Tafuta

Vatican News
Kanisa kuu la Asmara nchini Eritrea hivi karibuni lilikaribisha vijana zaidi ya 500 kutoka majimbo manne ili kuadhimisha Siku ya Vijana kwa ngazi ya Kitaifa Kanisa kuu la Asmara nchini Eritrea hivi karibuni lilikaribisha vijana zaidi ya 500 kutoka majimbo manne ili kuadhimisha Siku ya Vijana kwa ngazi ya Kitaifa 

ERITREA:Kanisa limeadhimisha Siku ya Vijana kwa ngazi ya kitaifa!

Ofisi ya kichungaji kitaifa pamoja na Kamati ya maandalizi imeandaa Siku ya Vijana duniani kwa ngazi ya kitaifa na katika fursa hiyo Jimbo Kuu la Asmara nchini Eritrea limewakaribisha vijana zaidi ya 500 kuanzia tarehe 8-10 Februari 2019

Na Sr. Angela Rwezaula

Kutokana na kwamba vijana wa Eritrea hawakupata fursa ya kuudhuria  Siku ya vijana Duniani huko Panama(WYD) hivi karibuni, kutokana na sababu mbalimbali kama vile umbali, uchumi na ukiritimba wa serikali, Ofisi ya Kichungaji kitaifa ya Baraza la Maaskofu pamoja na Kamati ya maandalizi wameandaa fursa Siku ya Vijana duniani kwa ngazi ya kitaifa katika Jimbo Kuu la Asmara, kuanzia tarehe 8-10 Februari 2019.

Vijana kutoka majimbo manne kwa ujumla waliwakilishwa na vijana zaidi ya  550 ambao wameweza kuwa pamoja katika fursa ambayo ni ya  kwanza kihistoria katika Kanisa la Eritrea. Umuhimu wa tukio hili ulioneshwa kwa uwepo wa Balozi  wa Vatican nchini Eritrea na Sudan na  ambaye kwa sasa amechaguliwa kwenda nchini Kenya, Askofu Mkuu Hubertus Matheus Maria van Megen. Yeye aliweza kufikisha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko alio utoa katika Siku ya Vijana duniani huko Panama, ambao umewafanya vijana wa Eritrea kuhisi kuwa sehemu moja ya ushiriki wa Siku ya vijana duniani.

Sr. Mehret Tzeggay Mkurugenzi wa Kichungaji kitaifa nchini Erirea anaeleze kwamba, katika fursa hiyo akifafanua Askofu Mkuu Van Megen  kwa vijana amewaeleza kuwa  Baba Mtakatifu Fransiko anawapenda na kupenda watu wa Eritrea. Imani yao imo ndani ya damu na ardhi yao. Na mara kwa mara anamuuliza juu yao na kusali kwa ajili yao kwani anatambua hali halisi. Naye msemaji mkuu katika fursa hiyo mheshimiwa Abune Fikremariam Hagos ambaye aliudhuria Sinodi ya Vijana mjini Roma mwaka jana ametumia fursa hiyo kushirikisha uzoefu wake wa Sinodi na kwa kwa jinsi gani Kanisa linatakiwa kuwasaidia vijana wake katika kukuza imani na mang’amuzi ya miito.

Jumapili tarehe 10 Februari 2019 maadhimisho ya Siku ya vijana ndogo nchini Eritrea yalihitimishwa na Liturujia ya Ukaristi Takatifu iliyoongozwa na Askofu Mkuu Menghesteab Teasfamariam pamoja na Balozi wa Vatican na idadi kubwa  ya mapadre. Wakati wa mahubiri ambayo yalijikita juu ya Injili ya Mtakatifu Luka  2:41-58, Askofu Mkuu Menghesteab alisisitizia kuwa hata kama  Yesu alikuwa ni Mungu, alisikiliza na kuuliza maswali kwa wazee na makuhani. Kwa kufuata mifano hiyo vijana wote wanapaswa kujifunza kusikiliza hekima ya wazee na kuuliza maswali ili  kujua mengi zaidi bila kujizuia wenyewe na kudai kuwa wanafahamu kila kitu na hawana haja ya kutambua  mengine zaidi.

Aidha Askofu Mkuu Teasfamariam alieleza jinsi gani Bikira Maria na Yosefu walimtii Mungu katika maisha yao na kwamba Yesu ni mtu kweli ambaye alikaa na wazazi wake akakua kwa kimo, hekima na neema ilikuwa juu yake. Vijana katika nyakati hizi, lazima wawatii wazazi wao na ili waweze kupata baraka na neema mbele ya Macho ya Mungu na watu amethibitisha! Kwa kuelezea shukrani zao hata  vijana wamethibitisha kumpenda  Baba Mtakatifu pia kuahidi kuendelea kusali kwa ajili yake na Kanisa. Na hatimaye wameonesha matumaini na utashi wao kuwa, siku moja Baba Mtakatifu Francisko anaweza kuitembelea hata nchi ya Eritrea.

 

06 March 2019, 15:19