Tafuta

Vatican News
Biashara haramu ya binadamu na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo! Biashara haramu ya binadamu na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo!  (©artit - stock.adobe.com)

Biashara haramu ya binadamu: Uelewa, madhara na hatua zake!

Takwimu zinaonesha kwamba, hadi sasa kuna zaidi ya watu milioni 45 ambao wametumbukizwa katika biashara hii inayozalisha kiasi cha dola za kimarekani bilioni 32 kwa mwaka, na hivyo, kuchuana kwa karibu sana na biashara haramu ya silaha na dawa za kulevya duniani. Wanawake, wasichana na watoto wadogo ndio walengwa wakuu wa mifumo ya utumwa mamboleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo ni kati ya changamoto kubwa zinaoikabili Jumuiya ya Kimataifa katika ulimwengu mamboleo. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi sasa kuna zaidi ya watu milioni 45 ambao wametumbukizwa katika biashara hii inayozalisha kiasi cha dola za kimarekani bilioni 32 kwa mwaka, na hivyo, kuchuana kwa karibu sana na biashara haramu ya silaha na dawa za kulevya duniani.

Wanawake, wasichana na watoto wadogo ndio walengwa wakuu wa mifumo ya utumwa mamboleo, yaani: kazi za suluba, utalii wa ngono pamoja na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake. Kashfa hii imeanza kuzoeleka kati ya watu, kiasi kwamba, inaonekana kuwa ni jambo la kawaida katika maisha. Lakini, huu ni ukatili dhidi ya utu na heshima ya binadamu; ni kashfa kubwa na ni uvunjaji wa haki msingi za binadamu unaojionesha katika kiwango cha kimataifa kiasi hata cha kugusa sekta ya utalii duniani.

Hivi karibuni, Awamu ya Tatu ya Jukwaa la Utumwa Mamboleo, imeadhimishwa huko Istanbul, Uturuki kwa kuongozwa na kauli mbiu “Utambuzi, Vitendo na Madhara yake”. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli katika hotuba yake elekezi amekazia: Ujumbe wa Injili unaokita mizizi yake katika: usawa, haki, ukweli na upendo; mapambano dhidi ya vyanzo vya umaskini na mifumo ya utumwa mamboleo kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema, mchango mkubwa unaoweza kutolewa na dini mbali mbali duniani!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, Injili ya Kristo Yesu inakita mizizi yake katika misingi ya usawa, haki na ukweli kama njia ya kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu; daima utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa msukumo wa pekee. Uchu wa mali, madaraka na heshima, ni kati ya vishawishi ambavyo vimeendelea kumwanadama mwanadamu katika historia ya maisha yake, kiasi hata cha kuwatumbukiza wengine katika majanga na maafa. Injili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu inapania pamoja na mambo mengine kufyekelea mbali vyanzo vya umaskini wa hali na kipato, ili kumrejeshea tena mwanadamu hadhi, heshima na utu wake, kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Upendo wa Kristo, umewawajibisha Wakristo wengi kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kujitakasa na kuanza kujifunza kutenda mema; kwa kutoa hukumu ya haki; kwa kuwalinda na kuwatetea maskini na wanyonge katika jamii. Kuna watu wanaoteseka kutokana na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo! Huu ni wakati wa kusimamia ukweli na uwazi, ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kupambana na uhalifu huu wa kimataifa, unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu!

Umaskini ni matokeo ya uchoyo, ubinafsi na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu; uchu wa mali, madaraka na umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko na matokeo yake ni kuibuka kwa mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo, kielelezo cha uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu! Ubaguzi wa rangi, ulaji wa kupindukia, uchoyo na ubinafsi ni hatari sana kwa ustawi na maendeleo ya wengi. Dini mbali mbali duniani zinapaswa kuunganisha nguvu ili kupambana na utumwa mamboleo kwa kujikita katika misingi ya haki na amani; upatanisho na mshikamano pamoja na kuendelea kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mifumo ya utumwa mamboleo inakwenda kinyume kabisa na misingi ya Injili ya Kristo Yesu na Kanisa lake!

Chanzo kikuu kinachopelekea kukua na kupanuka kwa biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo ya utumwa mamboleo ni umaskini wa hali na kipato; lakini kubwa zaidi ni kwamba, hizi ni dalili za kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema. Watu wanaotumbukizwa kwenye utumwa mamboleo ni wale wanaokabiliwa pamoja na mambo mengine na baa la ujinga, ukosefu wa fursa za ajira au majanga asilia yanayowafanya kutafuta kwa udi na uvumba: hifadhi, usalama na matamanio ya maisha bora zaidi. Kuna uhusiano mkubwa kati ya vita, ghasia, biashara haramu ya binadamu pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Makundi ya wahalifu wa kimataifa wameendelea kupandikiza mbegu ya chuki na uhasama kati ya watu na hivyo kusababisha vita, ghasia na mipasuko ya kisiasa, kikabila na kijamii hali ambayo inapelekea makundi makubwa ya watu kuzihama au kuzikimbia nchi zao wenyewe.

Shirika la Kimataifa la Wahamiaji IOM, linafafanua kwamba, biashara haramu ya binadamu inaendelea kushamiri sana duniani kutokana na wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi. Biashara hii Barani Afrika inakadiriwa kufikia kiasi cha dola za kimarekani milioni 400 kwa mwaka. Ni fedha inayolipwa kwa wafanyabiashara haramu kwa njia ya gharama za usafiri jangwani na baharini sanjari na kazi za suluba ughaibuni. Hawa ni watu kutoka: Somalia, Sudan ya Kusini, Eritrea, Mali. Senegal, Gambia, Chad, Niger na Nigeria na wengine ni wale wanaotoka Bangaladesh.

Utumwa Mamboleo

 

08 February 2019, 08:26