Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linawahimiza wananchi kulinda na kudumisha amani na utulivu kabla na baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu kutangazwa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linawahimiza wananchi kulinda na kudumisha amani na utulivu kabla na baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu kutangazwa  (AFP or licensors)

Uchaguzi Mkuu DRC: Lindeni na kudumisha amani na utulivu!

Wananchi wa DRC wanataka mabadiliko ya kweli kwa kuzingatia misingi ya kidemokrasia, vinginevyo, DRC wanasema “patachimbika sana”. Matokeo ya uchaguzi mkuu yanatarajiwa kutangazwa rasmi hapo tarehe 6 Januari 2019 ingawa hadi sasa kuna malalamiko kutoka katika vyama vya upinzani kwamba, kuna kasoro kubwa ambazo zimejitokeza katika zoezi zima la uchaguzi nchini DRC.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kamati Maalum ya Waamini Walei nchini DRC, CLC, inaitaka familia ya Mungu nchini humo, kusimama kidete, bila kusinzia, ili haki iweze kutendeka na demokrasia kushika mkondo wake, bila wajanja wachache kutaka kuvuruga amani kwa kuiba kura. Hii ni changamoto inayotolewa na Kamati hii wakati ambao zoezi zima la kuhesabu kura za uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo, tarehe 30 Desemba 2018 linaendelea. Kamati Maalum ya Waamini Walei Nchini DRC katika kipindi cha mwaka 2018 iliandaa maandamano makubwa ili kumshinikiza Rais Joseph Kabila kuondoka madarakani baada ya kukosa sifa ya kuongoza nchi kikatiba.

Wananchi wa DRC wanataka mabadiliko ya kweli kwa kuzingatia misingi ya kidemokrasia, vinginevyo, DRC wanasema “patachimbika sana”. Matokeo ya uchaguzi mkuu yanatarajiwa kutangazwa rasmi hapo tarehe 6 Januari 2019 ingawa hadi sasa kuna malalamiko kutoka katika vyama vya upinzani kwamba, kuna kasoro kubwa ambazo zimejitokeza katika zoezi zima la uchaguzi nchini DRC. Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linawahimiza wananchi kudumisha amani na utulivu kabla na baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu.

Rais Joseph Kabila anatarajiwa kung’atuka kutoka madarakani baada ya kuiongoza DRC kwa kipindi cha miaka 17. Anapania kuhakikisha kwamba, DRC inaanza mwaka 2019 kwa mapinduzi ya kidemokrasia kwa kubadilishana madaraka kwa njia ya kidemokrasia, tukio la kihistoria, kutendeka tangu mwaka 1960 DRC ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Ubelgiji! Rais Kabila anamuunga mkono aliyekuwa Waziri wa mambo ya ndani Bwana Emmanuel Ramazani Shadary, ambaye ndiye mgombea wa chama tawala. Wagombea wakuu wa upinzani ni: Martin Fayulu , ambaye afisa mtendaji wa kampuni ya mafuta na Felix Tshisekedi , mtoto wa kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi.

Wakati huo huo, Askofu mkuu Marcel Utembi Tapa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, hivi karibuni, alituma ujumbe wa mshikamano wa haki na amani, kwa familia ya Mungu nchini DRC, kwa kuonesha masikitiko yake kwa baadhi ya wananchi kutengwa katika zoezi la kupiga kura, hapo tarehe 30 Desemba 2018. Maaskofu wanasema, sababu zilizotolewa na CENI hazina mashiko, kwani tayari mbinu mkakati ulikuwa umetangazwa ili kuhakikisha kwamba, wananchi wanalindwa dhidi ya ugonjwa wa Ebola, ili waweze kushiriki katika zoezi hili la kidemokrasia, kama sehemu ya utekelezaji wa haki zao msingi kikatiba!

Maaskofu pia wanapenda kuungana na wananchi wa Yumbi walioathirika kutokana na vurugu zilizojitokeza na kusababisha makazi kadhaa ya watu kuchomwa moto! Maaskofu wamelaani vitendo hivi kwa kusema kwamba, maisha ya binadamu ni matakatifu yanapaswa kulindwa, kuendelezwa na kudumishwa. Maaskofu wanaitaka Serikali kuhakikisha kwamba, inatekeleza vyema dhamana na wajibu wake wa kuwalinda raia na mali zao.

DRC: Uchaguzi Mkuu

 

03 January 2019, 09:39