Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili VII ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Upendo kwa adui! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili VII ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Upendo kwa adui! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili VII ya Mwaka: Upendo wa adui!

Yesu anawaambia wafuasi wake mara kwa mara wawapende adui, kuwatendea mema wanaowachukia, kugeuza shavu la pili. Upendo, huruma na msamaha ni alama za ushindi za ufuasi. Luka anaamini kuwa haya yote yatawezekana kwa vile aliyeweka haya ana uwezo huo. Kadiri ya Mtume Paulo katika Fil. 4:13 – anasema ‘naweza yote katika yeye anayeniimarisha’.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.

Injili ya leo yaongelea kuhusu amri ya dhahabu – mtendee mwenzako kama upendavyo kutendewa – Agano Jipya. Agano la Kale limeweka amri hii kinyume chake – Tobia 4:15 ‘usimtendee mtu usilopenda kutendewa wewe’. Wafaransa wana msemo kuwa hakuna adui mdogo. Hivyo kila mtu ajitahidi asiwe na adui. Na Waitaliano husema ampataye rafiki amepata dhahabu ya kweli. Mwandishi Eugene H. Maly katika kitabu chake ‘THE WORD ALIVE’ Reflections and Commentaries on the Sunday Readings – Cycles A.B.C katika tafakari ya Neno la Mungu dominika hii ya leo anaelezea maana ya andiko hili akiangalia mtazamo wa kihistoria.

Inaonekana kuwa kuna mwingiliano wa uelewa au mkazo kati ya ni kipi kinatangulia kati ya imani kwa Kristo (right Orthodoxy) na utendaji bora (right conduct). Je, kwa mkristo ni kipi kinatangulia kwanza kati ya haya mawili, yaani kumwamini Kristo kwanza au kumpenda jirani kama tunavyojipenda wenyewe? Kadiri ya Agano Jipya inaonekana kuwa imani inatakiwa kwanza. Mtume Paulo akiandika kwa Wakorintho anasema – ‘hakuna awezaye kusema Yesu ni Bwana isipokuwa katika Roho Mtakatifu – 1Kor. 12:3’. Na katika 1Yoh. 5:1 – tunasoma kuwa ‘kila asadikiye ya kuwa Yesu ni Kristo ana asili yake katika Mungu. Na kila ampendaye Baba, ampenda pia aliyezaliwa naye’. Pia katika 1Yoh. 5:5 tunasoma ‘ni nani awezaye kuushinda ulimwengu isipokuwa yeye asadikiye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu?’ Kwa hiyo Mtume Paulo anasisitiza imani kwanza kwa Kristo - (right orthodoxy).

Kwa upande mwingine tukisoma mahali fulani katika Injili ya Mathayo hasa tukisoma mfano maarufu katika 25:31-46; … atakapokuja … ataweka kondoo mkono wa kulia …. tunaona kuwa anasisitiza zaidi utendaji bora (right conduct). Katika mfano huu Yesu anaonekana kama hakimu-mfalme katika mwisho wa nyakati. Wana taalimungu wanakubali kuwa uhusiano wa karibu upo kabisa kati ya hizi pande mbili. Wakati mfano toka Injili ya Mathayo 25:31-46 waonesha kuwa asiye mkristo aweza kuokolewa kwa upendo wake kwa jirani lakini iko wazi kuwa kwa mkristo, itawezekana tu kama atatenda hayo kwa jina la Yesu. Hata hivyo katika Agano Jipya huonekana wazi kuwa imani ndiyo msingi kwa ajili ya kuwapenda wengine. Mkristo anatakiwa kuthibitisha imani yake kwa matendo mema – tunaona katika waraka wa Yakobo. Yaonekana kuwa bila matendo mema orthopaxy), imani sahihi (orthodoxy) haina maana.

Kwa namna ya pekee lakini, sehemu ya Injili ya leo yasisitiza matendo (orthopaxy). Yesu anawaambia wafuasi wake mara kwa mara wawapende adui, kuwatendea mema wanaowachukia, kugeuza shavu la pili. Upendo, huruma na msamaha ni alama za ushindi za ufuasi.  Luka anaamini kuwa haya yote yatawezekana kwa vile aliyeweka haya ana uwezo huo. Kadiri ya Mtume Paulo katika Fil. 4:13 – anasema ‘naweza yote katika yeye anayeniimarisha’. Mtume Paulo alimfahamu Yesu kwa hivyo alikuwa na matumaini. Anasema wazi matendo yanatokana na imani.

Katika somo la kwanza toka kitabu cha Samweli tunaona mwandishi akihusianisha na hiki tulichoona hapo juu. Daudi anapata umaarufu kwa sababu ya ushindi wake dhidi ya adui na hata watu wanamshangaa na hivi inaongeza umaarufu wake. Pale ambapo angemtendea ubaya adui yake anaenda mbali, anaogopa kumuua mpakwa mafuta wa Bwana. Usiku ule Daud angeweza kumuua Saul. Daudi hakumtendea vibaya Saul kwa sababu za kidini. Matendo yaliandamana na imani yake. Daudi alikuwa na hofu ya Mungu.

Kwa hakika Agano Jipya limeweka msisitizo katika imani, katika kumtambua Baba na Yesu Kristo Mwanae. Mwinjili Yohani anasema yote aliyoandika lengo lake ni kusaidia mwamini kutambua kuwa Yesu ni Masiya, Mwana wa Mungu – Yoh. 20:31.  Mtu mwenye imani haba au asiyeamini kabisa ageweza kusema sasa katika mazingira haya yanayodai imani na utendaji, Yesu yuko wapi hapa ili niweze kuamini na kutenda inavyotakiwa? Mt. Teresa wa Avila anatusaidia kutoa jibu akisema; ingawa hatuna Bwana wetu kati yetu katika hali ya kimwili, tunaye jirani, ambaye kwa ajili ya upendo na matendo mema, ni mzuri kama vile angekuwa ni Bwana wetu mwenyewe. Na matokeo yake ni ushuhuda kama anavyoandika Yoh. 13:35 – ‘hivyo watu wote watawatambua kuwa wafuasi wangu mkipendana.’ Hakika tukiishi katika uelewa huu hatutakuwa na maadui katika maisha yetu.

Tumsifu Yesu Kristo.

20 February 2019, 16:33