Cerca

Vatican News
Jimbo kuu la Dodoma Tanzania linaendelea kuimarisha huduma za kichungaji kwa familia ya Mungu Jimboni humo! Jimbo Kuu la Dodoma Tanzania linaendelea kuimarisha huduma za kichungaji kwa familia ya Mungu Jimboni humo! 

Jimbo kuu la Dodoma, lilizinduliwa 18 Januari 2015! Leo?

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo Kuu la Dodoma amezindua Parokia mpya ya Mtakatifu Inyas wa Loyola, na hivyo kulifanya Jimbo kuu la Dodoma hadi mwanzo mwa Mwaka 2019 kuwa na Parokia 72. Lengo kuu ni kusogeza huduma za shughuli za kichungaji kwa familia ya Mungu Jimboni Dodoma, familia ambayo inaongezeka kutokana na kasi kubwa ya kupanuka kwa Jiji la Dodoma.

Na Rodrick Minja, Dodoma & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa, mahali pa kuinjilisha, kuwafunda na kuwatakatifuza watu wa Mungu, tayari kutoka kifua mbele kutangaza furaha ya Injili; huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa Mataifa. Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa mwaka 2018 wamekazia umuhimu wa Kanisa kupyaisha maisha na utume wa Parokia, ili kuleta mvuto na mashiko kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na waamini katika ujumla wao, ili kujenga familia ya Mungu inayowajibikiana katika: imani, matumaini na mapendo.

Parokia ni mfano mwangavu wa utume wa kijumuiya; kwa kuunganisha pamoja tofauti za watu ambao wanaishi katika eneo lake na kwa kuziingiza uwepo wao. Waamini walei wazoee kufanya kazi Parokiani bega kwa bega na mapadre wao, kuieleza jumuiya ya Kanisa matatizo yao wenyewe na ya ulimwengu, na masuala yanayohusu wokovu wa wanadamu, ili yachunguzwe na kutatuliwa kwa mchango wa wote; wazoee pia kujitoa kwa bidii, kulingana na uwezo wa kila mmoja, kwa tendo lolote la kitume na la kimisionari la jamaa yao ya kikanisa.

Hivi karibuni, Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo Kuu la Dodoma amezindua Parokia mpya ya Mtakatifu Inyas wa Loyola, na hivyo kulifanya Jimbo kuu la Dodoma hadi mwanzo mwa Mwaka 2019 kuwa na Parokia 72. Lengo kuu ni kusogeza huduma za shughuli za kichungaji kwa familia ya Mungu Jimboni Dodoma, familia ambayo inaongezeka kila kukicha kutokana na kasi kubwa ya kupanuka kwa Jiji la Dodoma! Yaani hadi raha ya shughuli za kichungaji!

Katika maadhimisho haya, Askofu Kinyaiya ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 33, Sakramenti ya Komunio ya kwanza vijana 10 na wanandoa 8 wamerudia tena ahadi zao za ndoa ili kujenga na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kama Kanisa dogo la nyumbani, nyumba ya sala, sadaka na majiundo makini ya watoto. Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Kinyaiya amewataka waamini kuwa ni mawe hai, katika maisha na utume wao; kusaidiana na kutakatifuzana; wakijitahidi kudumu katika ahadi zao za Ubatizo na Ndoa.

Wakristo walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara wawe ni mashuhuda wa kulinda, kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Waendelee kujitajirisha kwa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa na kamwe wasikubali kuyumbishwa yumbishwa kama “daladala iliyokatika usukani! Waamini wametakiwa kushirikiana na kushikamana na viongozi wa Halmashauri ya walei pamoja na Mapadre wao; daima wakitoa nafasi kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwapyaisha na kuwategemeza katika kupanga na kutekeleza shughuli mbali mbali za kichungaji na kitume!

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 6 Novemba 2014 alilipandisha hadhi Jimbo Katoliki la Dodoma na kuwa Jimbo kuu la Dodoma linalojumuisha majimbo ya Singida na Kondoa. Baba Mtakatifu akamteua Askofu Beatus Kinyaiya kuwa Askofu mkuu wa kwanza wa Jimbo kuu la Dodoma, Tanzania. Kabla ya uteuzi huu, Askofu Kinyaiya alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki Mbulu. Jimbo kuu la Dodoma likazinduliwa rasmi tarehe 18 Januari 2015.

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya alizaliwa kunako tarehe 9 Mei 1957 huko Shimbwe, Jimbo Katoliki la Moshi. Baada ya masomo na malezi yake ya kitawa, akaweka nadhiri kunako tarehe 5 Juni 1988. Tarehe 25 Juni 1989 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 22 Aprili, 2006, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akamteua kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbulu na kuwekwa wakfu tarehe 2 Juni 2006 kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbulu.

Jimbo kuu la Dodoma
18 January 2019, 16:25