Tafuta

Vatican News
Fumbo la Umwilisho ni kielelezo cha unyenyekevu, upendo, ukuu na utukufu wa Mungu unaofumbatwa katika maisha ya binadamu! Fumbo la Umwilisho ni kielelezo cha unyenyekevu, upendo, ukuu na utukufu wa Mungu unaofumbatwa katika maisha ya binadamu!  (ANSA)

Noeli: Ushuhuda wa unyenyekevu, ukuu na upendo!

Katika Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu amejivika hali ya mtoto mdogo na kuambata fadhila zake, ili kuwa kweli Emmanuel, kiasi kwamba, amekuwa karibu sana na waja wake. Imani kwa ukuu na utukufu wa Mungu inaleta mageuzi makubwa kwa kuwa ni chombo cha upatanisho kati ya Mungu na binadamu; upatanisho kati ya mbingu na nchi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwa neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu hata mwaka 2018 waamini wamekirimiwa tena fursa ya kuadhimisha Noeli, Sherehe ya Kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Neno wa Baba wa milele anayekuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Hili ni Fumbo kuu la unyenyekevu wa Mungu anayekuja kufukuzia mbali giza la dhambi na mauti, tayari kumwangazia mwanadamu, Mwanga angavu ili aweze kutembea kama mtoto wa mwanga. Neno wa Mungu anajitwalia hali ya binadamu na kuwa sawa na binadamu katika mambo yote isipokuwa dhambi, mchakato unaowawezesha hata binadamu kuwa ni wana wateule wa Mungu.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2018 kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol. Anaendelea kufafanua kwamba, katika Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu amejivika hali ya mtoto mdogo na hivyo kuambata fadhila zake, ili kuwa kweli Emmanuel, yaani Mungu pamoja na watu wake, kiasi kwamba, amekuwa karibu sana na waja wake kiasi hata cha kuwa ni mmoja ya wanafamilia. Imani kwa ukuu na utukufu wa Mungu inaleta mageuzi makubwa kwa kuwa ni chombo cha upatanisho kati ya Mungu na binadamu; upatanisho kati ya mbingu na nchi.

Neno wa Mungu aliyefanyika mwili ni ukweli na uzima; ni mkombozi anayemwokoa mwanadamu kutoka katika changamoto zinazoendelea kumwandama kutokana na ubinafsi na uchoyo wake; ili aweze kuambata na kutembea katika haki na ukweli wa maisha. Tabia ya ukanimungu inayojielekeza zaidi katika kuukataa Umungu wa Kristo na Umama wa Bikira Maria ni changamoto zinazofumbatwa katika nguvu ya kiuchumi; kielelezo cha jeuri na kiburi cha binadamu cha kudhani kwamba, anaweza kujiokoa mwenyewe hata bila ya msaada wa Mungu; ni ugonjwa wa kutaka raha mustarehe kwa kupindisha upendo wa kweli na hatimaye, kutopea katika mambo yanayokinzana na kanuni maadili na utu wema.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, hii ndiyo tabia ya walimwengu mamboleo wanaotaka kuadhibu mwili kwa kisingizio kwamba, umegeuka kuwa ni nyumba ya shetani. Kimsingi, hawa ni watu wanaodhani kwamba, tayari wamekwisha kuwa watakatifu na wao ndio wenye ufunguo wa kweli zote za maisha ya binadamu. Hizi ni dalili za misimamo mikali ya kidini na kiimani inayorutubishwa kwa dhana potofu ya kilele cha maendeleo na matokeo yake ni vita, mipasuko na misigano katika medani mbali mbali za maisha; kihistoria, kitamaduni na kiustaarabu, ili kujijengea uhuru usiokuwa na mipaka.

Imani ya Kikristo inakiri uweza wa Mungu kumwokoa na kumkomboa mwanadamu, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma na upendo wake wa dhati kwa binadamu; upendo unaofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho na waamini kwa njia ya Fumbo la Umwilisho wanafanyika kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wake yaani Kanisa, kielelezo cha Umungu na ubinadamu wa Kristo. Kanisa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo; mahali pa wokovu wa pamoja. Kwa njia ya Kanisa, Kristo Yesu ameonesha kuwa Mtu kweli na Mungu kweli; kielelezo cha uhuru na matumaini ya Ufalme wa Mungu. Kanisa ni mahali pa kutekeleza uhuru wa kweli, unaowakirimia wote maana ya uhuru katika maisha yao.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anaendelea kufafanua kwamba, upendo wa Mungu unavuka mipaka, kwani Mwenyezi Mungu kwa kumtuma Mwanaye wa pekee, ni kutaka watu waweze kumwilisha pendo lake katika maisha yao kwa kutambua kwamba, Mungu ndiye aliyewapenda kwanza na hivyo, hata wao wanapaswa kupendana na kusaidiana. Ukweli huu unaookoa unapaswa kushuhudiwa na waamini katika maadhimisho ya Sherehe za kuzaliwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Huyu ni Mwana wa Mungu anayekuja kuwatembelea waja wake kutoka juu, kama kielelezo cha utimilifu wa nyakati.

Kipindi cha Sherehe za Noeli ni muda ambao waamini wanapaswa kujifahamu na kuendelea kumshukuru Mungu kwa ukuu na utukufu wake, daima kwa kushuhudia ukweli wa Fumbo la Umwilisho katika maisha ya Kristo. Ni mwaliko wa kujenga na kudumisha utandawazi wa upendo na mshikamano, kwa kumweka Kristo Yesu kuwa ni kiini cha Noeli badala ya kumezwa na malimwengu kwa kujitakia umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko! Ni muda muafaka wa kuganga na kuponya:vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kwa kutambua kwamba, hata leo hii, Mtoto Yesu bado anaendelea kuteseka sehemu mbali mbali za dunia!

Neno wa Mungu aliyefanyika mwili ni ukweli mfunuliwa, unaowawezesha waamini kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu na kuendelea kujitakatifuza, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni: Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho na nyakati zote ni zake. Kanisa litaendelea kuwa ni mahali pa kuwatakasa na kuwatakatifuza waamini; mahali muafaka pa kupyaisha maisha ya watu na ulimwengu katika ujumla wake; ni mahali pa ushuhuda wa Kiinjili na kiekumene ili kushirikishana zawadi za Mungu kwa waja wake yaani: upendo, haki, amani na upatanisho, nguvu ya ufufuko na matumaini ya uzima wa milele. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwendea Bikira Maria na kumsujudia Mtoto Yesu; Neno wa Mungu aliyefanyika mwili; kwa kuwakumbuka na kuwaombea watoto wote wa Kanisa. Anawatakia wote heri, baraka na furaha tele kwa Mwaka mpya 2019.

Bartolomeo: Noeli 2018
24 December 2018, 13:41