Tafuta

Baba Mtakatifu alikutana na wahamiaji katika Makao makuu ya Caritas Morocco Baba Mtakatifu alikutana na wahamiaji katika Makao makuu ya Caritas Morocco 

Caritas Morocco:Watu wasikilize ushauri wa Papa juu ya wahamiaji!

Mwakilishi wa Vatican News katika ziara ya Kitume ya Papa,Padre P. Samasumo alikutana na Hannes Stegemann mhusika wa Caritas nchini Morocco na katika mahojiano,anasisitizia umuhimu wa watu kusikiliza ushauri wa Papa katika suala la wahamiaji.Pia mtazamo wa kiuchumi anasema ni jambo zuri kwani mtu anatafuta kwa ajili ya familia

Na Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Katika ziara ya Baba Mtakatifu Francisko, ameongozana na waandishi wengi wa habari wa Radio Vatican na wengine wengi ambao wamefika huko mapema mjini Rabat,na kuweza kutembelea vituo vya hali halisi ya maeneo ya huduma kwa ajili ya watu mbalimbali hasa vituo ambavyo Baba Mtakatifu Francisko ameweza kutembelea mjini Rabat,kutoka Vatican Idhaa ya Kingereza Afrika, ni Padre Paulo Samasumo ambaye alitembelea kituo cha Caritas na mwandishi mwingine Daniele Rocchi alitembelea Kituo cha Utafiti wa mafunzo ya kidini na Ujenzi wa Amani.

Hannes Stegemann mhusika wa Caritas Rabat anaeleza shughuli zao za kituo

Padre Samasumo alikutana na Hannes Stegemann mhusika wa Caritas akiwa ofisi ya  Kituo cha wahamiaji kutoka nchi za Afrika chini ya Jangwa la sahara mjini Rabat. Stegemann akiwa na mambo mengi ya harakati za kundaa ziara  ya kutembelewa na Baba Mtakatifu, wakati huo akiwa amezungukwa watu wengine mahalia, wa mataifa na vyombo vya habari  kwa maana, dunia nzima ilikuwa inataka kujua zaidi kuhusu kituo hicho, lakini kwa bahati nzuri alipata fursa ya kuzungumza naye kuhusu Kituo hicho Caritas ya Rabat kinajihusisha na nini. Stegemann ameeleza kwamba, Caritas nchini Morocco inafahamika sana kwa kazi  kuhusu wahamiaji, lakini hiyo ni moja ya sehemu, kati ya michakato mingine ya shughuli zake zinazotendeka, kwa  mfano wanasaidia mpango kwa ajili raia katika jamii ya Morocco, wanafanya kazi na Mpango wa Utamaduni wa maendeleo vijijini katika nchi na zaidi sasa wanawasindikiza hata vyama 14  vya Morocco ambavyo vinajikita na shughuli ya huduma ya watu walemavu. Japokuwa na shughuli hizo anadhibitisha bado wanajulikana zaidi kwa umma katika kazi ya wahamiaji wanaopitia Morocco au wanaamua kubaki nchini humo.

Ni heshima kutembelewa na Papa na kukutana na wahamiaji

Akiulizwa kile alichokuwa akihisi kuhusu Baba Mtakatifu Francisko kuwatembelea  na kukutana na wahamiaji 60 katika makao makuu ya  Caritas mjini Rabat, amethibitisha, furaha ya hajabu, hasa heshima ya kutembelewa na Baba Mtakatifu na kukutana na wahamiaji ao walio andaliwa. Aidha akijibu swali kuhusu neno la uhamiaji kwa ajili ya uchumi katika mtazamo wa Caritas Morocco, yeye anajibu kwamba, mhamiaji wa kiuchumi si mtu mbaya. Ni mtu anaye tafuta kipato cha kuweza kulisha familia yake hususan watu wanaotoka nchi ambazo hakuna hali  halisi inayo wawezesha kuwa na fursa au msaada wa kijamii. Wahamiaji wanakwenda mahali ambapo kuna kazi,hiyo inawezekana ikawa hata nchi za Afrika au mahali penginepo, anasisitiza Stegemann.

Mzunguko wa uhamiaji kiuchumi ulifanya kazi vizuri sana

Kadhalika ameongeza kusema kuwa huu ni utamaduni wa muda mrefu kwa watu wengi hawa. Kabla ya Mkataba wa Schengen wa mwaka 1985 huko Ulaya, ilikuwa ni kawaida kwa mfano vijana kwenda Ufaransa wakati wa kiangazi kwa ajili ya kufanya kazi katika kiwanda cha magari na kurudi tena baada ya mwaka. Mzunguko wa uhamiaji kiuchumi ulifanya kazi vizuri sana, japokuwa hiyo sasa imebadilika. Suala jingine ambalo limepuuzwa  anaongeza kusema, hasa baada ya kuanguka kwa utawala wa  Muammar Gaddafi, ni kwamba, kati ya watu milioni moja hadi moja na nusu wa Afrika chini ya Jangwa la sahara, walikuwa wana fanyakazi nchini Libya. Hiyo pia imebadilika kutokana na kuanguka kwa utawala wa Libia, Stegemman amesema. Kwa maana hiyo katika suala hili anathibitisha kuwa ni matarajio yake kwamba watu wa Ulaya, waandishi wa habari, wanasiasa na hasa nchi zilizo na watu wengi wakatoliki wanaweza kutumia muda huu kusikiliza Baba Mtakatifu Francisko anapozungumza kuhusu hali ya wahamiaji. Kwa maana sasa katika dunia mjadala mkubwa unaosikika unaongozwa na hofu. Kadhalika ameelezea juu ya hali halisi ya Morocco kwamba Uislamu ndiyo dini ya serikali, lakini  katiba inahakikisha huru wa kila mmoja ili kukiri imani yake, japokuwa haina maana ya kufanya upropaganda.

CARITAS -RABAT
31 March 2019, 12:59