Tafuta

Vatican News
Imani ni chanzo cha uzima wa milele; Kristo ni Nabii wa Agano Jipya na waamini kwa njia ya Ubatizo wanashiriki: Unabii, Ufalme na Ukuhani wake! Imani ni chanzo cha uzima wa milele; Kristo ni Nabii wa Agano Jipya na waamini kwa njia ya Ubatizo wanashiriki: Unabii, Ufalme na Ukuhani wake!  (ANSA)

Tafakari ya Neno la Mungu: Jumapili III ya Mwaka C: Unabii

Mama Kanisa anafundisha kwamba, imani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ni chanzo cha uzima wa milele. Kristo Yesu ni Nabii wa Agano Jipya na la Milele. Waamini kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wanashiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo! Kumbe, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa maneno na matendo!

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.

Ndugu mpendwa, karibu tena katika tafakari ya neno la Mungu dominika hii ya kawaida ya tatu ya mwaka. Dominika iliyopita tulialikwa na kuambiwa kuwa tukitaka kutenda miujiza basi hatuna budi kuwajali wengine. Na tukaona jinsi Yesu alivyowajali wengine kwa kuwatimizia mahitaji yao. Kwao ukawa muujiza mkubwa. Hivyo basi nasi leo tukitaka kufanya miujiza, hatuna budi kuwajali wengine kwa kutambua mahitaji yao na kuwasaidia. Leo twaona Yesu akiweka wazi sababu na nguvu ya utume wake. Aidha katika Injili ya Luka hatuna maelezo ya pekee juu ya utoto wa Yesu, ubatizo wake, siku arobaini jangwani kama ilivyo kwa Yohani ila twaona mara akiwa katika utume wake hadharani, akihubiri ufalme wa Mungu huko Galilaya. Luka akifanana na Marko, amwonesha Yesu akifanya utume wake Galillaya na akiwa safarini kuelekea Yerusalemu, atakapohitimisha utume wake.

Fundisho la Yesu katika Sinagogi la Nazareti kuhusiana na Agano la Kale na himizo la Luka juu ya desturi za zamani, yaonesha kuwa dini kubwa zaweka kumbukumbu na uhusiano na mila na desturi za zamani. Jamii iliyo hai huweka kumbukumbu za vyanzo vyake. Somo la kwanza laeleza mchakato wa kujenga Yerusalemu mpya, baada ya uhamisho wa Babeli. Watu waliotoka utumwani wakiwa bila kumbukumbu ya desturi zao, wanashangaa pale Ezra anapowasomea kitabu cha sheria. Walijisahau na wanalia wanaposikia Ezra akiwasomea na kuwaelezea maana yake. Kinachoonekana hapa ni kuwa  ni katika Roho twaweza elewa Neno la Mungu ili Roho zetu zioshwe na macho yetu kuangazwa. Kazi ya Ezra ilikuwa kulijenga upya hekalu na kutoa maana mpya ya fundisho la Neno la Mungu.

Katika injili, Luka anaweka wazi kuwa injili anayohubiri Yesu ni ushuhuda wa imani iliyoletwa katika jamii – I Kor. 15: 1-11 – iliyoletwa kwao na wale walioshuhudia na kuhudumia neno. Luka mwongofu, msomi, akijua mahitaji ya waongofu wapya  wa ukristo anaweka wazi mambo muhimu yanayoonekana na kupatikana katika injili – furaha ya imani, baraka ipatikanayo katika sala, nafasi ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu ya kikristo, nafasi ya wanawake katika maisha ya hadharani ya Yesu na nafasi ya maskini katika ufalme wa Mungu.

Kilele cha injili kipo katika tamko la Yesu anayeleta matumaini hai kwa Israeli ya zamani. Hapa twaona nguvu ya Roho Mtakatifu katika maisha ya hadharani ya Kristo. Kwa njia ya huyo roho analeta habari mpya na uhuru kwa wafungwa. Kama ilivyo katika Injili, somo la pili laonesha kuwa huyo apatikanaye katika ubatizo, yaani roho, ndiye ajengaye umoja wa kanisa. Wingi wa utajiri wa viungo vyetu waunganishwa na huyo roho. Sisi hatuna budi kuungana katika huyo Roho na kama alivyofanya Bwana ili tuendelee kuujenga huo ufalme.

