Tafuta

Vatican News
Kardinali Polycarp Pengo, ameitaka familia ya Mungu Jimbo kuu la Mbeya, Tanzania kushirikiana na Askofu mkuu Gervas Nyaisonga katika maisha na utume wa Kanisa! Kardinali Polycarp Pengo, ameitaka familia ya Mungu Jimbo kuu la Mbeya, Tanzania kushirikiana na Askofu mkuu Gervas Nyaisonga katika maisha na utume wa Kanisa! 

Askofu mkuu Gervas Nyaisonga: Umoja, Upendo na Mshikamano!

Ibada ya kusimikwa kwa Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga kuwa Askofu mkuu wa kwanza wa Jimbo kuu la Mbeya ni tukio ambalo limeshuhudia ule utambulisho wa familia ya Mungu nchini Tanzania katika umoja, upendo na mshikamano wake, licha ya tofauti zao msingi za: kidini, kiimani, kiitikadi na mahali wanakotoka watu! Hata Rais Magufuli ameliona hili na kulikiri!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya, Tanzania mara baada ya kusimikwa na kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Kuu la Mbeya, Jumapili ya huruma ya Mungu, tarehe 28 Aprili 2019, kwenye Uwanja wa Michezo wa Sokoine, Jijini Mbeya, ameishukuru kwa namna ya pekee familia ya Mungu nchini Tanzania, kwa ushuhuda wa uwepo wake katika tukio hili kuu, linalompatia dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifu watu wa Mungu. Amewaomba waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kumsindikiza katika maisha na utume wake ili “wote wawe na uhai”, kauli mbiu ya maisha na utume wake kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mbeya.

Wachunguzi wa mambo wanasema, hii ni kati ya hotuba fupi sana, kuwahi kutolewa kwenye matukio kama haya! Askofu Flavian Matindi Kassala, Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC katika mahojiano maalum na Vatican News anakiri kwamba, familia ya Mungu nchini Tanzania katika tukio hili la kusimikwa kwa Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mbeya ni tukio ambalo limeshuhudia ule utambulisho wa familia ya Mungu nchini Tanzania katika umoja, upendo na mshikamano wake, licha ya tofauti zao msingi za kidini, kiimani, kiitikadi na mahali wanakotoka watu!

Kumekuwepo na uwakilishi na ushiriki mkubwa wa viongozi wa dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo sanjari na  uwepo wa waamini walei kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Mbeya, changamoto na mwaliko kwa familia ya Mungu, kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kulinda na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu na umoja wa kitaifa, daima: ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi vikipewa kipambele cha kwanza! Itakumbukwa kwamba, Kanisa Katoliki nchini Tanzania mwaka 2019 ni Mwaka wa Familia unaoongozwa na kauli mbiu “Familia kama Kanisa la nyumbani na Shule ya Imani na Maadili”.

Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, ndiye aliyetoa mahubiri katika Ibada ya Misa Takatifu ya kumsimika Askofu mkuu Nyaisonga! Amekazia umuhimu wa kumwilisha huruma ya Mungu katika maisha ya waamini kwa kuondokana na dhambi, ili kukuza na kudumisha amani, utume ambao Kristo Yesu amewapatia wafuasi wake kama zawadi yake ya kwanza baada ya kufufuka kutoka kwa wafu! Ameitaka familia ya Mungu Jimbo kuu la Mbeya kutenda shughuli zake kwa ujasiri, ari na moyo mkuu pasi na woga. Kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu alipowatokea siku ile ya kwanza ya Juma, aliwakirimia kwa namna ya pekee zawadi ya amani na utume wa kuwaondolea watu dhambi. Waamini wanapaswa kushirikiana na kushikamana na Askofu mkuu Nyaisonga ili aweze kutekeleza vyema dhamana na utume wake wa kuongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu, Jimbo kuu la Mbeya!

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi” anawakumbusha vijana kwamba, wao ni leo ya Mungu; na ujumbe makini kwa vijana ni kwamba, Mungu ni upendo na anawapenda vijana! Kardinali Pengo amesema, kuna haja kwa Kanisa na Serikali kushirikiana katika mchakato wa kukuza na kudumisha kanuni maadili na utu wema. Kwa njia hii, familia ya Mungu nchini Tanzania itaendelea kukua na kuimarika zaidi. Jambo la msingi ni kumwachia Roho Mtakatifu kuweza kutekeleza dhamana na utume wake kwa familia ya Mungu nchini Tanzania.

Dhambi ikiondolewa nchini Tanzania, Tanzania itaweza kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uwepo wa dhambi ni sababu ya mipasuko, hali ya kubaguana na watu kutenda yale yasiyofaa mbele ya Mungu na jirani. Kardinali Pengo ameendelea kufafanua umuhimu wa familia ya Mungu Jimbo kuu la Mbeya kutafakari dhamana na wajibu waliokirimiwa na Mama Kanisa kwa kuwapandisha hadhi na kuwa Jimbo kuu la Mbeya. Anasema, hiki ni kielelezo cha ukomavu wa imani.

Katika hotuba yake, Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania amesema, Serikali ya awamu ya tano, itaendelea kukuza na kudumisha uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu, kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania. Licha ya tofauti zao msingi, lakini watanzania wanapaswa kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa. Serikali inatambua dini na taasisi za kiini kuwa ni wadau wakuu wa ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi hasa katika sekta ya elimu na afya.

Rais Magufuli, amewasihi viongozi wa kidini nchini Tanzania kuendelea kuliombea taifa ili liweze kudumu katika misingi ya haki, amani, umoja na mshikamano sanjari na kuwafunda waamini wao ili kuondokana na dhambi zinazoendelea kusababisha majanga, rushwa, ubadhilifu na vitendo vyote vinavyovunja haki, utu na heshima ya binadamu! Amewaomba viongozi wa dini pamoja na waamini wao, kuendelea kumwombea, ili aweze kutekeleza vyema dhamana na majukumu yake kama Rais, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wanyonge.

Kwa namna ya pekee kabisa, amempongeza Askofu mkuu Nyaisonga ambaye alimfahamu tangu alipokuwa Jimbo Katoliki la Dodoma, lakini zaidi, pale viongozi wakuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania walipomtembelea Ikulu, kumsalimia na kujitambulisha! Alionja ndani mwake: unyenyekevu wa hali ya juu na upendo thabiti, kiasi kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alimpoteua kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mbeya, hakushangazwa sana na uteuzi huu. Amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwombea Askofu mkuu Nyaisonga ili aweze kusonga mbele katika maisha na utume wake.

Rais Magufuli anasema, licha ya kuwa Askofu mkuu Nyaisonga ana uzoefu mkubwa katika maisha na utume wake, anatambua wazi kwamba, huu ni utume nyeti, wenye changamoto mbali mbali. Kwa maneno ya Mtume Paulo kwa Tomotheo kuhusu Askofu, kwa kukazia zaidi kuhusu: busara, utaratibu, ukarimu, nidhamu na wala asiwe mtu mlevi wala mwenye kupenda fedha. Rais Magufuli amesema katika ujana wake, alitamani sana kuwa Padre, lakini hakufanikiwa, anawaomba Mapadre kudumu katika maisha na wito wao na kamwe wasilegee na kutamani kuondoka huko! Wakati wa matoleo, Rais Magufuli amekusanya sadaka kutoka kwenye jukwaa la viongozi waalikwa na kuiwakilisha kwa Askofu mkuu Nyaisonga aliyekuwa anaongoza Ibada. Amewasihi kuihesabu vyema!

Askofu mkuu Gervas Nyaisonga
29 April 2019, 17:03