Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu katoliki Ufaransa: Ujumbe wa Kwaresima 2019: Kauli mbiu "Kukua katika ukweli na matumaini" Baraza la Maaskofu katoliki Ufaransa: Ujumbe wa Kwaresima 2019: Kauli mbiu "Kukua katika ukweli na matumaini" 

Maaskofu Katoliki Ufaransa: Kwaresima 2019: Ukweli na matumaini

Kauli mbiu ya ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa, 2019 ni “Kukua katika ukweli na matumaini”. Kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, anaweza kuwaganga na kuwaponya watoto wake kutoka katika dhambi, na kuwapatia nafasi ya kuanza tena upya kwa kuzingatia kwa dhati:Toba na wongofu wa ndani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo imechafua maisha na utume wa Kanisa. Waathirika wameonesha ujasiri wa kutoka mbele na kushuhudia matatizo na changamoto wanazokumbana nazo katika maisha, kama sehemu ya kuponya na kuganga athari za nyanyaso za kijinsia dhidi yao! Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa katika ujumbe wake kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2019 linasema, Kanisa litaendelea kujikita katika mchakato wa ukweli, uwazi na uwajibikaji kama sehemu ya mchakato wa kufyekelea mbali kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo.

Ujumbe huu unakuja wakati ambapo, Kardinali Philippe Barbarin, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lione ametiwa hatiani na kuhukumiwa na Mahakama kwenda jela kwa muda wa miezi sita. Kutokana na hukumu hii, Kardinali Philippe Barbarin ameamua kuwajibika na kung’atuka kutoka madarakani, ili haki iweze kutendeka. Kardinali Barbarin amepatikana na hatia ya kutotoa taarifa kwa vyombo vya sheria kati ya mwaka 2014-2015 baada ya kijana mmoja kushtaki kwamba, alikuwa amenyanyaswa kijinsia, jambo ambalo limewashtua sana watu wengi nchini Ufaransa.

Inasikitisha kuona kwamba, vitendo hivi vinafanywa na viongozi waliopewa dhamana ya kimaadili na kiutu katika malezi na makuzi ya watoto na vijana! Waathirika hawa ni sehemu ya familia ya Mungu inayoteseka kutokana na nyanyaso za kijinsia. Ni kutokana na ushuhuda wao, Kanisa limeweza kutambua kwa ndani zaidi madhara ya nyanyaso za kijinsia katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, kwa sasa linataka kusonga mbele katika kukuza na kudumisha ukweli na uwazi kama sehemu ya mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.

Kristo Yesu anawachangamotisha wafuasi wake kwa kusema, ukweli ambao utawaweka huru! Nyanyaso hizi ni sehemu ya kashfa ya matumizi mabaya ya madaraka ndani ya Kanisa na kwamba, hizi ni dalili za dhamiri mfu! Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa linakumbusha kwamba, Kanisa ni chimbuko la utakatifu wa maisha yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Lakini, Kanisa pia lina watoto wake ambao wamejeruhiwa sana na dhambi ya asili, kiasi kwamba, wanaogelea na hata wakati mwingine, kutopea katika dhambi na ubaya wa moyo!

Kumbe, kauli mbiu ya ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa kwa mwaka 2019 ni “Kukua katika ukweli na matumaini”. Kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, anaweza kuwaganga na kuwaponya watoto wake kutoka katika dhambi, na kuwapatia nafasi ya kuanza tena upya! Toba na wongofu wa ndani ni mambo msingi na kwamba, Kanisa litaendelea kujenga utamaduni wa kuwasikiliza waathirika kwa moyo wa unyenyekevu, ili ukweli uweze kufahamika na haki kushika mkondo wake, na hatimaye, Mama Kanisa aendelee kuwa ni chemchemi ya neema, baraka na utakatifu wa maisha.

Familia ya Mungu nchini Ufaransa inahamasishwa kutoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha, kila mtu alijitahidi kujisadaka bila ya kujibakiza hata kidogo! Waamini na watu wote wenye mapenzi mema waendelee kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake; wawe mashuhuda na vyombo vya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ni changamoto ya kuendelea kuutafuta uso wa Mungu kwa njia ya sala, toba na wongofu wa ndani!

Maaskofu: Ufaransa
18 March 2019, 09:26