo wa kutosha na mwenye sifa za uongozi. Anahusiana vyema na watu, ana wasiliana mara nyingi na watu wenye vyeo vya juu katika ngazi ya serikali na dini. Anaonekana pia amehamasika vizuri sana. Kwa kweli bwana huyo amechomoza sana katika kundi kwa kuwa na kiwango cha hali ya juu sana cha kufikiri na nimuwajibikaji mzuri. Anaweza kufuata vizuri kasi yako ya kazi.

Hivi sisi sote kama jopo la wataalamu wa Saikolojia kwa kauli moja tunampendekeza bwana Yuda Iskarioti umweke mkono wako wa kuume, ili aweze kwa karibu zaidi kuratibu vizuri kazi zako, hususan masuala ya uchumi na uongozi kijumla.  (Waganga Kitengo cha Saikolojia). Baada ya kuipata na kusoma ripoti hii kutoka kwa Wataalamu wale, Yesu akaichana na kuichoma moto kwa sababu alishaijua tabia ya mitume wake itakavyokuwa hapo mbele na hatima yake. Aidha yeye alifuata vigezo vya mtindo wake vilivyotofautiana kabisa na vipimo vya wataalamu wa duniani. Kwa hiyo, akaamua mara moja kuwateua Mitume wake na kuwaweka karibu naye, akitegemea baadaye kuwatuma kazi ya uvuvi wa watu yaani uchungaji. Lakini baada ya kuwa na mitume hao kwa muda fulani, ikagundulika kwamba mitume wale walikuwa kweli na tabia ileile kama ilivyoandikwa katika ripoti ya Wanasaikolojia.

Hebu fuatilia: Mathalani Petro. Huyu ndiye aliyemkana Yesu kule uani kwa Kuhani mkuu (Mt 26:69-75). Hii inadhihirisha kwamba Petro hakuwa mwaminifu. Alikosa msimamo na nguvu ya kusimama kama mwanaume na kujitetea mbele za watu. Aidha alionesha wazi wazi papara zake na kulopoka mambo bila kufikiri na kuapa uwongo hata mbele ya kijakazi. Halafu Andrea mdogo wake Petro. Tabia ya huyu bwana ilijitokeza zaidi katika nafasi ile Yesu alipoongeza mikate na samaki na kuwalisha watu. Andreas alimwambia Yesu: “Hapa yupo mvulana mdogo ambaye ana mikate mitano ya shayiri na samaki wadogo wawili. Lakini vitu hivi ni nini kwa watu wengi sana hivi?” (John 6:9)

Mapendekezo na swali hili la Andrea linaonesha wazi kwamba hakujua kitu chochote juu ya uwezo wa Yesu. Yaonesha kama vile anamfundisha Yesu kazi, na hivi hamwamini. Halafu Yesu aliwaita Yakobo na Yohani wakiwa ndani ya mashua wakizitengeneza nyavu pamoja na baba yao Zebedeo kama tusomavyo: “Pia, alipoendelea mbele kutoka hapo akaona wengine wawili waliokuwa ndugu, Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana ndugu yake, katika mashua pamoja na Zebedayo baba yao, wakitengeneza nyavu zao, naye akawaita.” (Mt 4:21).  Umeona mwenyewe kwamba mabwana hao waliposikia tu mwito wa Yesu mara moja wakaziacha nyavu na baba yao mashuani wakamfuata. Ukiwafuatilia vizuri haraka hii ya kuacha kazi na mzazi, inaonesha kama vile hawakuridhika na kipato walichokuwa wanapata katika shughuli hiyo na pengine hata hawakuridhika sana kufanya kazi na mzee wao. Hivi walipopata mwanya huo wa kuitwa wakachangamkia masuala na kuondoka mara kumfuata Yesu. Kwa hiyo siyo bure, mabwana hawa walikuwa na agenda zao binafsi za kumfuata kama tusemavyo waswahili: “Mkono mtupu haulambwi.”