Anasimulia Padre Edward Hayes, M.M, katika kitabu ‘Hadithi za Kiafrika’ katika ushuhuda – sisi waafrika hutumia vichwa vyetu. Kisa hiki kilimpata padre Edward wakati gari lake lilipoharibika barabarani akiwa na wageni waliomtembelea toka Marekani. Gari lake lilizimika ghafla barabarani. Namna pekee ya kutaka kugundua shida ilikuwa ni kutumia kitabu mwongozo (manual book) ili kugundua tatizo. Anasema alitumia muda mrefu akijaribu kusoma kile kitabu mwongozo ili kugundua tatizo lakini hakuweza kugundua tatizo. Anasema hatimaye liliwasili lori likiendeshwa na dereva Mwafrika mtu wa makamo. Yule dereva alisimama ili kutoa msaada.

Padre Edward akamweleza yaliyomsibu. Wakati padre Edward akiendelea kupekua kitabu chake yule dereva aliingia uvunguni mwa gari kuangalia sababu ya tatizo. Mara yule dereva akatoka uvunguni mwa gari akicheka akiwa ameshagundua tatizo na akiwa ameshatengeneza lile gari na mara akapiga moto na gari kuwaka. Padre akajibu, mbona sisi tumeshindwa kupata jibu pamoja na kuwa na kitabu mwongozo? Yule dereva akajibu, ‘wageni wanaweza kutumia kitabu, lakini sisi Waafrika hutumia vichwa vyetu’.

Ndugu zangu, vitabu vimeandikwa lakini yatabaki tu kuwa maandishi kama vichwa vyetu, iwapo uelewa wetu hautawekwa katika matendo. Tumeona hili katika somo la kwanza, injili na mfano wa padre Edward. Wale Waisraeli walikuwa na sheria nzuri sana tena zilizoandikwa. Bahati nzuri Ezra anazieleza vizuri kwa watu na tunasikia kuwa watu walitoa machozi. Kumbe walikuwa na sheria nzuri zilizowaweka karibu kabisa na Mungu lakini hawakuzielewa na wakaishia utumwani. Walikosa maelezo fasaha ili kuwasaidia kuelewa mapenzi ya Mungu. Tunaona pia kuwa Bwana wetu Yesu Kristo aliishi zile sheria za Kimungu na akaweka maana mpya katika zile sheria za kale. Waliomsikiliza wakapona.

Mwinjili Luka aliandika vizuri na kuwaeleza watu wake habari ya mapenzi ya Mungu. Yule dereva aliingia uvunguni mwa gari. Bila shaka alifanya hivyo kwa vile alishapata elimu ya kitabu. Akaweka katika matendo. Gari likapona na wasafiri wakaendelea na safari yao. Sisi pia hatuna budi leo kuweka katika matendo sheria ya Mungu kama tunavyoifahamu ili wengine waifahamu, vinginevyo itabaki kuwa maandishi tu. Yesu alishaweka katika matendo. Hatuna budi kujiongeza katika ufahamu wetu na wito wetu wa kutimiza mapenzi yake Mungu.

Ili kufuata mfano wa Yesu na Paulo, ni lazima kuongeza imani yetu kwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Hatuna budi kumpenda Roho Mtakatifu kama mgeni rasmi wa roho zetu, kiongozi na mtengenezaji wa ukuaji wa kiroho. Hivyo tunaimarishwa na neema zake na tukiwa na huyo roho tuna uhakika kuwa tutabaki waaminifu katika utume wake Kristo. Hivyo neno hili la leo latukumbusha juu ya nafasi ya roho katika maisha yetu ya ukristo ambapo sisi tunakuwa wajumbe wake Kristo katika ulimwengu wetu huu na kati ya watu wake. Neno la Mungu linaposikika halina budi kugusa maisha yetu na hali zetu na kuleta mageuzi chanya ambayo hutangaza kwa mapendo ufalme wa Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo.

24 January 2019, 16:04