Ukweli ni kwamba watu hawa wawili walifuata vyeo, walitaka "kupata ujiko na umaarufu". Hilo unaliona jinsi wakati mmoja walivyomwendea Yesu na kumtega kwa swali nyeti: “Mwalimu, tunataka utufanyie chochote tutakachokuomba.” (Mk 10:35) Yesu hakuwajibu moja kwa moja badala yake akawauliza “Mnataka niwafanyie nini?” (Mk 10:37) Wakamwambia: “Uturuhusu kuketi, mmoja kwenye mkono wako wa kuume na mmoja kwenye mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako.” (Mk 10:36-37). Aidha kama unakumbuka zaidi mara moja walipopita kule Samaria jinsi wananchi wake walivyokataa kumpokea Yesu licha ya kwamba aliwatuma ndugu hawa wawili Yakobo na Yohane kuandaa ujio wake. Baadaye mabwana hao hao wakageuka na kumshauri Yesu: “Bwana unapenda tuagize moto toka angani tuwaunguze?”  (Lk 9:53). Ndiyo maana mabwana hawa wanaitwa pia Wana wa ngurumo. (Mk 3:17). Kwa hiyo unawaona moja kwa moja mabwana hawa kwamba walikuwa majasusi na majambazi wa kutupwa.

Halafu Yesu alimwita Bathlomayo. Kwa bahati mbaya hatujui zaidi habari zake. Mtume huyu anatajwa kuwa ni mmoja kati ya wale kumi na wawili. Lakini hatuambiwi alisema nini au alifanya kitu gani chenye mshiko katika utume wake. (Mat 10:3; Mark 3:18; Luke 6:14; Mdo 1:13). Yawezekana mtume huyu hajulikani kwa sababu pengine alikuwa mtu wa aibu aibu, asiye msemaji na mwenye kuona aibu ya kuongea mbele za watu. Halafu kuhusu Mateo (Mt 9:9). Kabla ya kuitwa kwake Mateo alikuwa mtoza ushuru. Kazi hii ilikuwa na kipato cha juu sana kilichopatikana pia kwa rushwa na ufisadi. Endapo Mateo angekuwa na sifa sawa na za watoza ushuru wengine asingekusanya kodi nyingi zaidi zilizomwezesha kwenda hadi Roma. Kadhalika ni dhahiri kwamba Mathayo, mtoza ushuru alikuwa fisadi na mwenye maadui na alikuwa na maadui wengi waliomchukia.

Yesu alimwita pia Tomas. Mtume huyu anajulikana kwa kukosa imani. Yeye aliweza tu kuamini ufufuko wa Yesu baada ya kutia vidole vyake kwenye majeraha ya misumari na kugusa kwa mkono wake tundu la mkuki uliotobolewa kwa mkuki. (Yoh. 20:25).  Kwa tabia hii ni dhahiri Tomas hakuwa na imani na Yesu.  Zaidi tunajiuliza maswali mawili nyeti yasiyo na majibu juu ya Tomas: Mosi, alikuwa wapi jioni ile ya Jumapili ya Pasaka pale Yesu alipowatokea mitume kwa mara ya kwanza? Pili kwa hoja gani alikosekana mle chumbani walimojifungia mitume wenzake?

Maswali kama haya tata ndiyo yanayotia dosari katika kazi za jumuiya au katika jamii yoyote ile. Halafu tunaye Simon aliyeitwa pia Mzeloti yaani Mkereketwa au Muwashwawashwa (Lk 6:15). Wazeloti walikuwa wanapigania uhuru (wanajeshi) dhidi ya utawala wa Kirumi. Ni dhahiri kwamba Simoni huyu mzeloti hakujua kwamba vurugu na vita hazina tija katika maisha bali zinachochea uovu tu. Kwa hiyo mtume huyu alikuwa bado na kazi ya kujifunza katika mwito alioitiwa. Yesu alimwita pia Yuda Iskarioti. Mtume huyu ndiye aliyemsaliti Yesu. (Mt 26:14-15).

Unakumbuka kwamba Mtume huyu ndiye aliyerundikiwa sifa nyingi sana za ukweli kutoka kwa wataalamu wa Saikolojia. Lakini matatizo ya Yuda yalijionesha hasa pale alipokuwa anamdai na kumlazimisha Yesu aingize utawala kadiri ya fikra zake. Mathalani, mara moja alithubutu kumzuzua Yesu kuwa hajui mahesabu na thamani ya vitu na matumizi yake pale Yesu alipojiruhusu kupakwa mafuta ya thamani sana na yule mwanamke. Kumbe Yuda baada ya kufanya mahesabu ya haraka haraka akaona kuna mshiko mkubwa. Hivi alitaka mafuta yale yauzwe ili pesa itakayopatikana igawiwe kwa maskini. (Yoh 12:4- 6) “Akili kichwani.” Lengo kuu la Yuda alitaka wagawiwe maskini ili aweze baadaye kuwaibia kiulaini.

Ndugu zangu hii ndiyo hali halisi ya tabia za mitume wa Yesu. Yuda peke yake ndiye aliyeonekana kuwa na sifa stahiki za kuwa kiongozi. Mara nyingi sifa nzuri kama za Yuda ndizo zinakuwa kigezo kinachotumika na wana wa ulimwengu huu katika kuwachagua viongozi wao. Hatimaye viongozi hao wanamwacha Mungu na wanategemea nguvu zao tu na mapato yake wanageuka kuwa mafisadi wakutupwa. Kumbe Yesu anatumia vigezo tofauti na vya ulimwengu huu. Yesu anapenda kuwachagua wakosefu, wadhambi wanaomtegemea yeye.  Kwa sababu ni hao tu ndiyo wanaweza kufanikisha kazi atakayowatuma. Kwa hiyo unaona kwamba ingawaje utafiti wa Wataalamu ulikuwa sahihi na mapato yake yameonekana kulingana, lakini uchaguzi wa Yesu umefanikisha makubwa sana kwa ajili ya Mungu na kinyume chake yule aliyesifiwa na wataalamu aligeuka kuwa fisadi na akamsaliti Yesu na kazi yake. 

Ndugu zangu kasoro na udhaifu wa mitume ulikuwa mkubwa sana. Udhaifu wa mitume ulikuwa kwazo zito zaidi kuliko lile wanalotumia manabii na watu mbalimbali kukosa kanisa siku ya leo. Yesu alishajua udhaifu wetu na fedheha itakayolipata kanisa lake. Lakini hata hivyo alituchagua kulitumikia. Padre yambidi kuwa mnyenyekevu na kuiga mifano ya mitume ya kuwa wanyenyekevu wenye imani na upendo. Paulo aliyewadhulumu Wakristu na aliyeshuhudia Stefano alipokuwa anapigwa mawe hadi kufa anatuambia: “Kwa maana mimi ni mdogo zaidi kati ya mitume, nami sifai kuitwa mtume, kwa sababu nililitesa kutaniko la Mungu. Lakini kwa fadhili zisizostahiliwa za Mungu mimi niko kama nilivyo. Na fadhili zake zisizostahiliwa zilizonielekea mimi hazikuwa za bure, bali nilifanya kazi kuwapita wao wote, lakini si mimi bali ni fadhili zisizostahiliwa za Mungu zilizo pamoja nami” (1 Kor 15:9-10).

Lakini mara nyingi sisi tunakosa imani kama Petro. Kumbe tuwe tayari kujifunza mambo kama Andrea na kuacha ubinafsi kama Yakobo na Yohane wa kutaka ukubwa. Tuache kung’ang’ana na mambo ya zamani kama Mateo. Aidha tuwe kama Tomasi tuache kuwa na wasiwasi na kukosa imani. Daima tukumbuke kwamba kama Yesu aliwaita na kuwatumia katika kazi mitume wale dhaifu, na hivi atatutumia hata sisi licha ya udhaifu wetu.  Yesu anajua maweza na madhaifu yetu na kitu gani tunaweza kukifanya kwa ajili ya ufalme wake. Sisi tuitikie tu mwito wake na tuwe wanyenyekevu. Tukiri udhaifu wetu na tukubali na kupokea tunapokoselewa. Tuujute udhaifu wetu na kujitahidi kuuacha.

Tusikilize kwa makini maonyo ya waamini. Tujisahihishe, tujivue magamba ya udhaifu wetu. Tusali sana hasa mbele ya Ekaristi Takatifu na tuwaombe waamini wetu watuombee mbele ya Ekaristi Takatifu. Yesu mwenyewe atatusaidia tusikate tamaa mbele ya manabii wa mitaani wanaotufedhehesha kwenye mitandao na kutuzingizia mambo ya ukweli. Kwa njia ya Yesu anayetukingia kifua mbele ya Baba na wewe mwenyewe ukijitahidi kusali mbele ya Ekaristi Takatifu, hapo utapata nguvu ya kutekeleza majukumu yako na kufanya kazi kubwa zaidi kwa sifa na utukufu wa Mungu na ufalme wake. Heri sana kwa sikukuu ya Upadre na Ekaristi Takatifu na huduma ya upendo kwa maskini na wanyonge zaidi! 

17 April 2019, 16:59